Sunday, February 8, 2009

MAADHIMISHO YA MIAKA 61 YA UHURU WA SRI LANKA

Februari 7, 2009.
Tarehe tajwa nilialikwa kuhudhuria maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa nchi kisiwa ya Sri Lanka. Nchi ambayo wakoloni wa Kiingereza waliipa jina la Ceylon, lakini baadaye wenye nchi yao waliamua kuipa heshima zaidi kwa kutumia jina la kienyeji la Sri Lanka. Nchi hii ni kisiwa kidogo kilichopo ncha iliyo kusini ya nchi ya India. Kisiwa hiki ni maarufu sana duniani kwa uzalishaji na uuzaji nje wa bidhaa yake kuu ya kilimo ya Chai.

Sri Lanka ilipata uhuru wake toka kwa Mwingereza tarehe 4/2/1948. Katika umri wake wa zaidi ya miaka 500 wa kuwa koloni, Sri Lanka iliwahi kutawaliwa na Wareno, Wadachi, ha hatimaye Waingereza. Kwa maelezo yao, mapambano yao ya kupigania uhuru kuikomboa nchi yao yalianzia mwaka 1915 hadi 1948 walipopata uhuru.

Maadhimisho haya nchini Marekani yalifanyika kwenye Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Jimbo la Columbia (University of District of Columbia [UDC] Auditorium). Ili ufike mahala hapo kwa sisi watembea kwa miguu, inabidi upande treni ya chini kwa chini (Red Line Metro Train) njia ya Reli Nyekundu toka nilipokuwa Tenleytown-AU hadi kituo cha pili tu cha Van Ness-UDC.

Nilifika muda muafaka kabisa wa saa 10.15 alasiri. Hafla yenyewe iliandaliwa kuanza saa 10.30 alasiri. Nikakuta msururu wa waliotutangulia wakihakikiwa majina na kupewa kadi za kuingilia ukumbini hapo. Nami nikajiunga mstarini na kuhakikiwa. Baada ya shughuli hiyo, Ubalozi wa Sri Lanka nchini Marekani walitayarisha na kugawa kwa wageni, vitu vitano ambavyo nimeona ni vizuri sana katika kuitambulisha na kuiuza nchi yao kibiashara.

1. Kulikuwa na kijitabu kinachotoa maelezo ya nchi hiyo kwa ujumla wamekiita " 61st Anniversary of Independece of Sri Lanka

2. Kijitabu kingine kilichokuwa kinatoa taarifa za namna ya uwekezaji nchini Sri Lanka kwa wenyeji wa Sri Lanka na kwa wageni pia, kilichopewa jina "Government of Sri Lanka Treasury Bills & Treasury Bonds".

3. Compact Disk (CD) iliyotolewa na Bodi ya Utalii ya Sri Lanka, bila shaka iliyosheheni vivutio vya Kitalii nchini Sri Lanka.

4. Bendera ndogo ya Sri Lanka

5. Kifurushi chenye paketi tano (5) za Chai ya Sri Lanka.

Hafla yenyewe ilihusisha vitafunwa (snacks) na Chai ya Sri Lanka iliyotolewa na Sri Lanka "Tea Board". Baada ya vitafunwa hivyo, ndipo zilipofuatiwa na sala na hotuba na hatimaye maonyesho ya ngoma za kitamaduni na mavazi rasmi ya Sri Lanka (hivi vilikwenda pamoja).

Sala na hotuba zilifanyika katika lugha tatu tofauti kwa sababu Sri Lanka ni nchi yenye wenyeji wa asili mbili kuu; ya Tamil na Sinhale. Hivyo, hotuba za lugha hizo mbili hatimaye zilitafsiriwa katika lugha ya Kiingereza. Sala za Kihindu, Tamil na Kiislam ziliendeshwa pia katika lugha hizo pamoja na Kiarabu kwa sababu kuna Waislam pia nchini Sri Lanka. Baada ya kuomba madua kwa dini zao, sala hizo pia zilitafsiriwa kwa Kiingereza pale ilipowezekana.

Katika Maadhimisho haya, mbali na maofisa wa Serikali wa Marekani, pia na Mabalozi wa nchi; nadhani zote zenye Balozi zao Washington DC; walialikwa maana alipoingia Mheshimiwa Balozi wa Nchi ya Sri Lanka, Mheshimiwa Jaliya Wickramasuriya (Mwanamume), ulifuata msururu mreeeefu wa mabalozi wenzake toka nchi mbalimbali aliowaalika katika hafla hii. Kwa bahati mbaya Mtanzania mie sikuweza kumtambua Balozi Sefue kwa sababu sijamfahamu kwa sura hadi sasa.

Nimeona niwagawie hiki kidogo nilichokishudia ili nasi katika nchi zetu Afrika tuweze kuiga katika kuziuza nchi zetu nchi za nje. Kumbe wenzetu wanatumia fursa kama hii ya Maadhimisho haya kuitangaza na kuiuza nchi yao kwa wageni na wenyeji wao wakiwa nje. Katika maelezo yao ya kiuchumi waliyotoa, wamesema mwaka 2008, Wa-sri Lanka waliopo nje ya nchi yao wamechangia Dola za Marekani Bilioni tatu ($3 billion) katika uchumi wa nchi hiyo. Heko Sri Lanka kwa kutimiza Miaka 61 ya Uhuru.

No comments:

Post a Comment