Sunday, March 29, 2009

MAKALA NA. 12 YA AFYA BORA

Article 12 KUTOKA KWA DR. WILBERT BUNINI MANYILIZU wa Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro, Tanzania.

Caffeine

Caffeine ni kemikali inayopatikana katika baadhi ya vinywaji kama vile, kahawa, chai, kakao kwa viwango tofauti. Kiwango kikubwa kiko katika kahawa, chai ikifuatia na kidogo zaidi katika kakao ( Cocoa ). Pia caffeine huwekwa katika chokoleti. Caffeine huchukua kiasi cha robo saa (dakika 15) hivi kufika kwenye mzunguko wa damu na matokeo ya kazi yake hufifia baada ya masaa matatu na nusu.

Kiasi kidogo tu cha caffeine chaweza kumfanya mtumiaji achangamke na kubaki macho. Kiasi kikubwa kikitumiwa chaweza kusababisha maumivu ya kichwa, kutetemeka, kusikia hali ya woga, kukosa usingizi, kujisikia mwenye wasiwasi na katika mazingira ya hatari, kusikia mwenye kihelehele cha moyo na kusikia kelele zisizo za kawaida.

Utafiti wa hivi karibuni unaonesha kuwa matumizi makubwa ya kahawa yanaweza kuleta madhara katika afya ya mtumiaji. Hujenga tabia ya kuwa tegemezi kwa kutumia kinywaji chenye caffeine, yaani mtumiaji asipopata caffeine hujisikia kuzubaa, kichwa huuma, kuchoka, kutotulia, hofu mpaka atumie. Hivyo mtumiaji anapoamua kuacha yabidi aende akipunguza kiwango polepole sana ili asipate madhara ya kuacha, kwani huwa kama kileo.

Utafiti umeonesha mama mja mzito akitumia vinywaji vyenye caffeine nyingi (zaidi ya miligramu 800 au gramu 0.8 kwa siku) aweza kuhatarisha kuharibika kwa mimba. Pia imebainika kuwa caffeine zaidi ya gramu 0.3 kwa siku, pamoja na kuvuta sigara au pombe huongeza uwezekano wa mimba kuharibika.

Kwa akina mama wanyonyeshao caffeine inaweza kupita katika maziwa, hivyo mtoto akipata dozi yaweza kumletea matatizo ya usingizi, kutokuwa mtulivu na kutokunyonya vizuri. Kwa sababu pia kahawa hupoteza hamu ya chakula na kuharibu afya ya watoto.

Caffeine pia husababisha mtu kukojoa mara kwa mara (diuretic) na kumfanya mtumiaji kukaukiwa maji. Kama mtumiaji anatosheka na vinywaji vyenye caffeine basi ahakikishe anakunywa kiasi cha angalau glasi nane za maji kila siku, kama hawezi basi yuko katika hatari ya kukaukiwa maji.

Caffeine ni mbaya zaidi kwa mgonjwa wa shinikizo la damu au mwenye mapigo ya moyo yanayobadilikabadilika (Cardiac arrhythmias).

Kinywaji cha Cocacola kina caffeine ndani yake. Vinywaji vyote vilivyo na kemikali hii, huchochea mfumo wa simpathetiki mwilini na kuleta uzalishaji wa kemikali zingine kama adrenalini. Matokeo yake si ya kuunufaisha mwili, bali kuutia katika misukosuko na madhara zaidi kiafya yakilinganishwa na faida ambayo ni moja tu kujisikia mchangamfu na mwenye nguvu kwa muda mfupi.

Caffeine inapotumiwa huchochea kemikali zilizotajwa hapo juu na kuitibua sukari kuja kwenye damu na mtumiaji hujisikia nguvu na njaa kuondoka, lakini tukio hili halidumu muda mrefu, na linapokuwa limekwisha mwili huachwa mchovu, bila kunufaika na lishe nyingine isipokuwa sukari tu. Caffeine huushtua mwili (jitters), husababisha kukosa usingizi, huharibu mapigo ya moyo, hupandisha shinikizo la damu (BP), hupandisha kiwango cha kolestero kwenye damu. Madini na vitamini hupungua, pia husababisha uvimbe katika matiti, huchangia katika kuzaa watoto wenye ulemavu.
Madhara yanayoweza kujitokeza kwa mtumiaji
Kwa wanaotumia mara kwa mara hasa watoto, kinywaji kinaweza kuleta madhara.
Sababu utumiaji hupoteza hamu ya chakula chenye lishe na kwa kuwa kinywaji kina sukari nyingi huuridhisha mwili kana kwamba hauhitaji tena. Kawaida mwili unatakiwa upate vyakula vya wanga, protini, madini na vitamini ili uendelee kutenda kazi zake vizuri.

No comments:

Post a Comment