Sunday, February 15, 2009

MAYAI YA KUKU WA KUCHAKUA (FREE RANGE CHICKEN)

Wandugu,
Hapa Washington DC kuna Gulio kila siku ya Jumapili (wenyewe wanaita Sunday Market) mahala paitwapo Dupont Circle (Circle huku ni Round-about ya kwetu). Hivyo mahala hapo pana barabara kama nane hivi zinakutana na pia ni kituo maarufu cha Treni (za rangi nyekundu).

Lo, inabidi niwafahamishe hata hizi rangi za treni. Jiji hili lina ruti nne za treni cha chini kwa chini (metro). Kuna treni za hiyo Red Line kutoka Shady Grove hadi Glenmont. Blue Line inatoka Franconia-Springfield hadi Largo Town Center, Orange Line inatoka Vienna Firfax-GMU hadi New Carrolton na Green Line itokayo Branch Avenue hadi Greenbelt. Hizo ni njia za metro. Mabasi yapitayo juu ya barabara nayo yako mengi na ruti zake ziko nyingi tu.

Sasa leo nilipojitupa hapo Gulioni, nikaenda kwa muuza Mayai ya kuku wa kuchakua. Nikashangaa kukuta watu wamesimama mstari wakisubiri zamu yao wanunue mayai hayo. Nimeshangaa kwa sababu nimeona ni ustaarabu wa hali ya juu kutomzunguka/kutomzonga muuzaji ila kila ajaye awe anahudumiwa pekee na mwenye bidhaa. Hili ni jambo jema sana la kuigwa.

Ilipofika zamu yangu nikanunua mayai dazeni moja ya saizi ya kati (medium) kwa $3.50. Saizi kubwa ya mayai hayo anayauza kwa $4.50 na madogo zaidi anauza kwa $2.70. Muuzaji huyu kwa kumuangalia usoni tu ni mtu mzima anayeweza kuwa na wajukuu wengi tu. Kwa haraka haraka naweza kumkisia kama ana miaka inayoelekea au imeshavuka 70.

Muuzaji huyu alikuwa na Business Card zake hapo nami nikaomba na kuruhusiwa kuchukua moja. Mshangao wa pili. Mfugaji wa kuku wa mayai anazo business card za kuwagawia wateja ili wamsaidie kumtangaza! Bwana huyu anakaribisha wateja wake kwa bashasha ya hali ya juu na anatumia lugha ya kuvutia mteja hadi unajisikia uko nyumbani. Mimi nilipofika kwake sikujuwa pesa nilizoshika mkononi kama zingetosha hivyo nikamnyooshea mkono na sarafu nyingi tu za Marekani. Yeye akachagua hiyo $0.50 pamoja na noti tatu za dola mojamoja. Nikamwambia mimi sifahamu thamani ya sarafu zao na kwamba mayai yake ya kuku wa kuchakua yanafanana sana na mayai ya kwetu ya kuku hao hao wa kuchakua. Akaniuliza natoka nchi gani na kunikaribisha tena wiki ijayo. Nikamwambia natoka Tanzania, East Africa, akafurahi na kunikaribisha Marekani.

Mfanyabiashara huyu anaitwa Tom "Cranky" Hubric na biashara yake inaitwa "Waterview Foods". Simu yake kwenye kadi yake imeandikwa kuwa ni 410 873-3346. Ofisi yake ipo 9942 Kentucky Springs Rd., Suite 35, Meneral, Virginia 23117. Kwa kweli kwa jinsi alivyoisuuza nafsi yangu katika kunihudumia, nikaona na wenzangu mumkaribie kufanya naye biashara. Email yake ni tom@waterviewfoods.com na website yake ni www.waterviewfoods.com.

Baada ya kumalizana mfanyabiashara huyu nikaenda kwenye meza nyingine. Nikakuta kuna keki za maboga. Nikashangaa pia kwamba kumbe wenzetu wanaweza kutumia unga wa maboga kutengeneza keki. Nikanunua moja na hivi niandikavyo nimetoka kuila na nawahakikishia wasomaji kuwa ni nzuri sana, haina sukari nyingi, na katikati ya keki imewekwa krimu. Nilitamani kumuomba recipe aliyeniuzia keki hii lakini alikuwa amezungukwa na wanunuzi. Ila nina hakika keki hii itakuwa na lishe tele kwa sababu maboga ni katika mboga za majani zenye faida kubwa sana mwilini.

No comments:

Post a Comment