Thursday, March 26, 2009

CHUI HAFUGIKI !

Kutoka Gazeti la "Express", Gazeti dada la "Washington Post" la Washington DC, USA. la tarehe
24 Machi, 2009.

Gazeti hili limeripoti katika Ukurasa wake wa VIMBWANGA (Eye Openers) kwamba familia moja huko Weyhe, Ujerumani (Germany) imefahamishwa kwamba haiwezi kuishi na Chui waliokuwa wanamfuga kwa kipindi cha miezi 18 katika uwanja finyu wa mita za mraba 1,400. Hivyo walilazimika kumkabidhi chui huyo serikalini ili arudishwe msituni.

Watetea Haki za Wanyama nchini humo Tierschutzbund wameishawishi serikali yao ya mtaa kwamba kwa kweli Chui hastahili kufugwa. Uamuzi huo ulifikiwa baada ya kugundulika kwamba familia hii haikuwa na leseni ya kufuga Chui jike huyo.

Tierschutzbund wanastahili hongera sana kwa pande zote mbili kwa kuweza kuishawishi serikali yao kwamba Chui, kama mnyamapori, hastahili kufugwa nyumbani. Nasema hivi kwa sababu kwa upande wa Chui, kapata uhuru wake kwa kurudishwa msituni na kwa upande wa familia hii ambayo haikutajwa jina lake, uhai wao. Kwa hakika siku moja Chui huyo; pamoja na kulishwa na kupendwa kiasi gani na hawa wanadamu; siku moja wangekuwa kitoweo chake tu. Mnyama wangemzuiaje asili yake aliyojaaliwa na Mungu ya kuwinda?

Habari hii imenikumbusha mwaka 2003 tulipokwenda kuhesabu wanyama wakubwa, vipepeo na wanyama wadogo katika Bonde la Mto Kilombero tukiwa chini ya Uangalizi wa watafiti wa asasi ya Kimazingira ya Uingereza ya Frontier-Tanzania.

Julai, 2003 tulitinga katika Kambi ya Simba (Simba Camp) katika msitu wa Mafinji wilayani Ulanga, Tanzania kufanya kazi hii. Kambi hiyo ilikuwa kandoni mwa mto Mafinji. Wakati tunaishi hapo kwa miezi karibu mitatu, tulikuwa na jirani yetu Chui aliyekuwa anaishi kiasi kama mita 300 kutoka hapo kambini.

Katika kipindi chote tulichokuwa hapo hatukuwahi kumwona chui huyo; yaani hatukuwahi kukutana nae wala kumwona kwa mbali. Chui ana tabia ya kujificha sana mchana na pia kutumia muda mwingi sana akiwa juu ya msitu mnene uliokuwa na miti iliyozidi mita 40 kwa urefu hapo msituni. Sasa fikiria katika mazingira hayo sijui huko walikomweka Chui huyu wa kufugwa kama kulikuwa na mazingira muafaka kwa maisha yake. Huyu Chui wa Mafinji tulijua kuwa yupo kwa sababu wataalam wa sauti za wanyama tuliokuwa nao walimsikia saa za alfajiri akipita kambini kwetu kuelekea mawindoni kwake.

Si hivyo tu, ipo siku moja mlinzi wetu, Bwana Petro Msangameno alipokutana nae kwa mbali kidogo akiwa kwenye baiskeli akirudi kambini akitokea kijijini Luvili. Msangameno kwa kuhofia kuwa atanyatiwa kuwa kitoweo na chui huyo akabidi aongeze spidi katika mwendo wa baiskeli yake; kumbe wakati huo huo na Chui nae kwa aibu aliyonayo alikuwa anakimbia asigunduliwe na binadamu. Sehemu tuliyokuwa tukiishi hapo Simba Camp palikuwa na nyani na tumbili kibaaaao, ambao kwa kweli ndio walikuwa misosi vibonde kwa Chui huyo. Alikuwa na chakula cha kutosha kiasi kwamba hakuwahi kutubugudhi wanadamu sisi tuliokuwa jirani zake.

No comments:

Post a Comment