Friday, March 6, 2009

FRANK KANWATTA ANATAFUTWA MOROGORO

Eline Shaidi, Morogoro
Daily News; Friday,March 06, 2009 @20:14
Mmiliki wa Kampuni ya Ujenzi ya SENEFCO iliyopo mkoani hapa, Frank Kanwatta anatafutwa kwa tuhuma za kuchukua fedha na kushindwa kumalizia kazi aliyopewa kulingana na mkataba waliosainiana kati yake na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Akizungumza na 'HabariLeo' jana ofisini kwake, Mratibu wa Mradi wa Kilimo (PADEP) Julius Ngwita, alisema mmiliki huyo alisaini mkataba wa Sh milioni 4.4 kwa ajili ya ujenzi wa Soko la Tambuu lililopo kwenye Kata ya Lundi, Tarafa ya Matombo katika halmashauri hiyo.

Sambamba na fedha hizo za mradi, pia mkandarasi huyo ameondoka na fedha nyingine ambazo hazikuweza kujulikana, ambazo ni tathmini ya nguvu kazi ya wananchi pamoja na mchango wa halmashauri ambayo huchangia asilimia 20 kila mmoja katika miradi hiyo. Akifafanua zaidi, Mratibu huyo alisema kampuni hiyo ilipaswa kuanza ujenzi huo Januari 2007 na kumalizika Juni 2007, ujenzi ambao haukukamilika baada ya mkandarasi huyo kuchimba msingi na kukodisha chumba maalumu kwa ajili ya kuhifadhia vifaa vyake na kisha kutoweka kusikojulikana.

Baada ya Mkandarasi huyo kuondoka katika eneo hilo la mradi, halmashauri hiyo ilifanya jitihada za kumtafuta kwa simu na kumkosa, na hatimaye kwenda kwenye ofisi yake iliyopo katika Manispaa ya Morogoro na kushindwa kumpata kutokana na ofisi hiyo kufungwa kwa muda mrefu.

Halmashauri hiyo ililazimika kwenda kwenye kituo cha Polisi kwa ajili ya kutoa maelezo na kuchukua hati ya kumkamata yenye namba MOR / 5608 / 2008 ili waweze kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kumtafuta.Kwa mujibu wa Mratibu huyo, Julai 14 mwaka jana alikamatwa na kuwekwa rumande na kisha kutoka kwa dhamana na sasa haonekani. Gazeti hili halikumpata Kamanda wa Polisi mkoani hapa kuzungumzia hatua za polisi baada ya kuambiwa yupo kwenye mkutano.

No comments:

Post a Comment