Saturday, March 14, 2009

PROFESA JOSEPH MBELE NA UMUHIMU WA ELIMU UDSM

Imechangiwa na Profesa Joseph Mbele wa Chuo cha St. Olaf, Minnesota, USA

Mimi nilitamani kuwa mwalimu tangu nilipokuwa mtoto mdogo, kabla sijaenda shule. Sijui ni kwa nini, maana wazazi wangu walikuwa wakulima na mimi ni mtoto wa kwanza. Baadhi ya watu wanaingia kwenye profession kutokana na kufuata nyayo za baba, mama, kaka, na kadhalika. Kwa upande wangu, daima nimeamini kuwa ni Mungu ndiye aliyeniita na kuniingiza kwenye ualimu. Hakuna siku hata moja katika maisha yangu ambapo nilipata wasi wasi au kuterereka kwenye imani hiyo.

Matokeo yake, kwenye masuala ya kutafuta elimu na kufundisha, nimekuwa sawa na mlokole, "fundamentalist," au "extremist." Tangu nilipokuwa mtoto mdogo, nilikuwa nasoma kama sina akili nzuri, na miaka yote nilipokuwa shuleni ni hivyo, na nilipoanza kufundisha na hadi leo ni hivyo. Kila siku ninasali na kuomba mwongozo wa Mungu. Kila siku ninaogopa kuwa nisipofanya kweli, Mungu atanishughulikia. Sikudanganyi.

Kwa msingi huo, siwezi kujihusisha na rushwa, upendelevu, au uzembe. Daima nafanya mambo kwa kadiri ya uwezo wangu. Hata kama watu wataona ninachofanya ni cha kiwango cha chini, cha muhimu ni kuwa mimi najitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu. Hata kama wataona nakimbia kwa spidi ya kobe, all I want is to be sure that I am doing my best.

Hii kazi sikupewa na wanadamu, bali Mungu! Cha ajabu ni kuwa, hata kuja kwangu kufundisha hapa Marekani, sikuomba kuja, bali wao walinitafuta. Ni mkono wa Mungu! Siku tutakapokutana kwa JF na Heineken za baridi zikianza kukubali, nitakueleza kwa undani jinsi Mungu alivyofanya kazi hiyo. Wewe mwenyewe utakubali kuwa ni ajabu na kweli :-)

Kwa hivi, tunapoongelea utafiti, kwa upande wangu hakuna "choice." Ni wajibu mbele ya Mungu. Kwangu sio suala la kutafuta promotion au umaarufu. Ni wajibu mbele ya Mungu. Umaarufu ninao, lakini haya ni matokeo tu. Dini inatufundisha kuwa Mungu akikupa kipaji fulani, unawajibika kukitumia na kukiendeleza, kwa faida ya wanadamu. Kwa msingi huo, huwa naandika sana, iwe ni vitabu au makala kwenye magazeti au majarida. Yote ni wajibu mbele ya Mungu. Ninaamini kabisa kuwa nikizembea, nitaingia jehenam!

Ili kujibu ulizo lako kwa dhati imenibidi nianze kuelezea hii background.

Kuhusu walimu wa vyuo vikuu, msimamo wangu ni kuwa wale waliotangulia, yaani wenye uzoefu zaidi, wanao wajibu wa kuwafundisha, kuwaelekeza na kuwa mfano kwa wale ambao ni waajiriwa wapya au bado vijana kikazi. Pale UDSM, kwa mfano, wakati naajiriwa, tulikuwa na bahati ya kuwa na walimu wazoefu waliofuata maadili kisawa sawa na wakawa wanatuonyesha njia. Kwa upande wangu, walimu walionionyesha njia wakati nikiwa nimeajiriwa tu, ni kama Profesa Haroub Othman na marehamu Profesa Gilbert Gwassa walionifundisha kwenye MA ya Development Studies; akina marehemu Grant Kamenju (Mkenya, aliyenifundisha Literature), Gabriel Ruhumbika, na marehemu Mofolo Bulane (kutoka Lesotho, ambaye alinifundisha fokilori na nadharia ya fasihi), na wengine ambao walikuwa wanafundisha masomo mengine ingawa sikuwa mwanafunzi wao, kama vile akina Profesa Josephat Kanywanyi, Mgongo Fimbo, Dan Nabudere na Issa Shivji (wote kwenye kitivo cha Sheria), akina Arnold Temu, Isaria Kimambo, Fred Kaijage na Walter Rodney (Historia), akina marehemu Justinian Rweyemamu (Economics), na wengine akina Mahmoud Mamdani, Yashpal Tandon na Samuel Mushi (Siasa), akina Profesa Geoffrey Mmari, Severin Ndunguru, na Issa Omari, Abel Ishumi, na Marjoirie Mbilinyi (Education), na wengine wengi.

Enzi hizo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilikuwa kinavuma na kilichokuwa kinaheshimiwa hapo ni academic excellence, kwa upande wa wanafunzi na walimu. Walimu walikuwa wanajishughulisha na ufundishaji, utafiti na ufundishaji. Kutoa makala nzito au kuchapisha kitabu kizito ilikuwa ni jambo la kusifika. Leo hii, pamoja na kuwa wako walimu kadhaa bora pale UDSM, matapeli na wababaishaji nao wako sana. Kama methali isemavyo, katika msafara wa mamba na kenge nao wamo. Kuna kenge wengi katika msafara wa UDSM ya leo.

Kwa vile nilikuwa na bahati ya kufundishwa na walimu makini, kama nilivyoeleza, na kuanza kufundisha katika mazingira hayo, nikiwa na hao walimu wa kunionyesha mfano, na kisha nikaja kusomea permanent head damage huku Marekani, 1980-86, nilirudi UDSM nikiwa na moto sana na ari ya kufanya mambo ya uhakika.

Nilijitahidi kwa uwezo wote kuendeleza libeneke kama walivyonionyesha wale walimu wangu. Na kiti kimoja kilikuwa kuwaelekeza walimu wapya njia ya kufuata. Tulianzisha MA program pale idara ya Literature, na hii ilinipa fursa ya kuwamegea yote niliyojifunza mimi mwenyewe. Mmoja wa waliokuwa kwenye hilo darasa ni Hamza Njozi, ambaye alikuwa mwalimu mpya pale idara ya Literature. Huyu nilikuwa naongea naye sana na alikuwa msikilizaji mzuri, mwenye intellectual curiosity ya kiwango cha juu, na masuali tele. Leo hii Hamza Njozi is one of the best scholars in Tanzania, in terms of his research and publications. Wala mtu asikudanganye! Yeye ni Vice Chancellor wa Muslim University Morogoro. He is an internationally recognized scholar. Ukimsikia mtu anakuambia vingine, ujue ni mmbeya. Achana na umbeya.

Tatizo kubwa tulilo nalo Tanzania ya leo ni kuwa utamaduni tuliokulia sisi katika vyuo, umefifia. Tangu shule za msingi hadi sekondari na vyuo vikuu. Badala ya kufuata mkondo, ninajaribu kukumbushia maadili niliyopata, ingawa watu wengi Bongo hawaelewi. Ukipitia kablogu kangu, utaona kweli, kwa vigezo vya Bongo ya leo, akili yangu saa nyingine haijakaa sawa. Angalia mfano huu:

http://hapakwetu.blogspot.com/2009/01/raha-ya-kununua-vitabu.html

No comments:

Post a Comment