Tuesday, March 10, 2009

HABARI NJEMA KWA TANZANIA !

Date: Machi 9, 2009
Mpango wa Waziri Magufuli wanasa wavuvi haramu wa kimataifa


Walikuwa na tani 70 za samaki
Wapelekwa rumande *
Rais Kikwete ashangilia

Festo Polea na Leon Bahati

MIKAKATI ya Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, John Pombe Magufuli, kudhibiti maliasili za baharini imeanza kuonyesha makali baada ya kunasa meli iliyokuwa imebeba tani 70 za samaki waliovuliwa eneo la Tanzania kwenye pwani ya Bahari ya Hindi.

Waziri Magufuli, ambaye alipata umaarufu mkubwa wakati akitekeleza mipango ya serikali akiwa Waziri wa Miundombinu, aliagiza wafanyakazi 35 wa meli hiyo ya Tawariq I kuwekwa mahabusu wakati taratibu nyingine za kisheria zikifanywa.

“Leo nina furaha kwa kuwa maharamia hawa watalala katika jela yetu na hivyo kujua kuwa Tanzania inachukia wizi wa samaki na haina mchezo katika hilo,” Magufuli alisema akionyesha kufurahia mafanikio hayo baada ya kuhaha muda mrefu kutafuta dawa ya wezi wa maliasili za baharini.

“Walikuwa wakifanya uvuvi eneo la Tanzania kama vile ni shamba la bibi. Sasa nawafahamisha shamba la bibi halipo tena; bibi amekufa; hawa ni watoto wa bibi. Leo (jana) lazima wakalale (gerezani) Keko.”

Alisema kuwa kukamatwa kwa watu hao ni jambo la kujivunia kwa sababu kwa miaka 50 iliyopita, maharamia wamekuwa wakivua samaki kwenye pwani ya Tanzania bila kikwazo chochote, lakini akasema sasa Tanzania imeandika historia katika ramani ya kimataifa.

Alisema wanatarajia kuwafikisha mahakamani wakati wowote na kuwashtaki kwa mujibu wa sheria. Iwapo mahakama itabaini kuwa watu hao wana hatia, wanaweza kutozwa faini ya dola 20 milioni za Kimarekani au meli yao kutaifishwa ama adhabu zote kwa pamoja, kwa mujibu wa Magufuli.

Meli hiyo, ambayo ilikamatwa juzi ikiwa karibu maili 60 kutoka ufukweni, ilifikishwa Bandari ya Dar es salaam jana asubuhi.

Ilikuwa haina bendera ya nchi inakotoka na wafanyakazi wake hawakuwa na leseni wala vitambulisho na hadi jana lugha waliyokuwa wanatumia ilikuwa haieleweki.

Magufuli alisema kuwa meli iliyokamatwa haijulikani ni ya nchi gani, lakini mmoja wa vibarua wa meli hiyo aliiambia Mwananchi kuwa inamilikiwa na kampuni moja ya Taiwan, ingawa ubavuni imeandikwa Vietnam.

Mfanyakazi huyo wa meli hiyo alisema kuwa mmiliki wa kampuni hiyo ni raia wa Tawain ambaye muda mwingi huutumia nchini Kenya.

Waziri Magufuli alisema kabla hawajawekwa rumande, walitakiwa kuchomwa sindano za kinga kama ilivyo sheria ya kimataifa ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na kwamba, kati ya mabaharia 35 ni wanne tu ambao walikuwa wamepata chanjo hiyo, jambo alilosema litawafanya wawe na uangalifu mkubwa.

Kemn Govender, mkurugenzi msaidizi wa meli ya Sarah Baartman iliyokodishwa kwa ajili ya kusaka wavuvi haramu kwenye pwani ya Tanzania, alisema maharamia hao waligoma kujisalimisha hadi walipotishiwa kuwa zitatumika silaha za moto.

Govender alisema meli hiyo ilionekana juzi mchana ikiwa umbali wa maili 60 kwenye eneo la Tanzania na ndipo walipoanza kuwasiliana kwa njia ya simu, lakini hawakupata majibu yoyote kutoka kwenye meli hiyo.

“Tulipoitaka ijisalimishe, hatukupata majibu yoyote na walikuwa wamezima rada hadi tulipotaka kutumia mtutu na vyombo vya moto kukabiliana nao ndipo walipoamua kujisalimisha,” alisema Govender.

Govender alisema baada ya kufanya uchunguzi, walibaini tani 70 za samaki aina ya tuna ambao kwa kilo huuzwa kati ya Dola 8 na 10 za Kimarekani (sawa na takriban Sh13,100 za Kitanzania).

Alisema meli hiyo haina kibali wala leseni yoyote ya uvuvi na haikuwa na kitu chochote kinachoipa haki ya kufanya uvuvi na kwamba meli hiyo ilizima rada zake.

Operesheni ya kukamata meli zinazofanya uvuvi haramu kwenye pwani ya Tanzania inaendeshwa na meli ya Sarah Baartman.

Tangu kuanza zoezi la kusaka meli zinazofanya uharamia huo Februari 25, kumekuwepo na mafanikio makubwa baada ya meli nne kukamatwa. Tayari meli 31 zimeshakaguliwa na meli hiyo ya juzi ni ya kwanza kukamatwa nchini Tanzania.

Naye mmoja wa Wakenya wanaofanya kazi kwenye meli hiyo ambaye alijitambulisha kwa jina la Juma Kombo, alisema meli hiyo imekuwa ikifanya uvuvi eneo la Tanzania kwa zaidi ya miezi sita iliyopita.

Alisema meli hiyo ni maalumu kwa ajili ya uvuvi na kwamba kila baada ya siku kadhaa, meli nyingine hufika kubeba samaki wanaovuliwa na kuondoka nao, huku meli hiyo ikiendelea na kazi ya kuvua.

Akiwa na wenzake wengine wawili, Ally Ally Mkota na Sitta Walikoni kutoka maeneo ya Likon na Kisauni mjini Mombasa, alisema walichukuliwa na meli hiyo kwa muda wa miezi sita na hulipwa dola 200 kwa mwezi.

“Sisi tunafanya kazi meli hii ilituchukua tukavue na ukiangalia ugumu wa maisha na shida ya ajira tukaingia kwenye kazi ya uvuvi. Kama wana kibali ama hawana sisi hatujui tunachotafuta ni fedha. Wanatufanyisha kazi ya uvuvi na kutulipa kiwango ambacho kinaturidhisha,” alisema Kombo.

“Meli zipo zaidi ya hii ingawa ni ajabu kukamatwa kwani meli nyingi hazifiki eneo tulilokuwepo kwa sababu ni vigumu kufikika kutokana na eneo hilo kuwa la maficho sana.

"Lakini kwa kuwa meli hiyo iliyotukamata ni kubwa, waliweza kutuona na kutufikia kirahisi. Meli bado zipo nyingi wakienda tena na tena watakamata nyingine zaidi.”

Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete ameishukuru Afrika Kusini, na mabaharia wote waliofanikisha kukamatwa kwa meli kubwa iliyokuwa inavua samaki wa Tanzania kinyume cha sheria.

Meli hiyo inayoitwa Tawariq I ilikamatwa jana katika operesheni maalum iliyoshirikisha mabaharia kutoka Tanzania, Afrika Kusini, Msumbiji na Kenya.

Meli hiyo ilikamatwa katika siku ya pili ya operesheni maalum iliyoanzishwa na Tanzania kukomesha wizi wa samaki katika eneo lake la Bahari ya Hindi.

Tanzania, Kenya na Msumbiji zimetoa mabaharia wawili kila moja wakati Afrika Kusini imetoa mabahari watano.

Rais Kikwete alitoa shukurani hizo jana wakati alipokutana na mabaharia waliofanikisha kukamatwa kwa meli hiyo kubwa na akawakabidhi zawadi mbalimbali mabaharia hao.

No comments:

Post a Comment