Monday, March 30, 2009

ILI MRADI UWANJA UWE WAZI KWA WANAWAKE WASIO UWT!

meandikwa na Martha Mtangoo; Tarehe: 30th March 2009 @ 19:00

Image
Sofia Simba, Mwenyekiti wa UWT.



Miaka kadhaa iliyopita wanawake walikuwa watu wa mwisho katika kila kitu, ambacho walikuwa wakifanya licha ya kuwepo kwa usemi wa ‘Palipo na maendeleo, lazima mwanamke awepo’. Licha ya wanawake kuwa wa mwisho, pia wanawake wenyewe kwa wenyewe walikuwa hawapendani, jambo ambalo lilikuwa likisababisha kukwama katika mambo mbalimbali, ikiwemo kushindwa kupata nafasi za uongozi.

Hali hii imeendelea kwa muda mrefu. Kutokana na hali hiyo mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali, yalijaribu kuwasaidia wanawake katika kuhakikisha usawa unapatikana na wao wanapewa vipaumbele katika sehemu mbalimbali, ikiwemo nafasi ya kutoa maamuzi.

Sophia Simba ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), ambapo kutokana na wadhifa alionao wa kuwaongoza wanawake, anasema atahakikisha wanawake wa wanachama wa umoja huo, wanawezeshwa na UWT inatarajia kufufua miradi yake yote.

Sophia anasema kuwa UWT inatarajia kuanzisha miradi mikubwa kama zamani, achilia mbali jengo kubwa la ghorofa kumi, ambalo mkataba wake haukuwa mzuri. Anasema kuwa nia ni kuboresha UWT na kuifanya kuwa kimbilio la wanawake kama awali. Pia, anasema UWT itahakikisha akina mama wote ambao ni wanachama, wanaelekezwa mambo muhimu kuhusu Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS) na namna ya kujiunga na kupata mikopo.

“Lengo kubwa la UWT ni kumsaidia mwanamke kumuelekeza, akitaka mkopo anaenda wapi na anafuata taratibu gani ili aweze kupata mkopo, ambao unaweza kumsaidia, pia ni kuhakikisha mwanamke anayeonewa anasaidiwaje,” anasema. Mwenyekiti huyo wa Taifa wa UWT anasema kuwa kwa muda mrefu ofisi za umoja huo, zimekuwa zikiwakutanisha wanawake nyakati za mikutano.

Lakini, kutokana na hali ilivyo sasa mpango unafanywa ili kuhakikisha ofisi za UWT wilaya, zinakuwa mahali pa kukutana wanawake na kubadilishana mawazo. Aidha, anasema kuwa ili kuhakikisha hilo linafanikiwa elimu kwa viongozi wa chini, itatolewa ili kuhakikisha kuwa wanachama wa umoja huo, wanakuwa na uelewa wa juu sawa na viongozi wa juu, ambao tayari wanao uelewa wa kutosha.

Sophia anasema kuwa changamoto kubwa, anayokabiliana nayo katika umoja huo ni idadi ndogo ya wanachama iliyopo, ikilinganishwa na idadi ya wanawake wote hapa nchini. Anasema wanachama wa UWT waliopo sasa, hawafiki milioni 1.5, jambo ambalo anasema kuwa linasababishwa na kutokuwa na kadi na uelewa mdogo walionao.

Anasema ili kukabiliana na changamoto hiyo, viongozi wa UWT kwa ngazi zote, wanatakiwa kuhamasisha wanawake kuchukua kadi ili kuwa wanachama hai na kuongeza idadi kubwa ya wanachama. “Kadi zinauzwa na suala la kuwahamasisha wanawake kununua kadi na kuwa wanachama hai, na suala la dosari kuwepo katika mkusanyiko ni jambo la kawaida, nitajitahidi kuziondoa,” anasema Mwenyekiti huyo.

Changamoto nyingine anayoitaja ni kuhusu kuwapata vijana wanawake, ambao ni wanachama ambapo anasema katika kukabiliana nayo, UWT inatarajia kuanzisha klabu za vijana wanawake ili wawe wanakutana katika klabu hizo na kujadili masuala mbalimbali. Anasema UWT inatambua mchango wa vijana na walemavu na katika kuhakikisha hilo linatekelezwa, nafasi za vijana katika umoja huo, zimekuwa nyingi, ambapo pia pamoja na kuwepo kwa nafasi hizo, bado mabadiliko makubwa yanafanyika kuhakikisha vijana wanapewa nafasi zaidi.

Katika kuhakikisha umoja huo unafanya kazi 'kidot com' Sophia anasema kuwa UWT inatarajia kufungua Tovuti, ambayo itakuwa ikitumika katika kuwafahamisha makatibu wote wa mikoa wa umoja huo, juu ya utendaji wa kazi. Anasema kuwa utaratibu huo, utawasaidia katika utendaji wao wa kazi na hivyo kutumia teknolojia ya kisasa zaidi katika mawasiliano.

Kuhusu vitendea kazi, Sophia anasema kuwa UWT ina lengo la kuhakikisha kila ofisi inakuwa na kompyuta na mashine na kutolea nakala. “Katika wilaya nyingi wabunge wamekuwa wakisaidia vitendea kazi katika ofisi zao; na hali ya ofisi zetu kwa kweli si nzuri, zinatakiwa kuboreshwa ili ziweze kutunza kumbukumbu,” anasema Sophia.

Anasema kuwa kwa kuanzia, UWT imeamua kutoa baiskeli 137 katika wilaya zote ili kuwasaidia watendaji kuwafikia wanachama walioko mbali kwa njia hiyo. Anasema kuwa yapo magari machache, ambayo yako katika baadhi ya wilaya hayakidhi mahitaji, kuwa na magari ni gharama, kwa kuwa yanahitaji mafuta na matengenezo ya mara kwa mara.

Sophia anatoa mwito kwa makatibu na wenyeviti wa wilaya, kukaa pamoja na kuhamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi, kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao unafanyika mapema mwaka huu. “Hakuna nafasi ya mtu wasiogope eti huyu mwanaume, akina mama pia wajitokeze kuwapigia kura akina mama wenzao, kwa kuwa ni haki yao ya msingi kupiga kura,” anasisitiza.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake nchini (UWT), Husna Mwilima, anasema kuwa utaratibu unafanywa ili kuwashirikisha wanawake kutoka katika vyama vya siasa katika utendaji wa jumuiya hiyo. Husna anasema kuwa umoja wa wanawake nchini, haubagui wala kuoneana wivu na hivyo wanawake kutoka katika vyama vya upinzani, watashirikishwa katika shughuli za kiutendaji za UWT.

“Kwa mfano kama tunatoa mikopo hapa sisi UWT, au inatolewa mikopo katika saccos za UWT, katika utoaji wa mikopo hiyo hatutaangalia UCHADEMA au UCCM, tutawahudumia wote na kuwashirikisha wote bila kuangalia itikadi zao,” anasisitiza. Anasema UWT itafanya makongamano na warsha, kuhusu masuala mbalimbali ambayo yatawashirikisha wanawake kutoka vyama mbalimbali vya upinzani. Akizungumzia uteuzi wake kutoka ukuu wa wilaya hadi ukatibu mkuu wa UWT, Husna anasema kuwa amepokea kwa mikono miwili uteuzi huo, kwa kuwa anaamini kuwa kazi nzuri aliyoifanya akiwa wa wilaya, ndiyo iliyomfanya ateuliwe kushika wadhifa huo.

“Ukiwa mtendaji mzuri, hata kama utakuwa katika kata, ukiwekwa ufanye kazi ya kitaifa, utaweza tu, kwa hiyo mimi naamini naweza na nitafanya vizuri ninachoomba nipewe muda,” anasisitiza Katibu Mkuu huyo. Anasema kuwa hakuwa na sababu ya kukataa uteuzi huo, kwa kuwa aliyemteua katika ukuu wa wilaya, ndiye aliyemchagua kuwa katibu mkuu wa jumuiya hiyo.

No comments:

Post a Comment