Leo Machi 28, 2009 nimehudhuria mchezo wa ligi ya Mpira wa kikapu nchini Marekani (USA) katika Uwanja wa Verizon Center, Washington DC uliochezwa kati ya wenyeji Wizards na Pistons waliotoka jimbo la Detroit. Katika Mechi hiyo Detroit waliwafunga Wizards magoli 82 kwa 80.
Katika uwanja huo unaoweza kukaa watu 60,000 mchezo huo ulichezwa kwa kipindi cha saa mbili ukiondoa muda wa mapumziko. Kabla ya kuanza mechi hiyo uliimbwa wimbo wa taifa la Marekani (The Star Spangled Banner) na wanakwaya katikati ya uwanja huo.
Baada ya hapo yakafuata maonyesho ya muziki wa wasichana waliocheza kwa mtindo wa duara katikati ya uwanja huo. Baada ya hapo ndio mechi ikaanza kati ya timu hizo mbili kwa vipindi vifupi vifupi huku wakpumzika.
Baada ya burudani hiyo, mtangazani wa mchezo huo aliufahamisha umma uliohudhuria kuwa kuna wapiganaji watatu waliotoka vitani jana yake na wakaonyeshwa wapiganaji hao kwenye televisheni ya uwanjani hapo na wakashangiliwa kisawasawa.
Wakipumzika kwa muda wa robo saa au nusu saa, uwanjani wanaingia wachezaji wa miziki ya marekani ya kileo ya vijana na hapo wanajimwaga vijana hao kutoa burudani tosha kwa watazamaji wakati wachezaji wanapumzika.
Kuna kipindi kimoja, mtangazaji akaweka maandishi ya Kiss.Cam. Kipindi hicho yeyote atakayeonyeshwa katika televisheni kubwa iliyowekwa katikati ya uwanja huo anambusu jirani yake aliye karibu. Mtangazani alihakikisha anawaonyesha watu wawili wawili mwanamke na mwanamume. Naamini bila ya kujali endapo hawa watazamaji wana uhusiano wa kimapenzi au la. Ili mradi watakaoonyeshwa kwenye televisheni wanabusiana. Hii nayo ilikuwa ni burudani peke yake japo kwa mimi na rafiki zangu kutoka Zambia Bi. Chiseche Mibenge na Dong Cheng kutoka China, tumeona ni kioja.
Kuna biashara uwanja mzima zinatangazwa katika televisheni mbalimbali uwanjani hapo. Kuna biashara zingine zimetundikwa mabango ya nguo. Haya ni pamoja na timu zilizowahi kushinda katika mashindano haya huko nyuma katika uwanja huo. Matangazo ambayo nimeona kwa mara ya kwanza yakionyeshwa ni yale ya maputo mawili; moja likiwa kama gari na lingine kama ndege. Matangazo haya yote yalikuwa yakiendeshwa na tekinolojia ya kisasa na yalikuwa yakipotea mara mchezo unapoanza.
Burudani nyingine iliyokuwa inaonyeshwa katika mchezo huo ni kudondoshwa fulana na kofia za bure kwa watazamaji. Kulikuwa na bastola maalum ya kufyatua fulana hizo zilizokuwa zinaruka juu na kuwadondokea watazamaji. Ukifanikiwa kudaka fulana hiyo ya iliyoandikwa "Wizards" ndio mali yako. fulana zingine zilikuwa zinarushwa kutoka darini huku zimefungwa maputo ili zielee kwanza kabla ya kuwafikia wadakaji watazamaji. Ili mradi mchezo huu unatiwa nakshi ili watazamaji wasichoke.
Katika sheria za mchezo huu, ikitokea faulo, refarii anaamuru na zinapigwa peneti mbili. Faulo moja moja sana zilikuwa zinapigwa peneti moja moja tu. Mchezaji anayefanikiwa kufunga katika faulo kama hiyo anapata pointi 2. Mchezaji anayefanikiwa kufunga akiwa nje wa uwanja wa kujidai, anahesabiwa pointi 3. Ndio maana mchezo huu hadi unapomalizika unaweza kuzalisha magoli 80/80 au zaidi. Magoli yanakuwa ni mengi sana tofauti na mchezo tuliouzoea wa soka.
Mpira unawekwa kati unapoanza tu. Lakini kunapofungwa magoli, mpira unaanzia pale penye goli lililofungwa hauwekwi kati.
No comments:
Post a Comment