Sunday, February 8, 2009

TATIZO LA MIHADARATI

Tatizo hili si la kufumbia macho. Huku Marekani, tatizo hili baada ya kuwa sugu kwa muda wa miaka mingi, sasa wanalichukulia kama ni sehemu ya ugonjwa. Hawaiti tena "drug use" au "drug addiction". Wao kiserikali na kitakwimu wanaliita "substance abuse" na wanalichukulia kama ugonjwa sio matamanio. Hivyo watu wenye kutumia mihadarati hapa nchini Marekani wanatibiwa, wanapewa ushauri nasaha, wanatayarishiwa mafunzo ya kurejea kuwa raia mwema. Pia wanapewa misaada mingine mbalimbali, kwa sababu, nchi imeng'amua kuwa NGUVUKAZI yake kubwa inakosekana/imeharibiwa na janga hili la matumizi ya mihadarati.

2009-02-08 11:04:35
Na Mwandishi Wetu

Bado tatizo la uingizaji, usambazaji na matumizi ya madawa ya kulenya nchini linaonekana kuwekwa kando, huku vinara wakitamba na jamii ikiendelea kuangamia taratibu bila msaada wowote.

Pamoja na serikali kukiri mwaka 2006 kuwa tayari inayo orodha ya vinara wanaoingiza na kusambaza madawa hayo na kwamba inaifanyia uchunguzi, hadi sasa hakuna taarifa yoyote rasmi iliyotolewa kwa umma kuhusu matokeo ya uchunguzi huo.

Wadadisi wa mambo wameitaka serikali kuondoa ukimya kwa kueleza uchunguzi ulikofika na waliobainika kushiriki wafichukuliwe na kuchukuliwe hatua badala ya kuacha taifa likiangamia.

Kibaya zaidi, kundi linaloathirika zaidi na kuwepo kwa madawa hayo katika kona mbalimbali za nchi ni vijana, wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na hata vyuo vikuu.

Wiki hii, mjini Mororogo katika ukumbi wa Kanisa la Kilutheri la Kihonda, ulifanyika mkutano wa siri ulioandaliwa na baadhi ya viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini kwa kushirikiana na taasisi ya uchunguzi wa mazingira , MRECA, yenye makao yake mjini Mbeya.

Miongoni mwa washiriki kwenye mkutano huo ni vijana wapatao 266 kati ya 1887 waliotibiwa na kupewa ushauri nasaha na taasisi ya MRECA, hata kuachana kabisa na matumizi ya madawa hayo nchini.

Vijana hao wameilaumu serikali kwa kuwaachia milango wazi waingizaji wa dawa hizo kwa kipindi cha mwaka 2008 na hivyo kuzidisha kasi ya matumizi ya mihadarati kwa jamii hivi sasa.

Isitoshe, zipo taarifa za kuaminika kwamba baadhi ya waathirika wa dawa hizo wamo watoto wa mawaziri, wabunge na viongozi wengine serikalini na taasisi za umma na binafsi.

Lakini inashangaza viongozi hao wamekaa kimya kana kwamba hilo haliwahusu.

Akizungumza na Nipashe Jumapili, Mkurugenzi wa MRECA William Mwamalanga, alisema kuwa mkutano huo ulilenga kutathmini hali ya matumizi ya dawa za kulevya katika mikoa Mbeya, Morogoro, Dodoma, Dar es Salaam, Tanga na Zanzibar ambapo imegundulika kuwa kati ya Mei 2008 hadi sasa, kumeibuka kundi kubwa la wasambazaji wa mihadarati aina ya Cocaine, Heroine na bangi katika miji mbalimbali nchini.

Habari za ndani toka mkutanoni zinasema kuwa vinara wapatao 140 wanaoingiza na kusambaza madawa hayo nchini wameandikiwa barua za onyo kuacha mara moja hujuma hiyo ambayo inaliangamiza taifa na kupelekea chanzo cha maambukizi ya Ukimwi, mauaji ya maalbino, ongezeko la vibaka na hata migomo mashuleni na vyuo vikuu na maovu mengine.

Imeelezwa kuwa katika jumla ya idadi ya vinara wa uingizaji na usambazaji wa dawa hizo nchini ambayo orodha yao iko mikononi mwa Rais Jakaya Kikwete, tayari 40 wameshaachana kabisa na biashara hiyo.

Katika mkutano huo wa Morogoro, baadhi yao waliitwa na kuonywa, miongoni akiwemo padri wa Dar es Salaam, mchungaji wa kanisa la kilutheri Tanga, mchungaji kanisa la Pentekoste Mbeya, Sheikh toka Tanga, mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia wa Dar es Salaam na mwingine mfanyabiashara wa Dodoma. (majina yote yamehifadhiwa kwa sasa).

Mchungaji huyu wa Mbeya alikuwa kivutio kilichojaa masikitiko alipoeleza jinsi alivyokuwa akishiriki kufanikisha kupitishwa kwa dawa hizo kupitia mpaka wa Tunduma.

Pia alitaja namna silaha zilivyokuwa zinaingizwa toka Jamhuri ya Kongo na Burundi kupitia eneo hilo la mpaka.

Aidha baadhi ya vijana walioacha dawa hizo waliujulisha mkutano kuwa vijiwe vya kuuzia mihadarati vimeongezeka kutoka 450 mwaka 2005 hadi 1300 hivi sasa.

Vijana hao toka Dar es Salaam na Tanga ni Athuman Maleko, Mashaka Bwine, Said Amour, Hamisi Dazi.

Alfred Peter, Tino Halimoja na Sosipeter Hemed.

Wametaja Zanzibar kuwa ni njia ya wazi zaidi ya uingizaji wa mihadarati, ikifuatiwa na mipaka ya Tunduma, Kigoma na Kyela mkoani Mbeya. Wakati miji yote ya Tanzania Bara imetajwa kuwa na maduka ya kuuza Cocaine na Heroine.

Jiji la Mbeya na vitongoji vyake vya Uyole, Mwanjelwa na Mbalizi limetajwa kuwa na wauzaji 30 ambapo kwaka 2006 walikuwa watatu tu na Dodoma wapo 34, Arusha 146, Mwanza 115 na Unguja ni 76, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa kwenye mkutano huo.

Mchungaji mmoja wa kanisa la Evangelistic la mjini Mbeya amewataka wazazi na jamii kwa jumla kuwafichua watu wote wanaojihusisha na biashara hiyo haramu na serikali kwa upande wake iache kufanyia mzaha tatizo hilo linalotafuna kizazi hiki kimya kimya.

Katika orodha ya vinara wakubwa iliyokabidhiwa kwa Rais Kikwete ambayo gazeti hili iliwahi kuiona, imegawanywa katika makundi matatu, la kwanza likiwa ni la waingizaji dawa hizo nchini.

Kundi hili wanatajwa wafanyabiashara wanaomiliki kampuni kubwa kubwa, mmoja akiyaingiza kwa kutumia kondom, majokofu na vifaa vya hospitalini. Pia ana mahusiano na baadhi ya mawaziri serikalini.

Pia wengine wanatajwa kumiliki vituo vya mafuta ambapo mafuta huingia kwa wizi kupitia Tanga, wengine ni waingizaji wa nguo za mitumba.

Kundi la pili linataja majina ya wafadhili ambao majina yao hutumika kusafirishia dawa hizo wakiwemo wanawake wenye nyadhifa, baadhi ya wafanyabiashara wanaomiliki mahoteli, yapo majina ya wabunge, viongozi wa dini wenye makanisa, na maofisa wa polisi.

Kundi la tatu linahusisha wauzaji walioko mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Mwanza na Zanzibar. Ni orodha ndefu ya majina pamoja na kazi wazifanyazo.

Kinachosubiriwa ni matokeo ya uchunguzi alioahidi Rais kwamba unafanyika kubaini ukweli wa tuhuma zinazoelekezwa kwa wahusika ili tatizo hilo lidhibitiwe haraka kutokana na athari zake mbaya kwa taifa.

· SOURCE: Nipashe


No comments:

Post a Comment