Monday, March 23, 2009

UPEKEE WA WAMAREKANI (AMERICAN EXCEPTIONALISM)

Siku ya Jumatatu Machi 16, 2009, katika somo tulilopewa na mwalimu wetu mmoja chuoni Emory, Atlanta, Georgia tulikokuwa tunasoma somo la "Social Justice". Profesa Loretta J. Ross wa Sister Song (NGO) Atlanta, ametufahamisha jambo ambalo napenda leo niwafahamishe na wasomaji wengine. Mwalimu huyu ndio Mratibu wa Taifa wa asasi hii. Asasi hii inajishughulisha na Afya ya Uzazi ya Wanawake wenye Asili ya Kiafrika (Women of Color Reproductive Health Collective).

Amesema katika utamaduni wa Kimarekani, anajisikia vizuri sana anapokuta migahawa ya McDonald atembeapo katika nchi zingine. Kwamba amejitambulisha na kampuni hii maana yake ni kampuni ya watu wa kwao. Vile vile akasema hivi, anapokuta McDonald ana hakika ya kukuta vyoo visafi. Hiki ndicho nilichotaka kuwaambia kwa sifa kubwa kwa wenzetu hawa.

Vyoo vyao vyote vitumiwavyo na watu wengi au binafsi (public & private toilets), wao huwa wanaweka aina tatu tofauti ya makaratasi ya kutumia chooni. Pamoja na hayo, maji na sabuni pia havikosi katika vyoo vyao. Kwa watumiaji tuliozoea maji kama mimi, kinachokosekana ni chombo tu cha kuchotea maji hayo ili uyatumie. Sasa turudi kwenye makaratasi. Makaratasi yao ni kama ifuatavyo:

1. Aina ya karatasi ya kwanza ni ya kukalia kwenye choo chenyewe. Yaani kama mtumiaji anaona kinyaa kukaa juu ya choo ambacho hutumiwa na wengi, ili kuondoa hisia za maambukizi ya magonjwa, huchukua karatasi hii na kuitandika juu ya choo kabla hajatimiza haja aliyoendea.

2. Aina ya pili ni ile atakayoitumia baada ya kumaliza haja yake kwa kuchambia.

3. Aina ya tatu ya karatasi ni ile atakayotumia kama taulo. Yaani atakayojifutia maji baada ya kunawa na sabuni baada ya kumaliza haja yake aliyoendea chooni.

Sijapata uhakika endapo jambo hili limo ndani ya sheria; ingawa nashawishika kuamini hivyo kwa sababu lipo kila mahali. Isipokuwa hali hii hatukuikuta tulipotembelea Msitu asilia wa Shenandoah tu kule Virginia. Yawezekana hii ni kutokana na jinsi kulivyo porini sana. Kungine kote twendako, tunakuta hali hiyo. Hivyo nina sababu ya kuamini kwamba jambo hili ni sheria inayotekelezwa.

Si hivyo tu, kuhusu sheria za Marekani, hata ukiwa na mbwa ukitembea naye barabarani sheria inasema unatakiwa kuokota kinyesi chake atakapojisaidia. Hivyo wenzetu huku hutembea na mifuko ya plastiki (au mifuko hiyo hutundikwa sehemu maalum barabarani kwa ajili hiyo) wawapo na wanyama wao (ambao huku wanawaita ni sehemu ya familia; kama vile mtoto, ndugu, mama, n.k.).

Ni ajabu na kweli kwamba nchini Marekani, wanyama wanaheshimiwa na kutunzwa vizuri zaidi kwa bei ghali na watu kuliko binadamu wenzao. Mathalani niliwahi kuandika humuhumu huko nyuma jinsi Wamarekani miaka ya hivi karibuni wanavyowapeleka wazazi wao vikongwe na wagonjwa wakalelewe na Serikali au Nyumba Binafsi za Walezi. Huku wanaita Retirement Homes (nyumba ya kustaafia), au Living Assisted Residence (Nyumba ya Makazi ya kuhdumiwa), n.k.

No comments:

Post a Comment