Friday, March 13, 2009

KILIMO CHA MATUNDA YA TUFAA NI MAENDELEO

Mwandishi Wetu
Daily News; Wednesday,March 11, 2009 @20:01

Halmashauri ya Mji wa Njombe iko katika mkakati wa kuboresha kilimo cha matunda aina ya tufaa ili yaweze kushindana katika soko na yale yanayoagizwa kutoka Afrika Kusini. Ofisa Kilimo, Mifugo na Ushirika wa Njombe, Naftali Mundu alisema juzi kwamba matunda hayo yanayolimwa wilayani hapa, ni matamu na yenye ladha kuliko yanayotoka nje. “Tatizo ni namna linavyoonekana, halivutii kwa sababu halitunzwi vizuri,” alisema.

Alisema mkakati wao unalenga kuongeza uzalishaji kwa kutumia mbegu bora na kufuata masharti yote ya kilimo bora. Bwana Shamba wa Halmashauri hiyo, Victor Luvinga alisema wanahamasisha kila kaya iwe angalau na miti mitano ya tufaa itakayohudumiwa kwa masharti yanayozingatia kilimo bora ili izae matunda bora. “Huu ndio mkakati wetu, tukifanikiwa tunaamini zitakuwa na sura nzuri kama zile za Afrika Kusini kwa hiyo zitamudu ushindani katika soko,” alisema.

Alisema pamoja na tufaa, wilaya ya Njombe inalima matunda mengine yenye ubora wa hali ya juu kama mananasi, maparachichi na matopetope. Alisema katika kipindi cha mwaka 2007/2008 halmashauri ya mji wao iliweza kulima hekta 621 za matunda na mboga na tani 2,719 zilipatikana kutokana na kilimo hicho. Hata hivyo, alisema kiasi kikubwa cha matunda na mboga hupotelea shambani au kuharibika kutokana na ukosefu wa masoko ya uhakika, hali inayochangia kuwapotezea kipato wakulima na halmashauri yao.

Mmoja wa wakulima wa matunda katika mji huo wenye vijiji 44, Method Mlelwa alisema uanzishwaji wa viwanda vidogovidogo vya usindikaji wa matunda utaongeza tija katika kilimo hicho. Aidha Mlelwa aliwaonya wakulima kuacha uchu wa fedha kwa kuvuna matunda kabla ya muda wake kwa kuwa hali hiyo inachangia kupunguza ubora wake.

Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Iringa, Shaniel Nyoni alisema kwa kupitia Mpango wa Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (DADPs) halmashauri zote mkoani hapa zinaweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika kilimo. Hata hivyo alisema moja ya njia mwafaka ya kukabiliana na ukosefu wa masoko ya uhakika ya bidhaa zinazozalishwa mashambani alishauri uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya usindikaji wa mazao na matunda.

No comments:

Post a Comment