Thursday, March 26, 2009

HABARI ZA MSITU WA MAFINJI KUHUJUMIWA NA WAWEKEZAJI

Taarifa hii niliiandika na kuifikisha kwa vyombo vya habari mara niliporejea kutoka Msituni MAFINJI, Tarafa ya Mtimbira, Wilayani Ulanga, Mkoani Morogoro Septemba, 2003. Haikuchapishwa na gazeti lolote, sifahamu kwa nini wakati maslahi ya taifa la Tanzania yakiangamia. WANAKIJIJI ITETE WALALAMIKIA KUVURUGWA KWA UTARATIBU WA MAPITIO YA WANAYAMAPORI Wanakijiji wa kijiji cha Itete kilichopo tarafa ya Mtimbira, Wilayani Ulanga, Mkoani Morogoro walelalamikia mamlaka ya Kampuni ya Shamba la Msitu wa Mitiki (Kilombero Valley Teak Company – KVTC) inayomiliki mashamba ya misitu ya mitiki kuwa wamekiuka makubaliano ya awali ya Mkataba wao wa Uwekezaji kwa kupasua msitu eneo la mapitio ya Wanyamapori la Mafinji.

Katika mkutano wa pamoja kati ya wakereketwa wa Mazingira wa Kijijini hapo wenye kikundi chao kiitwacho TUMI(Tusonge Mbele Itete) na wawekezaji hao wa Kiingereza, wanakijiji hao wamelalamika kuwa njia za wanyamapori zimezibwa na Msitu wa Mitiki.

Katika njia iliyoonekana kujikosha ya KVTC walipotupiwa lawama hizo za kuhujumu maliasili ya taifa la Tanzania na uchumi wake, walijibu kuwa Kampuni yao haina mipaka yoyote iliyowekewa na Serikali ya Kijiji hicho.

Taarifa hizi ziliwastua sana viongozi wa TUMI waliohudhuria mkutano huo uliofanyika tarehe 29.8.2003 kijijini Itete Minazini kwenye Ofisi ya TUMI.

Wakijibu maswali yaliyojitokeza katika mkutano huo, wenyeviti wa Kijiji cha Itete Njiwa na Itete Minazini, Acquilino Sautanga na Fikirini Mgwalu walieleza kuwa mipaka ya Kijiji cha Itete Njiwa na Itete Minazini haijapimwa rasmi na Serikali Kuu ya Tanzania ili kubainisha wazi mipaka wa maeneo ya Wafugaji, maeneo ya Wakulima wanavijiji na Wawindishaji wa Mofu, katika Mbuga ya Bonde la Mto Kilombero.Hata hivyo kilimo cha msitu wa Mitiki kilichaonza mwaka 1992 kinaendelea kwa kuendelea kupasuliwa msitu zaidi hadi kufikia eneo hilo linalolalamikiwa la mapitio ya wanayamapori.

Wanyamapori hupita eneo hilo kwenye kilele cha kiangazi kutoka mbuga ya wanyama ya SELOUS kuelekea Bonde la Mto Kilombero kufuata maji na vivyo hivyo hutoka Bonde la Mto wa Kilombero lifurikapo wakati wa masika na kuelekea SELOUS. Pamoja na kutolewa lalamiko hilo kwa uchungu sana na viongozi wa TUMI, viongozi wawakilishi wa KVTC wameonyesha kubeza hoja hiyo ya wananchi wa Itete kwa kuelezea kuwa wao tayari wameshapanda Mitiki katika eneo linalobishaniwa na kwamba walalamikaji wameshachelewa mno kwani wao KVTC wameshaingia hasara ya kung’oa msitu wa asili na kupanda mitiki. Wananchi waliisikitikia sana hali hii na wakereketwa wa mazingira walidai kuwa KVTC walijua fika kwamba eneo la msitu wa Mafinji ni mapitio ya msimu ya Wanyamapori, lakini waliamua kuupasua tu, ili kuuhujumu uchumi utokanao na maliasili za Tanzania. Wanamazingira hao walijiuliza bora ni nini kwa Watanzania, kuwekezewa Msitu wa Mitiki ili kupata fedha za kukodi ardhi husika na kuwamaliza wanyamapori wa Tanzania, au kubakiza msitu wa asili na kudumisha mali asili zetu bila athari kwa wanyamapori wetu? Wanavijiji hao wamehoji kulikoni Muwekezaji aendelee kuvunja sheria za nchi halafu aruhusiwe kuwekeza nchin? Mkereketwa mmoja wa mazingira aliyehudhuria mkutano huo Petro Msangameno amesema kuwa kwa uelewa wake mdogo, lazima KVTC wamevunja sheria kwa kupasua msitu katika mapitio ya wanyamapori kwa kuwa Serikali Kuu yenyewe inaheshimu na kulinda sana Maliasili zake kama Wanyamapori wanaopatikana kwa idadi kubwa sana Nchini Tanzania kutokana na juhudu kubwa na za makusudi za kuwalinda kwa kuwa wao hawana sauti na sauti zao ndio wananchi wenyewe.

TUMI na wakereketwa wa mazingira kijijini Itete wameiomba sana serikali kuu iingilie kati jambo hili ambalo sio tu kwamba ni hujuma kwa taifa, bali hata kwa wananchi mmoja mmoja waishio maeneo hayo kwani wanayamapori wahamapo sasa wanazagaa ovyo baada ya mapitio yao ya asili kubomolewa (msitu) na hatima yake wanyama hupitia mashamba ya wananchi wanakoharibu mazao ya chakula na yale ya biashara.

Wananchi hao wamesema kuwa hali hii inaongezeka zaidi baada ya KVTC kuziba mapitio ya wanyama kwa uzio wa Umeme katika Msitu wa Mitiki wa Nakafulu na Mafinji na hivyo wanyama wathubutuo kukatiza hukutana na uzio na hivyo kupata shoki(shock) ya umeme na kuwageuza kuwa wakali sana na hivyo kutishia maisha ya wanavijiji vilivyo jirani na msitu huo.

Wanavijiji na wakereketwa wa mazingira wamesema kwa uchungu mkubwa huku wakiwahurumia wanyamapori kuwa KVTC wanaelewa fika kuwa eneo wanalolima mitiki linapitwa na wanyamapori lukuki; na kuwa wanyamapori hao hawaelewi mipaka wala uzio; "iweje wawawekee uzio tena wa umeme wanyamapori wetu?" Jambo ambalo sasa linaongeza umasikini wa mkulima kwa kuwa hana uhakika tena wa kuvuna mazao yoyote shambani; iwe msimu mzuri au mbaya. Wanakijiji wamemueleza muandishi wa habari hizi (mimi) aliyekuwepo kijijini Itete kuwa zamani walikuwa wanalinda migomba wakati wa mapito ya Tembo kwa kuwa Tembo hawawezekani kwa kupenda kula ndizi za aina zote, lakini sasa hata zao la mpunga, mahindi na mengine hupondwapondwa na Tembo na wanyama wengine wakati wa mapito ukianza.Wamesema kwa kuwa wanyama hawana sauti, wao ndio sauti za wanyama hao na wanasikitishwa sana na kitendo cha KVTC cha kuhakikisha kinawamaliza wanyamapori wa Ulanga na wa nchi hii; kwani wanaamini kabisa kwamba kuzibiwa mapitio yao kutawaathiri sana wanyamapori hata kusababisha kutoweka kwao. Hii inatokana na ukweli kwamba wanyama pori hao wamepungua sana tangu kung'olewa msitu asilia na kuanza kustawisha msitu huo wa Mitiki.
Mkutano wa tarehe 29.8.2003 ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa TUMI Thabit Mbassa na Katibu wake Claud Likomawagi; pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji ya TUMI. Upande wa KVTC uliwakilishwa na Afisa Mipango ya Jamii na Mazingira wake Simon Magessa

No comments:

Post a Comment