Friday, March 13, 2009

MZEE ABDALLAH AHMED RIYAMI AFARIKI DUNIA

Mwanahabari mkongwe Riyami afariki dunia na kuzikwa DAR.



MWANAHABARI mkongwe nchini, Abdullah Ahmed Riami amefariki dunia.

Riyami, ambaye sehemu kubwa ya uhai wake alitumikia sekta ya habari, alifariki dunia jana saa 7 mchana katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa.

Marehemu alizikwa jana saa 10 jioni katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam na mamia ya watu walihudhuria maziko hayo.

Kwa mujibu wa mwanawe, Gharib Riyami, mwanahabari huyo ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 87, alianza kuugua takriban miezi miwili iliyopita.

“Baba alianza kudhoofika takriban miezi miwili iliyopita, baada ya kuona hali hiyo tulimpeleka katika Hospitali ya Tumaini, Upanga na alikutwa na malaria, alitibiwa lakini hali iliendelea kuwa mbaya,” alieleza Gharib na kuongeza:

“Baada ya hali kuzidi kuwa mbaya alihamishiwa Aga Khan baada ya vipimo ikabainika kwamba alikuwa amepungukiwa damu kwa kiasi kikubwa pia figo zote mbili zilikuwa hazifanyi kazi.”

Akielezea wasifu wa baba yake, alisema baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia, ambayo alishiriki, aliajiriwa serikalini akiwa Mkurugenzi wa lililokuwa Shirika la Habari la Tanganyika (TIS).

Alisema alifanya kazi hiyo hadi mwaka 1974, alipostaafu na kuingia sekta binafsi.

Alisema licha ya umri mkubwa, baba yake aliendelea na uandishi wa habari wa kujitegemea wakati huohuo akiwa mweka hazina wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAJA).

Mashirika mengine aliyoyafanyia kazi akiwa mwandishi wa kujitegemea ni pamoja na BBC la Uingereza, AFP la Ufaransa na Reuters la Uingereza. Ameacha watoto 10, wajukuu 18 na vitukuu 10.

Pichani mzee riyami akisindikizwa katika safari yake ya mwisho.Picha hii ni kwa hisani ya issa michuzi
posted by Msimbe @ 9:37 AM

No comments:

Post a Comment