Tuesday, March 31, 2009

BWANA VIJISENTI ANDREW CHENGE MAHAKAMANI


Imeandikwa na Halima Mlacha; Tarehe: 30th March 2009

Image
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, akiongozwa na Polisi wa Usalama Barabarani (kulia) na wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam, kuingia mahakamani hapo jana kusomewa mashitaka yanayomkabili ya kusababisha ajali na vifo vya watu wawili hivi karibuni. (Picha na Mroki Mroki).
Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Kinondoni, kujibu mashitaka matatu yanayomkabili kutokana na ajali iliyotokea hivi karibuni na kuua watu wawili. Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, jana alisomewa mashitaka hayo yakiwamo mawili ya kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha vifo vya watu wawili.

Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Emilius Mchauru, Mwendesha Mashitaka, Mrakibu wa Polisi David Mwafimbo, alidai kuwa katika mashitaka ya kwanza na ya pili, Chenge alisababisha kifo kutokana na uendeshaji gari kizembe. Alidai kuwa Machi 27 mwaka huu saa 10.30 alfajiri katika barabara ya Haile Selassie akiwa dereva wa gari namba T 513 ACE Toyota Hilux Pick-up mshitakiwa aliendesha gari kizembe na kushindwa kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara hiyo.

Aliendelea kudai kuwa katika mashitaka hayo pia aliendesha kinyume akibana kulia zaidi na matokeo yake kugonga pikipiki ya magurudumu matatu ‘bajaj’ namba T 736 AXC na kusababisha vifo vya abiria wa bajaj hiyo, Victoria George na Beatrice Constantine. Mafwimbo alidai kuwa katika mashitaka ya tatu, mtuhumiwa siku hiyo kwa uendeshaji wake alivunja kifungu namba 50 na 63 (12) (d) cha Sheria za Usalama Barabarani namba 30 ya mwaka 1973 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Alidai kuwa uvunjaji wa kifungu hicho ulibainika kwa kuigonga bajaj na kuharibu pia gari lake.

Chenge alikana mashitaka na Hakimu Mchauru kusema dhamana yake iko wazi kwa Sh milioni mbili ambapo alidhaminiwa na Ezekiel Masanja ambaye ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa Sh milioni moja huku naye akitoa Sh milioni moja zingine. Katika hali isiyo ya kawaida, mmoja wa wana ndugu hao alisikika akivishutumu vyombo vya habari akidai vinamwandama ndugu yao.

“Nawaambieni mtabakia hivyo hivyo masikini hata mkipiga picha Chenge hamtatajirika.” Katika majibizano na waandishi ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo anatarajiwa kutolewa mahakamani kwa mlango wa nyuma, hali iliyowafanya wapiga picha wajipange nyuma na baadhi mbele. Gazeti hili lilimshuhudia akitolewa kwa mlango wa nyuma na kuingia kwenye gari namba T 382 ACP Toyota Harriet na kuondoka mahakamani hapo kwa kasi. “Haoo waandishi wamekosa picha,” baadhi ya ndugu zake walizomea.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa tena mahakamani hapo Aprili 30 mwaka huu. Na Chenge anatetewa na Wakili Melkizedeck Lutema. Katika kesi hiyo ya aina yake, eneo la Mahakama hiyo liligeuka kichekesho kwa wananchi waliofurika kumshuhudia mbunge huyo akipandishwa kizimbani, kutokana na ndugu na baadhi ya askari kujaribu kumtoa kwa mlango wa nyuma ili waandishi wasiweze kumpiga picha.

No comments:

Post a Comment