Thursday, March 19, 2009

DR. MWAKYEMBE AJIBU MAPIGO YA KUMCHAFUA

Dk Mwakyembe ajibu mapigo tuhuma za kumchafua kisiasa - Gazeti la Mwananchi

Date::3/18/2009
Dk Mwakyembe ajibu mapigo tuhuma za kumchafua kisiasa
Na Ramadhan Semtawa

MBUNGE wa Kyela na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini Dk Harrison Mwakyembe, amekiri kuwa mmoja wa wanahisa wa Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Power Pool East Africa Limited, huku akisisitiza kuwa hakuna mgongano wa kimaslahi.
Kauli hiyo ya kwanza ya Dk Mwakyembe kukiri kuwa mwanahisa wa Kampuni hiyo ya kuzalisha umeme wa hewa, imekuja wakati sakata hilo likionekana kama tuhuma mpya ambayo ni kete mbaya kisiasa kwa mbunge huyo.

Naibu Spika Anna Makinda, alipoulizwa kama kitendo hicho cha mbunge huyo ambaye alichunguza mkataba tete wa Richmond kinaweza kusababisha mgongano wa maslahi alijibu: "Bwana mwandishi sitaki majungu”.

Makinda alisema kwa kifupi kwamba, taarifa kuhusu Mwakyembe hajazipata kwa undani, hivyo akijadili kitu kabla ya hajaelewa kwa undani ni sawa na majungu.
Kwa upande wake Dk Mwakyembe akitangaza uanahisa wake katika mkutano maalumu na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Dk Mwakyembe alikiri uwepo wa kampuni hiyo lakini akisisitiza ni kwa maslahi ya taifa huku akigoma kutangaza maslahi kwani mradi huo haujaanza.

Dk Mwakyembe alipoulizwa iwapo alikuwa tayari kutangaza maslahi yake kwa Watanzania kutokana na kuwa na mradi ambao uko katika sekta ambayo yeye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati Nishati na Madini, alijibu: "Kutokana na usomi wangu, siko tayari kufanya hivyo, siwezi ku-declare interest (kutangaza maslahi) katika mradi ambao haujaanza, ni sawa wewe mkeo awe na mimba halafu useme atazaa mtoto Profesa".
Katika mkutano huo, Dk Mwakyembe alisisitiza kwamba, kampuni hiyo inaundwa na wazalendo ambao wameangalia maslahi ya taifa.

Dk Mwakyembe, alisema Watanzania wazalendo wakiwemo wasomi wa vyuo vikuu na watu wa kada tofauti, walibuni mradi huo kutokana na kuona nchi inaumizwa na tozo la gharama za maunganisho (Capacity Charge).

Akijibu maswali huku akitumia muda mwingi kuelekeza makombora kwa baadhi ya wanasiasa, wakati mwingine akimtaja zaidi Mbunge wa Igunga Rostam Azizi kuhusika kumchafua kupitia vyombo vyake anavyomiliki, alisema mradi huo ukija kuanza hakutakuwa na tozo la maunganisho ya umeme.

"Kuna watu ambao tayari wamechafuka nao wanataka kuchafua wenzao, Rostam Azizi vyombo vyake ndivyo vinanichafua, hana uadilifu wa kunichafua," alirusha kombora hilo kwa Rostam.

Rostam alipoulizwa na gazeti hili kwa njia ya simu, alisema ameona tuhuma dhidi ya Dk Mwakyembe kupitia vyombo vya habari na hivyo hawezi kujibizana naye.
Hata hivyo, Rostam alisema ni vema Dk Mwakyembe angejibu tuhuma au hoja zilizombele yake kuliko kuanza kushambulia watu wengine nje ya hoja na kutafuta mchawi.

"Ndugu mwandishi, hayo mambo kuhusu Dk Mwakyembe nimesikia na kusoma kupitia vyombo vya habari, sasa pia ndiyo nasikia kwamba Dk Mwakyembe kanitaja namchafua," alisema Rostam na kuongeza:

"Nafikiri, sina haja kujibizana naye, lakini jambo moja tu la msingi ni vema akajibu hoja zinazoulizwa kuliko kuanza kumtafuta mchawi," alijibu kwa kifupi.
Rostam akisema hayo, Dk Mwakyembe alisema kampuni hiyo tayari imepata ardhi ya kuanzia Mkoani Singida ambako wananchi wazalendo wameamua kujitolea.

Akifafanua, Dk Mwakyembe alisema wananchi hao wazalendo waliamua kutoa ardhi hiyo ili mradi huo uweze kukamilika.

Mbunge huyo machachari, alipoulizwa ni lini hasa atatangaza maslahi kutokana na mradi huo, alisema ni hadi pale utakapooanza kuzalisha.
"Hapa wengi wenu mnaweza mkawa mumesajili magazeti, lakini hayajaanza kufanyakazi hivi mnaweza kujitokeza na kutangaza maslahi yenu hadharani kwa mfano, ikihitajika?" alihoji.
Alisema wapo watu ambao dhahiri hawawezi kupenda kuona mradi huo unafanikiwa, kwani watakuwa wamepoteza mabilioni yao ambayo wamekuwa wakiyapata serikalini kutokana na tozo la maunganisho.

Kuhusu kwanini wamekuwa wakitaka ununuzi wa mitambo ya IPTL lakini wakikataa ya Dowans, alijibu : "jamani, hivi ni vitu viwili tofauti kabisa."
Dk Mwakyembe alifafanua utofauti huo, akitaja mambo mawili ambayo yamekuwa yakifanya wabunge washinikize ununuzi wa mitambo ya IPTL, ambayo kwanza, IPTL ilikuwa na mkataba na serikali ambao ilikuwa ikilipwa Sh3.7 bilioni kila mwezi, kiasi ambacho ni kikubwa.

Pili, Dk Mwakyembe alisema IPTL ilikuwa inamkataba huo wa miaka 20 ambao ungeendelea kuumiza serikali katika kulipa tozo hilo.

Kuhusu kwanini wanapinga ununuzi wa mitambo ya Dowans, alisema kwanza, hakukuwa na mkataba na pili hakuna umuhimu kwani tayari kampuni hiyo ina madeni makubwa katika mabenki huku ikiwa imeishtaki Tanesco katika mahakama nchini Ufaransa.
Hatua ya Dk Mwakyembe kuanza kubanwa pia imekuja katika kipindi ambacho mjadala kuhusu ununuzi wa mitambo ya Dowansa, ukiwa juu nchini baada ya serikali kutangaza kujitoa siku chache bada ya Tanesco pia kutangaza hivyo.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi 18-03-2009

No comments:

Post a Comment