Sunday, February 8, 2009

WAKILI ALISHWA SUMU JUU YA KESI YA EPA?

2009-02-08 11:03:00
Na Mwandishi Wetu

Mmoja wa watu muhimu anayeaminika kubeba siri nzito juu ya mmiliki halisi wa kampuni tata ya Kagoda, inayodaiwa kuchota Sh bilioni 40 kwenye akunti ya EPA, amelazwa katika Hospitali ya Mikocheni, jijini Dar es Salaam, tangu Januari 26 mwaka huu, baada ya kula kitu kinachodaiwa kutiwa sumu.

Huyu si mwingine bali ni Mwanasheria wa Jijini Dar es Salaam, Bered Malegesi (31), ambaye kampuni yake ilitoa mchango mkubwa katika kuzisajili baadhi ya kampuni zilizochota mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Malegesi alikuwa mshirika wa karibu wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Marehemu Daud Ballali.

Tukio hilo lisilo la kawaida, limekuja miezi tisa tu tangu Dk. Ballal, alipofariki dunia katika mazingira ya kutatanisha nchini Marekani, baada ya kudaiwa kula chakula chenye sumu.

``Aliletwa hapa akiwa hajitambui...lakini baada ya kumfanyia vipimo vya kimaabara tulibaini kuwa amekula kitu chenye sumu``, alisema daktari mmoja wa hospitali hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa sababu zinazojulikana.

Kumbukumbu za hospitali hiyo zinaonyesha kwamba, Maregesi, ametumia siku 11 akiwa amelazwa akipatiwa matibabu ya kuondolewa sumu inayodhaniwa alikula baada ya kutiwa kwenye chakula muda mfupi kabla hajaanza kuumwa.

Muuguzi aliyekuwa akimhudumia mwanasheria huyo hospitalini hapo ambaye naye alikataa jina lake lisiandikwe gazetini kwa maelezo kuwa si msemaji wa hospitali hiyo, alieleza kuwa Maregesi alipofikishwa hospitalini hapo alikuwa katika hali mbaya, akitapika mfululizo huku mwili ukiwa na joto kali.

``Hali yake ilitutisha sana...alikuwa hana uwezo wa kufanya chochote na timu nzima ya madaktari na wauguzi waliokuwa wakimhudumia walipata mshangao, tumeshawahi kupata matukio kama haya ya watu kuletwa wakiwa hawajitambui, lakini hili lilikuwa tofauti kabisa``.

``Tulikuwa tumemuweka katika uangalizi maalumu na wa karibu wakati wote, hata hivyo, hatuwezi kusema kama sumu hii imeingia mwilini baada ya kula chakula kilichotiwa sumu au hapana. Siku ya kwanza alipoletwa hali yake ilituchanganya sana, lakini sasa kadiri siku zinavyoenda anaanza kupata nafuu taratibu na hii ni faraja kwetu``, aliongeza kusema muuguzi huyo.

Hata hivyo, maadili ya kazi ya udaktari yanakataza madaktari na wauguzi kutoa taarifa kwa umma za mgonjwa aliyechini yao, hivyo kutokana na hali hiyo walikataa kutoa maelezo zaidi kuhusiana na mambo yaliyogundulika kwenye vipimo vya kimaabara.

``Hatuwezi kutoa taarifa zozote kuhusu aina ya sumu au matokeo yoyote tuliyoyabaini kwenye vipimo vya kimaabara bila ya ruhusu ya mgonjwa mwenyewe``, alisema muuguzi mmoja mwandamizi ambaye alikataa kuandikwa jina lake.

Inaelezwa kuwa daktari aliyechukua vipimo vya mgonjwa huyo ameshauri ufanyike uchunguzi zaidi wa kimaabara ili kuweza kubaini kiasi cha sumu kilichosambaa mwilini.

Hata hivyo, daktari huyo ameshaandika dawa anazotakiwa kutumia mgonjwa huyo, vikiwemo vidonge vya kuzuia kutapika, dawa za kupunguza maumivu na za kunyonya sumu toka mwilini.

Akizungumza na Nipashe Jumapili, baada ya kutoka hospitali juzi, Malegesi, alithibitisha kuwa alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Mikocheni baada ya kula kitu chenye sumu.

Alisema hawezi kuhukumu kama sumu hiyo atakuwa amewekewa kwa makusudi kwa lengo la kumdhuru au aliiinywa kwa bahati mbaya bila ya kujua.

Malegesi aliongeza kusema kuwa ameruhusiwa kutoka hospitali, lakini madaktari wamemshauri akapate matibabu zaidi nje ya nchi kutokana na sumu hiyo kumuathiri vibaya.

Hata hivyo, amesema kwa sasa hawezi kusafiri nje ya nchi kutokana na hati yake ya kusafiria kushikiliwa na Timu ya Rais iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza wizi uliotokea kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

· SOURCE: Nipashe

No comments:

Post a Comment