Monday, March 23, 2009

HEKO WANAFUNZI WA KIKE LUPANGA SEKONDARI KUWAGOMEA WALIMU WAKWARE !

Date: Mon, 23 Mar 2009 15:06:43
To: <list@tanzanet.org>
Subject: [tanzanet] Wanafunzi wagomea walimu wakware


John Nditi, Morogoro
Daily News; Monday,March 23, 2009 @17:48

Wanafunzi zaidi ya 600 wa sekondari ya Lupanga mkoani hapa, wametishia
kuendeleza mgomo wa masomo wakishinikiza kuchukuliwa hatua dhidi ya walimu
watano wa kiume waliokithiri kwa vitendo vya ngono na wanafunzi wa kike.

Wanafunzi hao wamedai kuwa hawataingia madarasani kuendelea na masomo yao
hadi hatua zichukuliwe dhidi ya walimu hao, wanaodaiwa kuwa wa masomo ya
Sayansi. Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kutokea mtafaruku huo
juzi, Kiranja Mkuu wa Shule hiyo, Daniel Emmanuel, alisema wanafunzi
waliamua kugoma kuingia madarasani wakishinikiza walimu hao wachukuliwe
hatua kali za kinidhamu.

Rais huyo wa wanafunzi alisema baada ya wanafunzi wa kike kuwasilisha
malalamiko juu ya vitendo viovu vya walimu hao kwa wenzao kwa kike, waliamua
kufikisha taarifa hizo kwa Mwalimu wa Malezi na baadaye kwa Mkuu wa Shule
hiyo.

Alisema kushindwa kulipatia ufumbuzi tatizo hilo, kuliwafanya wanafunzi
walipofika shuleni asubuhi ya siku hiyo, kugoma kuingia madarasani, wakitaka
kupata majibu sahihi kutoka kwa Mkuu wa Shule. Hata hivyo, alisema kutokana
na mgomo huo, Mkuu wa Shule alilazimika kuwaamuru wanafunzi kuingia
madarasani kwa ajili ya kupiga kura za maoni juu ya walimu hao.

Kwa upande wake, Kelvin Mhinda, kiongozi wa uzalishaji shuleni hapo, alisema
walimu hao wamekuwa na tabia ya kufanya mapenzi na wanafunzi tofauti
tofauti, wakati wakijua kwa kufanya hivyo wanakwenda kinyume na maadili yao.


Nao wanafunzi, Maria Yahya na Beatrice Josephat ambaye ni Makamu Kiranja
Mkuu wa wanafunzi hao, walisema kwa nyakati tofauti kuwa baadhi ya wanafunzi
wamefikisha malalamiko hayo kwa wazazi wao. Hata hivyo, Beatrice alisema
wanafunzi wa kike wa shule hiyo wamekuwa na nidhamu katika kuzingatia
maadili na hivyo kutokana na vitendo hivyo wanavyofanyiwa wanafunzi
wamelazimika kuyafikisha mbele ya uongozi wa shule hiyo.

Akizungumzia mgomo huo, Mkuu wa Shule, Pascal Mlimbo, alikiri kujitokeza kwa
tatizo hilo na kwamba alishaanza kuchukua hatua dhidi ya walimu hao kwa
kuwaita ofisini kupata utetezi wao juu ya madai ya shutuma hizo. “Nililetewa
ushahidi juu ya vitendo vya ngono vinavyowahusu walimu wanne wa shule hii na
nikawaita na kuwaonya wasiendelee na tabia ya ukiukwaji wa maadili ya kazi,“
alisema Mkuu wa Shule.

Hata hivyo, alisema wanafunzi hao waliendelea kuwasilisha malalamiko ya
kukithiri kwa tabia za walimu hao, hali iliyowafanya wanafunzi Machi 23
mwaka huu, kugoma kuingia madarasani wakishinikiza wachukuliwe hatua za
kinidhamu. Alisema kutokana na shutuma hizo, Mkuu wa Shule hiyo aliitisha
kikao cha dharura cha walimu na kujadili jambo hilo na kuamua wanafunzi wote
kupiga kura za maoni kuhusu madai hayo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule hiyo, iliyoanzishwa mwaka 2006 kwa ajili ya
mazoezi ya walimu wanafunzi wa Chuo cha Ualimu cha Morogoro, kura hizo
zitachambuliwa na hatimaye kuwataka wahusika kutoa maelezo ya maandishi
kujibu tuhuma hizo. Alisema kimsingi, walimu kufanya mapenzi na wanafunzi ni
kosa la kimaadili ya utumishi, jambo ambalo linaweza kuwaweka pabaya na
baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa kina, jambo hilo litafikishwa kwenye
Bodi ya Shule.

Hata hivyo, alisema wanafunzi wengi wavulana ni sugu katika uvutaji bangi na
dawa za kulevya na wengi wao wamediriki kukamatwa wakivuta bangi katika
maeneo ya mazingira ya shule na kupewa adhabu kali. Shule hiyo ina mikondo
11 yenye wanafunzi 617, wasichana ni 308 na wavulama 309 na walimu wa kudumu
19 kati yao wanaume ni 10 na wanawake ni tisa na walimu wanne wanafunzi wa
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

No comments:

Post a Comment