Friday, March 13, 2009

SERIKALI ZA MITAA NA WADAU WAKE

John Nditi
Daily News; Thursday,March 12, 2009 @19:00

http://www.habarileo.co.tz/pics/uhuru.JPG

Msajili wa Vyama Vya Siasa nchini, John Tendwa ( aliyesimama) akiwa na Waziri wa Tamisemi ( kuhoto kwake) , Celina Kombani wakati akisisitiza jambo kwa viongozi wa vyama.

“Tangu tujipatie uhuru miaka 47 iliyopita, sisi sote tumekuwa wamoja na tumejenga utamaduni wa kujadiliana na kukubaliana mambo yetu, kwa kutumia nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu.” Hiyo ni kauli ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Celina Kombani.

Kombani alisema hayo wakati wa mkutano uliofanyika Februari 19, mwaka huu mjini Morogoro. Mkutano huo ulishirikisha viongozi wa vyama vya siasa, wakurugenzi wa halmashauri na watendaji wakuu wa asasi zisizo za kiserikali, kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa.

Uchaguzi huo unatarajia kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu na utashirikisha vyama vya siasa wenye usajili wa kudumu. Akifungua mkutano huo, Kombani anasema uchaguzi wa Serikali za mitaa wa Oktoba mwaka huu, utakuwa wa uhuru na uwazi, kwa ajili ya kudumisha amani na utulivu nchini.

Anasema Watanzania ni wamoja na jambo hilo limewafanya watu kufanya uamuzi wao, bila kugombana wala kusuguana na hiyo ni katika chaguzi mbalimbali zilizofanyika kupitia mfumo wa vyama vingi vya siasa. Kwa mantiki hiyo, anasema uamuzi wa kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, haukufanyika kimakosa.

Mabadiliko ya katiba yaliyofanyika Julai mwaka 1992, ndiyo yaliyoruhusu mfumo wa vyama vingi, ambapo sasa miaka 17 imetimia. Tangu mfumo huo wa vyama vingi vya siasa uliporuhusiwa, uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge, umefanyika mara tatu. Wa kwanza uliokuwa na vuguvugu kubwa la mageuzi nchini ulifanyika mwaka 1995.

Mbali na uchaguzi huo mkuu wa Rais na wabunge unaofanyika kila baada ya miaka mitano, uchaguzi mwingine ni wa Serikali za mitaa. Huo nao hushirikisha vyama vingi vya siasa mwaka huu. Hivyo, anasema kutokana na kuwa wa uhuru na uwazi, hatarajii kuona Watanzania wakigombana, kusuguana na kuhitilafiana kwa misingi ya kabila, dini, jinsia na itikadi zao za kisiasa.

Anasema kwa kuzingatia jambo hilo, Serikali imeyakubali baadhi ya maoni yaliyotolewa na wadau hao, isipokuwa imeyaondoa machache ambayo yameboreshwa kwa lengo la kuufanya uchaguzi wa serikali za mitaa uwe na amani, utulivu na wa kidemokrasia. “Maboresho yaliyotolewa na wadau, yamezingatiwa kwa kiasi kikubwa katika mabadiliko ya sera, sheria na teknolojia pamoja na nyakati za hivi sasa,” anasema Kombani.

Anasema kutokana na umuhimu wa kuwa na uongozi madhubuti katika ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa, Serikali imedhamiria kwa dhati kugawa madaraka makubwa ya kufanya uamuzi katika ngazi hizo. Anasema sera ya kugawa madaraka ya kufanya uamuzi yatasaidia kuhusisha matumizi ya rasilimali fedha na rasilimali ya watu.

Sera hiyo pia itahusisha ngazi za msingi za serikali za mitaa, ambavyo ni vitongoji, vijiji na mitaa. Lengo ni viongozi hao waweze kupatikana kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa. Ili kukamilisha azma ya kuboresha uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu, wadau wote hawana budi kuendelea kuwa watulivu na wavumilivu katika kujadiliana na kukabiliana kwa nguvu ya hoja na sio hoja ya nguvu.

Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, ambaye katika mkutano huo alikuwa ni Mwenyekiti , anasema robo tatu ya mapendekezo yaliyopitishwa na Serikali, yametokana na wadau hao, ambao pia wengi wao ni viongozi wa vyama vya Siasa. Katika mchakato huo, wadau hao walishirikishwa kikamilifu katika mikutano yote mitatu iliyopita.

Kwa upande wake, Serikali imefanya mabadiliko madogo kwa nia ya kuboresha uchaguzi huo wa serikali za mitaa. “Serikali haiwezi kukubaliana kwa kila jambo, linalowasilishwa na wadau wa vyama vya upinzani. Uamuzi utakaofikiwa yatavinufaisha vyama vyote vinavyoshiriki katika uchaguzi huo wa serikali za mitaa mwaka huu,” anasema Tendwa.

Msajili wa Vyama vya Siasa anasema suala la mgombea binafsi, bado lipo Mahakama ya Rufaa na hivyo Serikali itaendelea kuutumia utaratibu wake uliopo, kwa wagombea wote watokane na vyama vyao vya siasa. Anasema kwamba uchaguzi wa mwaka huu, utakuwa na uhuru zaidi, kuliko ule wa miaka ya nyuma, kwa kuwa Tanzania hivi sasa imepiga hatua kubwa zaidi katika masuala ya demokrasia ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema pamoja na kujitokeza kwa kasoro nyingi za kanuni na sheria, zitakazotumiwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu, bado chama hicho kitashiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huo.

Anasema vyama vya upinzani vitashiriki katika uchaguzi huo, ambao wananchi watakuwa na uhuru wa kuwachagua viongozi wao wa serikali za vitongoji, vijiji na mitaa licha ya kuwepo kasoro hizo. Anasema baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa katika mikutano mitatu tofauti ni juu ya suala la kuwepo kwa mgombea binafsi na kuendelea na utaratibu uliotumika katika uchaguzi wa mwaka 2004.

Anadai kuwa yote hayo, Serikali imekataa kuyaafiki. Profesa Lipumba anasema suala la mgombea binafsi, lilishatolewa uamuzi na Mahakama Kuu, ambayo iliruhusu kuwepo na mgombea binafsi, lakini Serikali ilikata rufaa, ambayo bado halijatolewa maamuzi. Mwenyekiti hyo wa CUF anasema juhudi zaidi zinahitajika kuboresha daftari la kuandikisha wapigakura katika uchaguzi wa mwaka huu wa Serikali za Mitaa.

Daftari hilo limepangwa kuchukua siku 21. Anasema muda huo ni mfupi, ukilinganisha na ukubwa wa uchaguzi huo. Anasema utaratibu wa kuanzisha daftari hilo ni mzuri, lakini haujazingatia uwakilishi wa vyama vingine vya siasa, kwa kuwa hakuna mawakala wa vyama vya siasa watakaoshiriki katika zoezi hilo.


Akizungumzia suala hilo, Katibu Mwenezi wa chama cha UDP, Isaack Cheyo, anasema ni wajibu wa serikali kuweka utaratibu unaokubalika na wadau wote, utakaondoa migongano na vurugu, zitakazoharibu uchaguzi wa mwaka huu wa serikali za mitaa.

No comments:

Post a Comment