TUDUMISHE KISWAHILI
Copyright Selina L. P. Mushi, Ph.D. 1996 University of Toronto
Maelezo:
Shairi hili limetungwa na Dr. Selina Mushi, na kuimbwa na Doris Puja na Regina Shayo, katika mkutano wa kwanza (wa jumla) wa JUKUTA, uliofanyika katika chumba cha tafrija, jengo la 30 Charles West, Toronto, Canada, tarehe 23/3/1996. JUKUTA ni Jumuiya ya Kukuza Kiswahili Toronto. Shughuli za jumuiya hii zimebuniwa na kuanzishwa na Grace Puja na Dr. Selina Mushi, Machi 1996.
Description:This is a Kiswahili poem which was composed by Dr. Selina Mushi and sang by her daughter Regina Shayo and her friend's daughter, Doris Puja as part of the Kiswahili activities in the first meeting of JUKUTA. JUKUTA is an acronym denoting a community pursuing the development of Kiswahili in Toronto.
Tudumishe Kiswahili
Kiswahili lugha yetu, tunaipenda hakika,
Ni muhimu sana kwetu, ukweli tunatamka,
Hatutakubali katu, lugha ikidhalilika,
Tudumishe Kiswahili, kwani chatuunganisha.
Utamaduni wa kwetu, kuujua ukitaka,
Pia heshima ya mtu, vile anavyojiweka,
Kiswahili huthubutu, peke yake kukiweka,
Tudumishe Kiswahili, kwani chatuunganisha.
Duniani kuna vitu, kuvitenga ukitaka,
Utashindwa katu katu, pamoja vimefungika,
Kwetu sisi lugha yetu, utamaduni hakika,
Tudumishe Kiswahili, kwani chatuunganisha.
Hapa kusimama kwetu, si kusifu tunataka,
Tuna malengo matatu, na sasa tunatamka,
Kwanza kuthamini utu, ingawa pesa twataka,
Tudumishe Kiswahili, kwani chatuunganisha.
Pili chambueni kitu, mufikie muafaka,
Siwe kama mbwa mwitu, nyama wanapoitaka,
Lugha itapiga kutu, kama ni pesa mwasaka,
Tudumishe Kiswahili, kwani chatuunganisha.
Na lengo letu la tatu, watoto kufurahika,
Na ninyi wazazi wetu, pamoja kujumuika,
Ifikapo Jumatatu, msingi umejengeka,
Tudumishe Kiswahili, kwani chatuunganisha.
Tujuavyo wengi wetu, lugha imechanganyika,
Kimtang'ata Kitumbatu, Kiswahili chasikika,
Sanifu ndo nia yetu, sio lugha pata shika,
Tudumishe Kiswahili, kwani chatuunganisha.
Hivi leo ni mwanzo tu, taratibu tutafika,
Lugha hii ya Kibantu, duniani itashika,
Kama moto wa msitu, pote itafahamika,
Tudumishe Kiswahili, kwani chatuunganisha.
Hapa ni kikomo chetu, tamati tumeshafika,
Twawapa shukrani zetu, hapa kwa kukusanyika,
Yatia moyo wenzetu, mwito mlivyoitika,
Tudumishe Kiswahilli, kwani chatuunganisha.
Tunajidai mwakwetu, kwa maringo twaondoka,
Ni utamaduni wetu, Kiswahili twakishika,
Hiki ndo kilicho chetu, sikia tukitamka,
Tudumishe Kiswahili, kwani chatuunganisha.
===============================================================
Katika masomo yangu ya shahada ya juu, pamoja na mambo mengine muhimu niliyojifunza kuhusu ufundishaji wa lugha hasa kwa wale ambao tayari wana lugha nyingine, nimegundua kuwa lugha si chombo cha mawasiliano tu, si kioo cha utamaduni tu, ila ndio UTU wenyewe! Utu wa mtu unajitokeza haraka sana katika matumizi yake ya lugha, hasa lugha inayoambatana na utamaduni wake. Lugha pia inaweza kuwa chombo cha ukandamizaji na, hasa katika dunia ya "kunyang'anyana" kama tuliyo nayo wakati huu. Wapo wazungumzaji wa Kiswahili wanaoiona lugha hii kama chombo cha kujipatia fedha kwa "kuuza" maneno machache wanayojipatia hapa na pale, na mara nyingi kuyatumia bila usahihi. Huku ni kuua lugha, siyo kuikuza! Ni wajibu wetu sisi wenye lugha kuitumia, kuitangaza, kuiendeleza na kukabiliana na madhara yanayotokana na "uuzaji" wa Kiswahili. Walio na lengo hili la kuikuza lugha ya Kiswahili, wana haki ya kujiita wenye lugha.
Mimi nadhani ingefaa viongozi wa Tanzania msisitize kuzungumza Kiswahili kila inapowezekana, mnapotembelea nchi za nje. Ni jukumu la wasikilizaji kutafuta wakalimani ili waelewe kinachosemwa. Msemaji Mtanzania kuongea lugha ambayo si yake, na hasa katika maswali yanayohusu nchi na wananchi ambao ni wazungumzaji wa Kiswahili, ni kubana kufikiri kwa msemaji kusiambatane na utamaduni wake, kwa kuwa baadhi ya maneno hayana tafsiri kamili katika lugha nyingine, hasa Kiingereza. Kufuatana na mada yenyewe, msemaji anaweza kujikuta anaweka juhudi zaidi katika matumizi sahihi ya lugha ngeni anayoitumia, na hivyo kuupa ujumbe wake, ambao ndio muhimu, nafasi ya pili.
No comments:
Post a Comment