Sunday, March 15, 2009

SAFARI YA ATLANTA NIMETOLEWA UKOKO WA MACHO NA METRO !

Leo Machi 15, 2009 nilisafiri kutoka Washington DC hadi uwanja wa ndege wa Artsfield-Jackson Atlanta, Georgia, USA, mwendo wa kama saa mbili hivi kwa ndege aina ya Fokker Friendship. Naamini ni mwendo mfupi zaidi kwa kutumia ndege kubwa za aina ya Boeng. Uwanja wa ndege huu uliopo hapo Atlanta unasemekana ndio uwanja wa ndege ulio bize zaidi kuliko mingine duniani. Sijui ule wa Schipol, Netherlands unachukua nafasi ya ngapi!

Hili na hili sina, kumbe siku za Jumapili, Metro Rail station za Washington DC huchelewa kufunguliwa. Nilipanda basi la D6 litokalo Sibley Memorial Hospital lipitalo McArther Boulevard, jirani na ninapoishi saa 12.16 kuelekea Dupont Circle (Red Line) ili nikaunganishe na Metro kwenda Metro Center. Metro Center nibadilishe niingie kwenye Blue/Orange Line kwenda Rosslyn Station, Virginia. Kutoka Rosslyn kuna 5A Bus linakwenda Dulles airport ili nikawahi ndege inayoondoka saa 4.46 asubuhi kuelekea Atlanta.

Nilipofika Dupont Circle saa 12.35 nikakuta milango ya Metro imefungwa. Lo, likanishuka shuu!!!. Nikasubiri hadi saa 12.45 ndio akaingia meneja wa kituo. Yeye akaniarifu kuwa siku ya Jumapili kituo kinafunguliwa saa moja na dakika ishirini ! (7.40am). Kwa kuwa nilikuwa nimewahi hata hivyo na kwa kuangalia muda wa kusafiri, nimeona bado ninao muda wa kutosha hata kama nitaanza safari ya metro saa moja na dakika ishirini. Muda wa kufungua kituo kufika na kituo kufunguliwa, kuingia chini nikakuta treni ya kwanza inaondoka baada ya dakika kumi hivyo nikasubiri.

Kweli muda ulipofika treni ya kuelekea Glenmont (Red Line) ilifika na tukaingia tuliokuwepo hadi Metro Center. Na kufika Metro Center tulisubiri dakika tatu tu ikafika Metro ya kunipeleka Rosslyn. Nikaingia kwenye treni hiyo hadi huko Rosslyn. Nilipotoka Rosslyn kuangalia hilo basi litakalofuata kuelekea Dulles Airport ni la saa 2.45. Hapo machale yakanicheza, nikaona sasa ndio kuna dalili ya kuachwa na treni kwa sababu makisio ya kufika uwanja wa ndege ni dakika 40 hivyo nikiondoka hiyo saa 2.45 asubuhi ni kwamba nitafika saa tatu na kitu. Hofu yangu ilikuwa kuchelewa muda wa kucheck-in. Pia nilikuwa sija-print Uthibitisho wa Safari; ambao kwa maelekezo niliyopata katika tovuti ya AirTran niliyosafiria, nilitakiwa nika-print pale pale airport. Hivyo nikaona majukumu bado ninayo mengi na muda ndio unayoyoma.

Nikaamua badala ya kusubiri basi ambalo ningelipia chini ya $5.00, nikachukua taxi (huku wanaita cab) iliyonigharimu $52.00. Kwa kweli niliwahi saaaana na nilifanya nilichotakiwa kufanya kwa kwenda mtandaoni na ku-print huwo Uthibitisho wa Safari (Confirmation information) na hiyo ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kufanya kitu kama hicho. Lakini kilikuwa rahisi kwa sababu ni kiasi cha kufuata maelekezo tu unayopewa na mashine yenyewe husika.

Baada ya kuchapa hiyo taarifa nikapeleka ku-check in ambako nilicheki na mzigo wangu wa sanduku (ulio chini ya kilo ishirini) nililolipia kabla $15.0. Baada ya hapo katika Dawati la Idara ya Homeland Security (wana kodi inaitwa September 11 Security Fee: $5.00 kwa kila msafiri) nayo walihitaji uthibitisho wangu wa pasipoti nikawaonyesha na wakajiridhisha kuwa ni mimi. Kufuatia hapo ikaanza foleni ya kwenye kuchekiwa usalama wa maungo. Katika sehemu hiyo unavua kuanzia viatu, majaketi, makoti, kofia, gloves na scarves. Vyote vinatiwa kwenye kapu kupitishwa kwenye camera ya kompyuta kuthibitisha kama hakuna kifaa cha hatari kilichomo. Baada ya kupita hapo ndio sasa nikaelekea kwenye sehemu ya kupanda basi la kusindikiza (shuttle) la kunipeleka Geti Na. 67 mimi na wasafiri wengine, nilikopandia ndege kuelekea Atlanta.

Nikafika Atlanta salama salimini muda uliopangwa saa 6.33 mchana. Kutoka kwenye ndege ni kiasi cha kufuata alama zinazoonyesha sehemu ya kuchukulia mizigo. Kwenye uwanja wa ndege wa Atlanta, sehemu hiyo inafikika kwa treni nyingine ya chini kwa chini. Hapo kunaitwa "baggage Claim" ndio kituo cha mwisho cha treni hiyo. Katika sehemu hiyo kuna njia mbili unazoweza kuchagua kulingana na kampuni ya ndege uliyosafiria. Mimi nilipofika sehemu nikakata kulia kwa sababu kampuni ya AirTran ilikuwa mkono wa kulia. Nikafika sehemu ya kuchukua mizigo.

Heri ni kuwa ndege haikuwa kubwa na hivyo wasafiri wake si wengi sana na hata mizigo yake si mingi pia. Lakini pia nilichukua tahadhari tangu nyumbani ya kufunga sanduku langu kitambaa cha kulitambulisha. Siku hizi bila ya kufanya hekima hii ni rahisi sana kupoteza masanduku kwa sababu mengi yanafanana.

Kutoka kuchukua sanduku langu nikaelekea kupanda Metro za Atlanta kuelekea Villa International tulikopangiwa kukaa kwa wiki moja tutakayokuwa huko. Hivyo nikapanda metro toka Airport hadi Lindberg Center Station. Hapa Lindberg kulikuwa na mabasi yaendayo Emory University ambayo ndio yanapitia kwenye hoteli hiyo. Nilipofika kituo husika baada ya kuuliza wenyeji nikateremka na manyunyu yakinyesha.

Nikamshukuru Mungu kuwa kwa mara yangu ya kwanza kufika katika mji wa Atlanta, Georgia, nimeweza kufika nilipopangiwa bila ya kubabaika sana, bila ya kuhitaji kupanda taxi. Jambo muhimu zaidi mtu usafiripo katika viwanja vya ndege vya nchi zilizoendelea kama hii ni kusoma zaidi alama elekezi zinazobandikwa sehemu mbalimbali na pia kuuliza watu endapo msafiri mgeni huelewi.

Wenyeji wetu walitupangia kutembelea Makao Makuu ya Kituo cha Habari cha CNN mara tulipowasili. Tukapelekwa huko na kuonyeshwa ilivyoanzishwa, imefikia wapi, maendeleo ya kuanzisha kituo cha Televisheni ya CNN ya lugha ya Kihispania inayotangazwa katika nchi nyingi za Amerika ya Kusini, redio ya CNN na kumbukumbu nyingi tu za Wanahabari wake. Hapa CNN habari zinazotangazwa ndani ya Marekani ni tofauti na habari zinazotangazwa katika Idhaa yao ya Kimataifa. Pia tulipaona palipofanyikia Olimpiki za mwaka 1996. Olimpiki hizi ndizo zilizouzindua mji huu kuweza kutambulika zaidi duniani na pia kuleta biashara za wawekezaji wenyewe wa Marekani huku.

Wenyeji wanasema mji huu kabla ya 1996 ulikuwa mdogo sana na uliokuwa ukibezwa kama "kwamba ni mji wa watu weusi" (yaani usiokuwa na hadhi ya kufikiriwa kuendelezwa kiuchumi). Kwa hivyo wenzetu huku wanayashukuru mashindano hayo ya 1996 kuwa yalileta neema na kuufanya mji uanze taratibu kujengeka; pamoja na kwamba mji huu ni kiungo kikubwa tu na cha siku nyingi cha njia za miundombinu ya barabara na reli zinazounganisha mashariki na magharibi, kaskazini na kusini zaidi ya nchi hii.

No comments:

Post a Comment