Wednesday, March 25, 2009

KUSHINDANISHA WAKULIMA TANZANIA WATAPATA TIJA GANI?

Imeandikwa na Frank Leonard, Habari Leo, Tanzania, Machi 25, 2009.


Image

Gestula Mlelwa akionesha nyasi wanazozihifadhi kwa ajili ya malisho ya ng’ombe wao.

Kama kuna jambo ambalo halionekani, lakini lina uwezo mkubwa wa kuchochea shughuli za ufugaji na kilimo bora ni utaratibu wa kuwashindanisha wakulima kupitia sherehe za wakulima (Nane Nane). Sina hakika kama Watanzania wengi, wanafuatilia kwa makini mchakato mzima wa sherehe za Nane Nane, ambazo hufanyika Agosti 8.

Zilianza rasmi zaidi ya miaka kumi iliyopita. Wengi wanaozifahamu sherehe hizi, wanaweza wasiwe na majibu kama ukiuliza kwa nini kuna sherehe hizo kila mwaka. Jibu la haraka unaloweza kupewa na watu wengi wasiofuatilia mchakato wake, linaweza kuwa hizi ni sherehe tu za kitaifa, na tena zinazowahusu wakulima wanaozitumia kuonyesha na kuuza wanachozalisha, kutokana na shughuli zao za kilimo.

Nilibaini ukweli wa jibu hilo kwamba hauishii hapo, baada ya kumtembelea Isaya Mlelwa na mkewe Getula Mlelwa kitongoji cha Lunyanyui kijiji cha Magoda wilaya ya Njombe mkoani Iringa. Lakini familia hii ni ya akina nani na ni kwa nini niliamua kuiandikia makala? Ukibahatika kukutana na mkulima yeyote anayefuatilia mchakato wa sherehe za Nane Nane mkoani hapa, hutachelewa kuwajua wanafamilia hao ni akina nani.

“Ni wakulima wadogo wenye umaarufu wilayani Njombe na mkoa wetu wa Iringa kwa ujumla,” anasema Christa Nanda, mkulima wa matunda aina ya tufaa.Wengine wengi utakaowauliza, hakuna shaka watakupa jibu kama la Nanda. Lakini kwa nini wakulima hao wadogo wawe na sifa hiyo, iliyosambaa kila pembe ya mkoa wa Iringa, huku tukijua kwamba zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wake wanaishi kwa kutegemea shughuli za kilimo.

Hapo ndipo nilipopata jibu, kwa nini ushindanishaji wa wakulima kimkoa kupitia Nane Nane, unaweza kuhamasisha na hatimaye kuchochea shughuli za ufugaji na kilimo bora, kitakachotoa mazao bora yanayofaa kushindanishwa katika soko lolote la mazao la ndani na nje ya nchi.

Nilipofika nyumbani kwa Mlelwa na familia yake, niliweza kuubaini umaarufu wa mfano wa familia yao. “Sisi ni wakulima bora wa mkoa wa Iringa kwa msimu wa kilimo uliopita wa mwaka 2007/2008,” anasema mkewe Mlelwa, Gestula, alipoanza kunielezea historia yao kuhusu shughuli zao za ufugaji na kilimo.

Nilijiridhisha na jibu la Mlelwa baada ya kujionea shamba lao, lenye ukubwa wa hekta nne hivi, linalozunguka nyumba yao nzuri na ya kisasa, inayotumia umeme wa gesi itokanayo na kinyesi cha ng’ombe na zizi lao, lenye ng’ombe saba wa maziwa na nguruwe na kuku wengi wa kienyeji.

Akielezea historia yao katika shughuli hizo za kilimo na ufugaji, Mlelwa anasema miaka mitatu iliyopita waliamua kuachana na matumizi ya mbolea za viwandani na kujikita zaidi kwenye kilimo hai, kinachotumia mbolea na dawa ya asilia. Anasema ubora wa mazao aliyoyaona katika moja ya sherehe za Nane Nane, ambazo katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini hufanyika mkoani Mbeya, ni moja ya sababu iliyowasukuma kuacha matumizi ya dawa na mbolea za viwandani katika shamba lao.

“Ukijituma, ukafuata ushauri wa wataalamu unaweza ukaendesha kilimo hai na kwa muda mfupi ukaona matokeo yake, kama sisi tunavyofaidika nayo,” anasema. Anasema mafanikio yao yamewezekana, baada ya kuutumia vyema ushauri na mafunzo kwa vitendo kutoka kwa maofisa ugani wa Halmashauri ya Mji wa Njombe kupitia Mradi wa Maendeleo ya Mipango ya Kilimo Wilayani (DADPs).

Anasema katika kilimo hicho hai, walianza na shughuli ya ufugaji kwa kununua ng’ombe watatu wa maziwa, nguruwe watatu na kuku wengi wa kienyeji, ambao wameendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka. “Kinyesi cha mifugo hiyo pamoja na mbolea tunayotengeneza wenyewe kwa kutumia takataka, nyasi na mabaki ya vyakula vya mifugo, ndicho tunachotumia katika shamba letu,” anasema.

Anasema pamoja na kutengeneza samadi, wameweza kujenga mtambo wa kuzalishia umeme kwa kutumia kinyesi. Umeme huo wanaoutumia kwa matumizi yao mbalimbali ya nyumbani. Aidha anasema kwa msaada wa watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine, wameweza kubaini aina mbalimbali za miti asilia, wanayoitumia kutengeneza dawa zinazodhibiti magonjwa ya mimea.

“Kwa hiyo tunachozalisha kutoka katika shamba letu kina miujiza kwa sababu hatutumii kabisa kemikali za viwandani,” anasema. Mlelwa anasema katika shamba hilo, wanalima mahindi, viazi na aina mbalimbali za mboga. Anasema tangu waanze kutumia mbolea na dawa asilia, mazao wanayozalisha yameongezeka maradufu na hivyo kuwaongezea kipato zaidi.

Anasema wakati katika hekta moja, walikuwa wakipata gunia nane za mahindi, hivi sasa wanapata gunia 14.Kwa upande wa viazi, walikuwa wakipata gunia 30 kwa hekta, lakini hivi sasa wanapata gunia 70. “Hatuishii hapo, tutaendelea kuutumia ushauri wa kitaalamu ili tuzalishe zaidi ya kile tunachozalisha hivi sasa,” anasema.

Hata hivyo anasema pamoja na kuwepo kwa masoko ya uhakika kwa kile wanachozalisha, wamedhibiti bei ya mahindi, huku bei ya viazi ikipanda na kushuka kulingana na mahitaji yake na uharaka wake katika soko. “Soko la viazi bado lina matatizo yake, wakati mwingine unalazimika kukubaliana na bei za walanguzi, ili viazi visikuozee, tofauti na mahindi,” anasema. Mahindi wamekuwa wakiuza debe moja kwa Sh 5,000, hata kama wanaotumia dawa za viwandani, wanauza pungufu ya bei hiyo.

Kwa upande wa ng’ombe, anasema watatu kati ya saba wanawakamua maziwa yanayowapatia kipato zaidi cha kumudu gharama zao za maisha, zikiwamo za kusomesha watoto wao. “Kila ng’ombe anatoa lita 22 za maziwa kila siku, kwa hiyo kwa ng’ombe watatu tunapata lita 66 za maziwa kila siku, ambayo tunauza kwa Sh mia tano kwa lita moja,” anasema na kuongeza kwamba kati ya lita hizo, lita 60 wanauza na zinazobaki wanazitumia kwa matumizi yao ya nyumbani.


Anasema kutokana na mauzo ya lita 60, familia yao inapata Sh 30,000 kila siku na hivyo kuwafanya wajipatie Sh 900,000 kila mwezi. “Tulipoamua kujiingiza kwenye kilimo hai, tulianza na ufugaji, baadaye tukaingia kwenye kilimo chenyewe na baadaye kwa msaada wa wadau wengine tukaanza kuzalisha nishati ya umeme wa gesi asilia (bio-gas).

Haya ni mafanikio makubwa tunayoendelea kupata tangu tuanzishe kilimo hiki hai,” anasema. Anasema kwa kutumia kipato hicho, wameweza kujenga nyumba ya kisasa kijijini hapo, ambayo ina umeme wa gesi asilia na mipango yao ya baadaye ni kununua trekta sambamba na kuongeza ukubwa wa shamba na mifugo yao.

Anasema wakati wa jitihada zao zote hizo, hawakujua kama itakuja siku watakuwa wakulima bora wa mkoa wa Iringa. “Tuliingia katika kilimo hiki kwa lengo la kuonyesha na kushindanisha bidhaa tunazozalisha kwenye masoko, hatukuwahi kujua kama siku moja tungepata heshima hii tuliyopata.

Hali hii inatupa changamoto ya kuboresha zaidi kilimo chetu. Tunatoa mwito kwa wakulima wengine kuiga mfano huu ili wasiende kwenye sherehe za Nane Nane kwa lengo la kuonyesha na kuuza tu bidhaa zao, lakini waende huko wakijua wana changamoto kubwa ya kuboresha ubora wa bidhaa zao,” anasema. Anasema kutokana na kupata ushindi huo, walizawadiwa pampu ya maji, aina ya moneymaker yenye thamani ya Sh 80,000.

Akizungumzia mchakato wa kumpata mkulima bora, Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Iringa, Shaniel Nyoni, anataja taratibu zinazotumika kumpata mkulima bora wa mkoa, kwamba zinazingatia vipato vyao, ushauri wa kitaalamu wanaoupata na jinsi wanavyoutumia kuboresha kilimo chao. Nyoni anasema kila wilaya, baada ya kujiridhisha na vigezo hivyo, inatakiwa kuteua washiriki watatu ambao hutembelewa na idara ya kilimo ya mkoa kujionea hali ya uzalishaji wao katika kilimo na mifugo.

Baadaye, wakulima hao hugharimiwa na kupelekwa kwenye sherehe hizo za Nane Nane, wakiwa huko hufanyiwa tathmini ya mwisho inayotoa mkulima bora. Nyoni anasema ushindanishaji wakulima umeongeza hamasa kwa wakulima kufanya bidii katika kilimo chao na utafutaji wa fursa ya kukutana na wakulima wa mikoa mingine kupata uzoefu wao. Anasema kwa kupitia DADPs wilaya zote, zimekuwa zikipata fedha kwa ajili ya maendeleo ya shughuli za ufugaji na kilimo.

“Kwa kupitia mradi huu, wakulima wamekuwa wakijengewa uwezo ili watumie mbinu za kitaalamu katika shughuli hizo, lakini pia DADPs inatoa fedha kwa ajili ya miradi ya uwekezaji kama ujenzi wa masoko na machinjio ya kisasa,” anasema. Anawataka wakulima wengine mkoani Iringa, kuzingatia ushauri wa kitaalamu wanaopewa ili wanufaike kama inavyonufaika familia ya Mlelwa.

No comments:

Post a Comment