Saturday, March 21, 2009

MALIMBWENDE YA ATLANTA, GEORGIA, USA

Leo niwasimulie mambo ya kufurahisha niliyoyaona huko Atlanta Georgia Machi 19, 2009 nilipotembelea Hifadhi yao ya viumbe hai wa majini (Atlanta Aquarium) mjini Atlanta. Kiingilio peke yake ni bei tofauti kwa watoto, watu wazima na wazee. Mtu mzima kama mimi nililipa $27.00 kiingilio kwa siku.

Maana ya kiingilio hiki ukiingia saa nne asubuhi hadi saa 11.00 jioni wanapofunga hakuna atakayekuuliza ukiwa humo. Ili mradi tu uwe ndani ya hifadhi hiyo. Wazee kwa watu wa Marekani ni kuanzia miaka 65 na kuendelea. Kwa gharama hii peke yake na umati unaofurika hifadhini hapo kila kukicha, naamini kabisa kwamba hifadhi hii inajiendesha kwa ada hiyo. Bila shaka na waliokodi sehemu za migahawa ndani ya jengo hilo nao watakuwa wanachangia kodi sawia.

Wenyeji wetu walituambia kwamba hifadhi hii ya viumbe hai wa majini ndio iliyochukua ujazo mkubwa zaidi wa maji duniani. Ina maji mengi tu ya kuweza kuhifadhi nyangumi wa beluga (beluga whales) tuliwakuta watatu. Samaki hawa wamesema ni watoto ukilinganisha uhai na umbo lao. Kwamba wanaweza kukua hata kufikia mara mbili ya walivyo na pia huanza kuzaliana baada ya kutimiza miaka ishirini (20).

Samaki wengine tuliowaona ni papa upanga, papa taa, na wengine wengi tu. Kwa uzoefu wangu, samaki walionitoa ute ni aina Kolekole na Changu ambao ni wengi sana katika hifadhi hii. Bila shaka nina wapenzi wenzangu wanaochunwa na misosi ya samaki hawa. Ikabidi wanifurahishe kwa kuogelea kwao majini tu katika siku hiyo. Ilinifanya nikumbuke sana Bahari ya Hindi ambako ndiko tunakopata wa kwetu.

Sehemu nyingine iliyonifurahisha sana ni mfano wa Msitu wa Amazonia. Sehemu hii imejengwa na kuwekewa magogo na miti utafikiri uko katika msitu mnene sana na viumbe maji wake wamewekwa humo.

Tukiwa wageni wa Chuo Kikuu cha Emory, Atlanta, nilipata nyingine ya mwaka nilipokwenda kujipatia chakula katika bwalo lao. Katika bwalo hilo, chakula kinauzwa kwa bei moja (flat rate) tu ya $7.25. Yaani unalipia gharama hiyo kisha unaingia bwaloni na kuchagua utakacho kwa saizi ya tumbo lako. Kama hujashiba unaweza kurudia kwa hela yako hiyo hiyo. Hili lilinishangaza sana maana ninakosoma American University iliyopo Washington, DC chakula cha bwalo lao kinauzwa kwa uzito wake. Unachagua chakula kisha kitakapopimwa ndio utalipia gharama.

Hivyo nimeona watu wa Atlanta ni wakarimu sana kwa jambo hili. Maana ukichukua kidogo bei ni ileile na ukichukua kingi bei ni ile ile. Nilisikitika tu kwamba kwa bahati mbaya wenzetu Wamarekani wamebobea kwa tabia ya matumizi ya kukithiri (conspicuous consumption). Na jambo hilo kwa upande wa chakula wenzetu hawajali kabisa. Maana mtu atajaza sahani lakini atakula robo yake tu na kilichobaki atatia pipani.

Huku Marekani kuna utamaduni mzuri sana unaofaa kuigwa wa kutupa taka zako mwenyewe. Kila mtu alaye au achafuae mahala pa wazi popote (public place) anatakiwa akatupe mwenyewe taka zake. Jambo hili ni zuri sana japo kutupa huko ni pamoja na makombo.

Nilipofika Marekani Agosti, 2008 nilishangaa sana kuona wanafunzi pamoja na walimu wao na watu wengine hawachagui saa wala mahali pa kula. Wana tabia ya kula wima huku wakitembea, wakiendesha gari, wakisoma darasani au wakifundisha, wakisikiliza mihadhara, wakiangalia michezo, n.k. Nikawa naona tofauti tuliyonayo Watanzania. Kwetu mwanafunzi hata akila peremende (chewing gum) darasani ni kosa; yaani anachukuliwa kana kwamba haheshimu sehemu ile. Kumbe wenzetu wanajichana bila wasiwasi wowote. Kisha mapipa yapo kila mahali hivyo kutupa baada ya kula vitu kama makopo ya soda au juisi na makopo ya plastiki ya chakula ni rahisi.

Yawezekana sana tatizo walilo nalo la kujilia popote pale na wakati wowote ule, ndio linalochangia sana kwa wenzetu hawa kunenepeana kupita kiasi (obesity). Baadhi ya watoto wadogo wasiofikia miaka 20 wanapata taabu sana ya kutembea tokana na unene uliokithiri. Ni ajabu na kweli. Kisha huku Marekani, kumwambia mtu ukweli kuwa "wewe ni mnene sana, jitahidi kupunguza kula" au "kuwa mwangalifu wa kuchagua chakula kisichonenepesha" ni kosa kubwa sana. Hata ndugu wa kuzaliwa tumbo moja wanaweza wakawa maadui maisha kwa sentensi hiyo tu! Hivyo hawataki kuambiwa ukweli juu ya hali ya unene wao! Na hali hii inazidi kuwa mbaya kila kukicha maana wenzetu wanafanya utafiti na wanafahamu hata majimbo gani yenye watu wanene zaidi nchini humu.

No comments:

Post a Comment