Monday, March 2, 2009

SAFARI YA JIJI LA NEW YORK

Siku ya Alhamisi tarehe 26/2/2009 tulisafiri katika kundi letu la Humphrey Fellows 2008/2009 kutoka Washington DC kuelekea New York kutembelea Umoja wa Mataifa pamoja na ofisi nyingine muhimu. Tulifikia hoteli ya Hampton Inn iliyopo 851 51st na 8th Avenue. Hoteli hii ipo karibu sana na sehemu tatu muhimu. Mojawapo ni Central Park, nyingine ni Broadway na Times Square.

Tulifika Umoja wa Mataifa Ijumaa tarehe 27/2009. Katika matembezi yetu ndani ya Jengo hilo la Umoja wa Mataifa lililopo First Avenue, tulionyeshwa zawadi mbalimbali zilitozotolewa na nchi mbalimbali duniani kwa Umoja huo. Tuliona Busati lililosukwa kwa ufundi mkubwa kutoka Iran, na Kitambaa cha sufu aina ya Kente toka Ghana. Pia tuliona zawadi ya Thailand kwa Umoja huo ambayo ni mfano wa mashua ya Mfalme iliyochongwa kwa ufundi mkubwa. Mwongozaji wetu alituambia kuwa Mashua yenyewe ya Mfalme huyo ni mara kumi ile tuliyoiyona na kwamba imechongwa kwa kutumia mti mmoja tu. Yaani hiyo Mashua halisia ya Mfalme. Pia kulikuwa na zawadi ya kutoka kwa Jamii ya Wahindu, na picha zilizochorwa zilizoashiria vita na amani kutoka Panama.

Katika safu ya Picha za Waliokuwa Makatibu wakuu wa Umoja wa Mataifa kabla ya kuanza kwa Katibu Mkuu wa Kwanza (jina sikulihifadhi), kuna kinyago cha sehemu ya kichwa ya Mfalme wa Namibia, nae pia sikuhifadhi jina lake.

Katika ziara yetu hiyo pia tulipewa elimu juu ya Ofisi ya Haki za Binadamu hapo Umoja wa Mataifa. Bw. Craig G. Mokhiber, Naibu Mkurugenzi wa Tume ya Haki za Binadamu, Ofisi ya New York, alituelimisha juu ya kazi za ofisi yake na kutukumbusha kuwa Umoja wa Mataifa umeundwa ili kudumisha Amani, Kuondoa dhuluma (social justice) na Kudumisha Haki za Binadamu. Katika hayo, amesema ofisi yake ndio imefanikiwa zaidi katika majukumu yake wakati jitihada za kutekeleza yaliyobaki yanakwazwa sana na Wenye Kura ya Turufu (Veto) na nchi zenye uwezo zaidi duniani.

Jiji la New York kwa ujumla wake lina watu wengi mno na majengo marefu mno kiasi kwamba kuiona anga ni nadra kwa sababu ya moshi mzito unaotanda juu kuzuia anga lakini jua litokapo hali ya hewa inakuwa nzuri kwa sababu tulifika wakati wa baridi.

Kama kawaida ya miji mingi sana Marekani, mji huu pia umejaa masanamu ya kila aina ya waheshimiwa wao wa zamani na watu maarufu wengine.

No comments:

Post a Comment