Tuesday, February 3, 2009

WIZI WA MIUNDOMBINU YA HUDUMA ZA UMMA TANZANIA

2009-02-02 17:21:00
Na Immaculate Njalangi, Jijini

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka, DAWASCO, imekata maji kwa zaidi ya wakazi 500 waishio Kunduchi Beach na Mtongani Jijini.

Aidha, katika operesheni hiyo, DAWASCO imegundua wizi wa maji uliofanywa na baadhi ya wakazi hao na kusababisha hasara ya shilingi 16,500,000 kwa mwaka.

Afisa Biashara wa DAWASCO Raymond Mndolwa, amesema kuwa huo ni muendelezo wa operesheni ya kukata maji katika Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake baada ya kugundua kuwa wakazi wengi wa Jijini, na pia baadhi ya makampuni, wamekuwa wakiiba huduma ya maji na kuliingizia shirika hasara kubwa.

``Baadhi ya wakazi wa Mtongani wamejiunganishia maji isivyo halali na hivyo kuiingizia DAWSCO hasara, kuna zaidi ya wakazi 500 wamejiunganishia maji kiholela. Kampuni itawachukulia hatua kali za kisheria,`` Mndolwa akasema.

Bw. Mndolwa amesema kuwa katika `operesheni` hiyo waligundua kuwa kampuni moja ya Johnson Group, imejiunganishia zaidi ya line mbili za maji kiholela huku wafanyakazi wa kampuni hiyo wakidai hawajapata huduma ya maji kwa muda mrefu.

``Angalieni ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya Watanzania wasiokuwa na nia njema na taifa hili,`` akasema Mndolwa, akiwaonyesha waandishi wa habari mabomba yaliyokuwa yakitiririsha maji katika jengo la kampuni hiyo ya Johnson.

Mndolwa amesema kuwa opresheni hiyo itaendelea kuwafichua na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaoihujumu DAWSCO, ikiwa ni siku chache tu tangu wadai kuwa hoteli ya Lamada imefanya hujuma zilizowaingizia hasara ya zaidi ya shilingi milioni 96.

· SOURCE: Alasiri

No comments:

Post a Comment