Friday, March 6, 2009

MAJI KUONGEZEKA MOROGORO

Eline Shaidi, MorogoroDaily News; Friday,March 06, 2009 @20:07
Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Morogoro (MORUWASA) inatarajia kuongeza uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 24,000 hadi mita za ujazo 27,000 kwa siku kupitia fedha za mradi wa changamoto za Milenia ambao utaanza rasmi Oktoba mwaka huu. Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo John Mtaita, alisema MORUWASA imepata Sh bilioni sita kupitia changamoto za Milenia na kueleza kuwa fedha hizo zitatumika katika kuboresha miundombinu ya maji katika manispaa hiyo. Alisema fedha hizo ambazo zitatumika katika vyanzo viwili vya usambazaji maji katika manispaa hiyo, zimepitia serikalini na kwamba pia zina lengo la kuboresha huduma za maji. Mtaita alisema hivi sasa mradi huo upo kwenye hatua ya awali ya kuandaa michoro pamoja na usanifu wa mazingira, kabla ya kuanza kwa mradi huo utakaowawezesha wananchi kupata maji safi na salama. Akifafanua zaidi, alisema fedha hizo zitasaidia katika kituo cha maji cha Mambogo kwa ajili ya ununuzi wa tangi jipya lenye ujazo wa mita 450, machujio mapya ya kusafisha na kutibu maji yenye ukubwa wa mita za ujazo 6,000, kukarabati mabirika matano ya maji yenye ujazo wa mita 1,104, yaliyopo barabara ya Boma na Bahati pamoja na kutengeneza barabara yenye urefu wa zaidi ya mita 500. Pia fedha hizo zitatumika katika kutengeneza kituo cha maji cha Mafiga kwa kukarabati machujio ya maji ili kuweza kuongeza ujazo wa maji kutoka lita za ujazo 24,000 hadi 27,000, kufunga pampu mbili za maji zenye uwezo wa kutoa maji lita za ujazo 1,000 kwa saa.

No comments:

Post a Comment