HEKOOOOOO na HONGERA SANA WILAC! Ikunda Erick Daily News; Sunday,March 01, 2009 @19:00 | |||||
Lakini pamoja na sheria na Katiba ya nchi kuyataja hayo na kusisitiza, bado kuna baadhi ya wanajamii ambao huzivunja na kukandamiza baadhi ya makundi katika jamii, kwa manufaa binafsi. Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na Watoto (WLAC), ni shirika binafsi la kujitolea lililoanzishwa na kusajiliwa rasmi mwaka 1994, kwa lengo la kusaidia makundi hayo katika jamii kupata msaada wa kisheria ili kuondoa unyanyasaji uliokithiri. Uanzishwaji wa kituo hicho ni mwendelezo wa kitengo cha msaada wa sheria katika Shirika la Uchumi la Wanawake (Suwata) lililoanzishwa mwaka 1989, likiwa na njozi ya kuona jamii inaheshimu haki za wanawake na watoto. Wiki iliyopita Dar es Salaam, WLAC walifanya maadhimisho ya miaka 20 ya kituo hicho ambacho kimekuwa Nyota ya msaada wa kisheria katika kufanikisha urejeshwaji wa haki za makundi hayo zilizoporwa. Mkurugenzi Mtendaji wa WLAC, Scholastica Jullu ambaye kitaaluma ni mwanasheria, anasema tangu kuanzishwa kwake, wanawake 39,670 wamefanikiwa kupewa msaada wa kisheria ambapo 39,470 kati ya hao wamepata haki zao mahakamani. Katika hao waliopata haki mahakamani ni pamoja na wale wajane waliofiwa na waume ambapo mara baada ya msiba, ndugu wa mume waliwanyang’ang’a mali na kuwaacha wakiwa na masikini. Scholastica anasema ingawa sio wote waliofika moja kwa moja katika ofisi za shirika hilo ambazo ziko kwenye maeneo tofauti nchini, lakini wapo walioweza kupewa msaada wa kisheria kwa njia ya simu. “Tunashukuru tumeweza kuona manufaa ya kituo hiki, tumewakomboa waliokata tamaa ya maisha kwa kutojua ni wapi pa kwenda kuomba msaada wa sheria, wengine waliogopa gharama za kuendesha kesi, lakini sisi tunasaidia bure”, anasema Scholastica. Anasema WLAC imekuwa msaada mkubwa ndani ya jamii kwa kuwa kwa hao waliokwishapata msaada wa kisheria, nao wamekuwa wakiwaambia na wengine wanaonyanyaswa juu ya kituo hicho, hivyo kuwawezesha nao kupata haki zao zilizopotea. Kwa kushirikiana na mashirika mengine ikiwemo serikali, wamefanikishwa kupitisha sheria zinazomlinda mwanamke, hadhi, haki na utu wake. Mwaka 1998 sheria ya makosa ya kujamiiana ilirekebisha sheria tano zinazohusu mwenendo na namna ya kushughulikia makosa ya kujamiiana au makosa yanayoweza kutendeka, na hivi sasa marekebisho hayo yameingizwa katika sheria husika. Pia ni kupitia WLAC, wameweza kufungua kesi ya mfano mahakamani ya kutaka ufafanuzi juu ya hali ya utata wa kikatiba uliopo katika sheria ya mirathi ya kimila. Katika sheria hiyo inawanyima haki wanawake wajane na watoto wa kike kurithi mali zilizoachwa na marehemu waume/baba zao, hivyo kufanya haki zao kuporwa na ndugu na kuacha familia ikiwa masikini bila msaada. Katika jamii, unyanyasaji dhidi ya watoto na wanawake umekuwa ukifanywa na ndugu hasa baada ya mzazi wa kiume kufariki ambapo tumaini na ndoto ya maendeleo huyeyuka kutokana na familia nyingi kuvurugwa na kudhulumiwa haki zao. Akitoa ushuhuda wa manyanyaso na kudhulumiwa, ambapo WLAC iliingilia kati na kumkomboa, Martha Justine (55) mama wa watoto wawili mkazi wa Segerea, Dar es Salaam anasema baada ya kufiwa na mumewe mwaka 1989, mashemeji walimdhulumu nyumba na mali. Martha anasema mumewe, alipofariki, alimuachia mtoto mdogo wa mwaka mmoja aitwaye Nyangeta ambaye sasa ni msichana mkubwa anayesubiri kuendelea na chuo Septemba mwaka huu, baada ya kushinda kesi yao. Akisimulia huku machozi ya furaha yakibubujika, baada ya kupewa msaada wa kisheria na kufanikisha kurudisha nyumba aliyonyang’anywa na hao mashemeji, Martha anasema hakutegemea kama haki yake na marehemu mumewe ingerudi. “Mume wangu alikuwa mfanyakazi Maliasili, alimiliki silaha na tulikuwa na nyumba ya biashara pale Mwenge kwenye vinyago (Dar es Salaam), lakini kifo chake kilinifanya niwe fukara wa kutupa, ila mahakama imerudisha haki yangu”, anasema Martha. Anasimulia, nyumba hiyo ya biashara shemeji zake waliichukua na kuifanya yao, hivyo hakuweza tena kupata fedha za pango ambazo awali walikuwa wakizitumia kulipia nyumba waliyopanga. Kutokana na hali hiyo, ilimlazimu kuondoka kwenye nyumba ya kupanga aliyoishi na mumewe na kwenda kupanga chumba kimoja na kuishi yeye na wanawe. Anasema hali ilikuwa ngumu na ikambidi aanze kufanya vibarua kwenye maeneo mbalimbali kama vya kukata majani ya ng’ombe na kuuza, kuuza maji barabarani na pia alikuwa mpishi kwenye shirika la Tanesco. Martha anasema akiwa Tanesco, Rais Jakaya Kikwete alitembelea shirika hilo na hapo ndipo aliposhindwa kuvumilia machungu yake na kuangua kilio cha kuomba rais amsaidie jambo ambalo lilikuwa mkombozi wake. Baada ya kulia kwa uchungu, anasema rais alimuita Ikulu na kusikilizwa na wahusika ambapo kupitia WLAC, walimuwezesha kufungua kesi ya mwaka 2005, ambapo Oktoba mwaka jana alishinda na kurudishiwa nyumba yake. “Sikuwa na kitu, si fedha wala nini ila WLAC walinipa mwanasheria ambaye kila mara nilikwenda naye mahakamani na yeye kuniongoza hatimaye nyumba nimerudishiwa, mwanangu sasa atasoma”, anasema Martha kwa uchungu. Anasema baada ya mahakama kutoa amri hiyo, hivi sasa nyumba hiyo ameipangisha na kodi yake inamsaidia kujikimu yeye na familia yake na fedha nyingine zitampeleka chuo mwanaye. “Kituo hiki kimefanya hayo yote leo nimekuwa tena mtu, si tegemezi tena kwani ninauelewa wa kujua wapi pa kupata haki, na pia jasho la marehemu mume wangu na mimi limerudi”, anasema Martha. Hivi sasa Martha anauza mkaa na kwamba ule muda wa kuhudhuria mahakamani kwa zaidi ya miaka mitatu, umekwisha na anautumia kufanya mambo mengine ya maendeleo ili kujikomboa yeye na familia yake. Huo ni baadhi tu ya mifano hai ambayo kupitia WLAC, wameweza kusaidia na kuidhihirishia jamii kwamba vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, na elimu duni ya sheria vinaweza kuifanya jamii kuwa masikini na tegemezi. Hiyo ni hali halisi kwa hapa mjini, ambapo vituo vya sheria na wasomi wengi wako karibu ukilinganisha na maeneo ya vijijini, lakini bado ukatili na unyanyasaji unaendelea kufanywa dhidi ya makundi hayo hata kwa maeneo ya miji. Mwenyekiti wa kituo hicho Nakazaeli Tenga, ambaye pia ni wakili, anaitaja mikoa 19 yenye ofisi za kituo hicho kuwa ni Kilimanjaro, Arusha, Kigoma, Lindi, Mtwara, Manyara, Mwanza, Ruvuma, Shinyanga, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga, Dodoma, Iringa, Pwani, Mbeya, Tabora, Singida na Kagera. Nakazaeli anasema pamoja na huduma waitoayo kuwa na mafanikio, bado zipo changamto ambazo zinaendelea kuwa kikwazo kwa huduma hiyo kufika maeneo mengi. Baadhi ya changamoto hizo ni uelewa mdogo wa jamii kuhusu sheria mbalimbali na haki za binadamu, ambapo wenye shida wengi huenda kituoni wakati kesi zimeshapitwa na muda. Pia uwepo wa sheria za kibaguzi dhidi ya wanawake imekuwa ni kikwazo kikubwa cha ufumbuzi au kuchukua muda mrefu kupata suluhu la tatizo. Hata hivyo anasema pamoja na vikwazo hivyo zikiwamo pia vya kituo kuendeshwa kwa ufadhili wa nje na kutoweza kujitegemea, lakini bado nia yao ya kuisaidia jamii hususan makundi hayo unaendelea na pia elimu inatolewa ili kukomesha vitendo vya unyanyasaji. Ni dhahiri kwamba jamii inapaswa kubadilika na kufahamu kwamba mwanamke katika jamii ni nguzo muhimu ya maendeleo, hivyo wana haki ya kumiliki mali na haki nyingine kama sheria na Katiba ya nchi inavyosema. Ni wajibu wa jamii kuzingatia sheria na kufahamu kwamba hakuna aliye juu ya sheria na kwamba awe mtoto, wanaume au mwanamke wote wana haki sawa mbele ya sheria. |
Monday, March 2, 2009
WOMEN LEGAL AID CENTRE (WLAC) MIAKA 20
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment