Mchungaji afungwa kwa kukataa kuapa (Angalia kama haki imetendeka au la chini ya habari hii)
na Kenneth Mwazembe, Mbozi, Tanzania Daima
Ijumaa Feb-06-2009
MCHUNGAJI wa Kanisa la EAGT lillilopo Mtaa wa Ichenjezya, mjini Vwawa, wilayani Mbozi, Mbeya, Simon Kitwike (48), amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela baada ya kukataa kuapa ili atoe ushahidi mahakamani.
Mchungaji huyo, alihukumiwa kifungo hicho jana na Hakimu Kajanja Nyasige wa Mahakama ya Wilaya ya Mbozi.
Kitwike, aliyevunjiwa nyumba yake mwishoni mwa mwaka jana na kuibiwa mali kadhaa , alifika mahakamani hapo, ili kutoa ushahidi wake, lakini alikataa kuapa kabla ya kutoa ushahidi wake akidai ni dhambi.
Hakimu Nyasige, alimwamuru asome kifungu katika Biblia kinachomtaka asiape mahakamani, ndipo mchungaji huyo alifungua Mathayo 5: 35 na kudai ndicho kinachompa msimamo huo.
Baada ya kusoma kifungu hicho, Hakimu Nyasige alimuuliza tena kama atakuwa tayari kuapa, ili atoe ushahidi, lakini mchungaji huyo aliendelea kubaki na msimamo wake wa kukataa kuapa.
Ndipo hakimu huyo alimsomea kifungu cha sheria na 198 (1) kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 kinachokataza mtu kudharau mahakama na kuwa kuendelea kukataa kuapa ni kuvunja sheria na hivyo ametenda kosa la jinai.
Hata hivyo, Hakimu Nyasige aliendelea kumvumilia mchungaji huyo, ili abadili msimamo wake kwa kumwamuru kusoma Biblia hiyo tena Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 13:1- 5, shahidi huyo alisoma kifungu hicho, lakini alipoulizwa kama amebadili msimamo wake alijibu kuwa hawezi kubadili msimamo wake.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Nyasige aalimtia hatiani kutokana na kumuamuru kwenda jela miezi sita na atatakiwa kufika mahakamani Machi 2, mwaka huu, ili atoe ushahidi wake kwa kesi ya msingi.
Akizungumza na Tanzania Daima baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mchungaji Mwandamizi wa kanisa hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwakasaka, alisema amesikitishwa na hukumu hiyo na kudai mchungaji wake alielewa vibaya vifungu vya Biblia vinavyozungumzia viapo.
Naye Mchungaji Erasto Makalla wa Kanisa la Pentekoste, alieleza kusikitishwa kwake na hatua hiyo ya mchungaji kupingana na mamlaka ya serikali na akasema kuna haja ya kuwafanyia semina wachungaji ili waelewe taratibu za serikali.
MAJIBU YA HOJA YA KUFUATA AU KUTOFUATA SHERIA KWA HAKIMU HAYA HAPA
MAJIBU YA HOJA YA KUFUATA AU KUTOFUATA SHERIA KWA HAKIMU HAYA HAPA
Kutoka kwa George Kakoti (gkakoti@gmail.com)
Kadri ninavyoelewa mimi, mtizamo wako ndio unaofuatwa na sheria za Tanzania. Vipo viapo vya aina mbalimbali--vya mahakamani wakati wa kutoa ushahidi, vya maandishi mbele ya wakili (k.m. Affidavit), vya kusimikwa wadhifa, mfano madaktari, viongozi wa serikali , vya kushughulikia nyaraka za siri n.k. Vyote hivi kwa jumla vinatawaliwa na sheria mama ya viapo--Oaths (Judicial Proceedings) and Statutory Declarations Act No 59 (1966).Hata hivyo wakati mwingine hutokea kupitishwa sheria mahsusi inayoweka utaratibu tofauti wa kiapo kwa shughuli fulani. Ikitokea hivyo, sheria ambayo ni "Specific" hutawala suala fulani na huiengua sheria ambayo ni "General." Mfani ni sheria inayotawala masuala ya viapo kwenye fomu za kuwania ubunge; mgombea wa Chadema alikosa nafasi yagombea ubunge kwa kuwa sheria ilitaka kiapo kifanyike kwa maandishi na kushuhudiwa na hakimu pekee, wala si mbele ya wakili.
Kuhusu viapo ndani ya mahakama wakati wa kutoa ushahidi, sijawahi kuona mtu akiapishwa kwa kushika katiba-hii itakuwa ni mbwembwe tu zisizo na nguvu kisheria. Ama tuseme sijaona sheria inayosema hivyo-huenda imenipita kushoto. Sheria kuu ya viapo inawaruhusu mashahidi wasiotaka kutoa maelezo kwa kiapo kwa sababu mbalimbali-mathalani kwa tafsiri yao dini (imani) yao inakataza viapo, ama hawafuati dini yoyote, kutoa maelezo kwa kutoa tamko ama ahadi ya kusema ukweli; basi. Hakuna ulazima wa kuapa kwa Msahafu ama Katiba.
Sheria yenyewe (kipande husika-kifungu cha 4 ) ina proviso inayosema hivi:
...Provided that where any persons who is required to make an oath professes any faith other than the Christian faith or objects to being sworn; stating as the ground of his objection, either that he has no religious belief or that the making of such oath is contrary to his religious belief, such person shall be permitted to make his solemn affirmation instead of making an oath and such affirmation shall be of the same effect as if he had made an oath.
Kwa maana hiyo hakimu huyo alikosea kwa kuleta Udini kwenye shughuli pasipohitajika.
No comments:
Post a Comment