Imeandikwa na Hellen Mlacky, Moshi; Tarehe: 27th March 2009 @ 20:26
Kiwanda cha uzalishaji wa sukari cha TPC wilayani Moshi, kimelipa kodi yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 37 tangu kuanza uzalishaji wake mwaka 2000, ikiwa ni baada ya uwekezaji. Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho, Robert Baisac aliyasema hayo wakati wa kikao na waandishi wa habari kuhusu mafanikio iliyopata kiwanda hicho tangu kubinafsishwa kwake.
“Pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa sukari katika soko la ndani, lakini pia kiwanda kimeweza kuchangia uchumi wa nchi kwa kulipa kodi mbalimbali inayokadiriwa kuzidi kiasi cha shilingi bilioni 37,” alisema Baisac. Alisema kiwanda hicho kilipata uwekezaji kutoka nchini Mauritius inayomiliki asilimia 75 huku serikali ikibakiwa na asilimia 25 na kwamba imekuwa ikipata mafanikio kutokana na kuboreshwa kwa miundombinu ya kiwanda hicho.
Alisema kiwanda hicho kina eneo lenye ukubwa wa hekta 16,000, lakini eneo linalolimwa kwa sasa ni hekta 7,800 ambapo waliongeza eneo la kulimwa mwaka 2005/2006. Alisema eneo hilo la kilimo linalimwa kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji, aidha kwa kuchimba maji ardhini na maeneo mengine hutumia maji ya mito iliyopo pembezoni mwa mashamba ya kiwanda.
Sanjari na maendeleo ya kiwanda kwa ujumla, ofisa huyo alisema kiwanda kimekuwa kikitoa huduma kwa wafanyakazi wake pamoja na jamii inayozunguka ili kuimarisha ujirani mwema. Alisema kimetengeneza barabara za vijiji vinavyozunguka kiwanda hicho ambapo kwa wastani hutumia zaidi ya Sh milioni 30 kwa mwaka. Huduma nyingine ni pamoja na huduma za jamii katika masuala mbalimbali ambapo nayo kwa wastani hutumia Sh milioni 14 kwa mwaka mmoja.
No comments:
Post a Comment