UHUSIANO WA MAFUTA YA KULA NA AFYA YA MTUMIAJI
Matumizi ya mafuta ya kula, vitambi na magonjwa
Binadamu huhitaji mafuta katika chakula. Mafuta huongeza hisia ya shibe, hamu, ladha na ubora wa chakula kinywani. Mafuta pia ni muhimu mwilini kwa kutoa viini lishe muhimu kwa kukua na utendaji kazi wa neva za fahamu. Mafuta hufaa sana kwa unyonywaji wa vitamini kama A, D, E na vitamini K. Lakini si mafuta aina zote yenye manufaa haya mazuri ya kiafya. Mafuta hutoa akiba ya nguvu mwilini wakati wa njaa ya siku nyingi (starvation) inapokuwa imetokea. Kwani huvunjwavunjwa na kutumika kuzalisha nguvu na joto. Ni vema ieleweke kuwa mafuta haya huwa hayatumiki kwa njaa za kawaida za kila siku.
Aina za mafuta
Mafuta yote hayafanani. Kuna aina kuu mbili za mafuta nazo ni; mafuta hatari na mafuta yenye hatari kidogo. Hii ina maana kuwa baadhi ya mafuta ni mazuri kidogo kwa afya, mengine hupandisha kolestero ambayo ni hatari kwenye damu (kama tulivyoona kwenye article 2) na husababisha madhara kwenye mishipa ya damu hasa kwenye moyo. Kutia mafuta kiasi kikubwa au kula vyakula vyenye mafuta ya aina yoyote kuzidi mahitaji ya mwili hakuna mwisho mzuri. Kwani aina zote huleta kuongezeka kwa uzito na unene japo kwa viwango tofauti. Ujumbe huu utamsaidia msomaji kuamua chakula kipi atumie ili kujiepusha madhara katika afya yake. Ndani ya mafuta haya kuna kolestero.
Mafuta mazuri kiasi kwa afya na salama kwa moyo
Mafuta ambayo huwa yako katika hali ya kimiminika katika joto la kawaida (room temperature) huitwa Unsaturated fats. Lakini mafuta haya yaweza kutiwa haidrojeni kidogo katika kuyasindika ili yakae muda mrefu, kwa kuyatia haidrojeni basi huganda na kuyafanya yaingie kwenye kundi la mafuta ya hatari.
Umbo la kikemia la mafuta haya hupatikana zaidi kwenye vyakula vinavyotokana na mimea, pia hupatikana kwenye samaki wanaokula mimea midogo midogo mtoni, ziwani au baharini. Aina nyingine katika kundi hili la mafuta ni ya Omega 3 (omega 3 fatty acids). Utafiti unaonesha kuwa mafuta haya yana faida, kwa mfano, hupunguza vifo vya ghafla vinavyotokana na moyo, kwa sababu husaidia kuondoa ugumu au ukakamavu wa mishipa ya damu na pia huzuia damu kuganda isivyohitajika. Mafuta mengine katika kundi hili ni ya (polyunsaturated fats) na jingine lile la (monounsaturated fats). Aina hizi hapa juu hupunguza aina hatari (mbaya) ya kolestero (LDL).
Vyanzo vya mafuta ya aina hii
Omega 3 fatty acids
· Sato, dagaa
· Jamii ya karanga
Poly unsaturated fats huitwa (omega 6 fatty acids)
· Mafuta ya mimea; kama vile nafaka, ufuta, alizeti, pamba, mawese
· Maboga (pumpkin) na soya
Monounsaturated fats
· Mimea kama zeituni “olive oil”, aina za karanga, korosho, embe mafuta “avocado”.
Mafuta hatari (mabaya) kwa afya
Mafuta aina hii hupatikana zaidi katika vyakula vyenye asili ya wanyama, kwenye nyama za mafuta, mazao ya maziwa na mifugo. Na mengi ya haya huwa yameganda katika joto la kawaida.
“Trans fatty acids (trans fats)”
Yapo katika vyakula vilivyotiwa haidrojeni ambayo ni ya mimea. Kawaida kitendo cha kutiwa haidrojeni hufanyika viwandani ili kuyafanya yadumu muda mrefu. Hivyo kitendo cha mafuta mazuri ya mimea kuyapitisha katika mitambo huyafanya yawe na tabia tofauti huleta hatari kwa afya ya mtumiaji. Vyakula vya kukaangwa na vinginevyo vinavyopita viwandani, kama “margarine” za kunata (siyo laini), vyote hutoa aina hii ya mafuta.
Utafiti unaonesha kuwa aina zote za saturated na trans fats hupandisha LDL ambayo ni kolestero hatari kwa afya. Kemikali hii huenda na kunata kwenye ukingo wa ndani wa mishipa mikubwa ya damu. Mishipa hii hupungua kipenyo, na pia hukakamaa, hivyo kusababisha damu kupita kwa shida na hii hupelekea damu kuhitaji shinikizo la juu ili iweze kupita (shinikizo la damu). Kibaya kingine, mafuta ya aina ya “trans fat” na yale ya wanyama hupunguza zaidi kolestero salama (HDL) ambayo husaidia mwili.
Vyanzo vya mafuta haya hatari yanayotakiwa kuepukwa
“Saturated fats”
Huongeza kiwango cha kolestero mbaya LDL
· Mapande ya nyama za mafuta
· Nguruwe na kondoo
· Ngozi ya kuku, mabawa ya kuku
· Siagi (cheese/butter), (mafuta ya maziwa-cream) maziwa yenye mafuta (cream)
“Trans fats”
Huchangia kuongeza kiwango cha kolestero mbaya aina ya LDL
· Siagi ya kunata
· Vyakula vilivyokaangwa, kama “chips” mayai nakadhalika
· Zaidi sana aina hii hupatikana katika vyakula vilivyosindikwa viwandani, vilivyotiwa haidrojeni
· Keki nakadhalika
Kolestero katika vyakula vingine
Kolestero siyo mafuta. Isipokuwa ni kemikali inayonata inayopatikana katika vyakula vyenye asili ya wanyama; kama nyama, aina za kuku, vyakula vya baharini, kiini cha yai, maziwa ya krimu.
Mwanadamu hahitaji kutumia kolestero sababu miili inaweza kutengeneza kolestero zake kwa mahitaji ya ngozi za chembe chembe (cell membrane) na pia kwa ajili ya homoni. Kupata kolestero isiyohitajika ni kuleta magonjwa ya mishipa ya damu na magonjwa ya moyo, kiharusi (stroke), kisukari, kansa na mengineyo.
Vyakula vifuatavyo vina kolestero nyingi
· Kiini cha yai, inashauriwa kiwango kisizidi mayai mawili kwa wiki kwa mtu mzima
· Nyama za mafuta, zikiwemo nyama za viungo kama moyo, nundu, ubongo, figo na maini
· Vyakula vya baharini
· Nyama za kuku hasa wa kisasa, na zaidi ile ngozi ya kuku.
Baadhi ya wasomaji wanaamini kuwa watu wanene ndio wenye hatari ya kuwa na kolestero na magonjwa ya moyo na yanayofanana na hayo na siyo wembamba. Wanene na wembamba wanaweza kuwa na kolestero kama matokeo ya vigezo kadhaa na siyo uzito pekee. Hii ni pamoja na tabia za kula (kula kula kila wakati bila utaratibu), aina za vyakula, kiwango cha kolestero katika vyakula, kuzaliwa kwenye ukoo wa asili ya kuwa na milango ya kupokea kemikali hii na kupata magonjwa haya (Magonjwa ya urithi)
Ushauri
Msomaji anashauriwa baada ya kuelewa tatizo, aamue kujaribu kupunguza matumizi ya mafuta hatari kwa afya binafsi. Yapasa mara nyingi kuchagua vyakula vyenye mafuta kidogo na zaidi vichaguliwe vyakula vile vyenye asili ya mimea.
Kuwa mwangalifu na vitu vinavyopitia mdomo kwani magonjwa mengi hupitia hapo. Mazoezi, na kunywa maji mengi, kula vyakula vya asili, matunda na mbogamboga husaidia kudhibiti athari za mafuta. Tunahitaji kiasi fulani cha mafuta ya mimea kwa utendaji kazi mbalimbali mwilini kwa afya bora.
Chakula kisicho na mafuta au chenye mafuta kidogo sana husababisha mapungufu katika mwili kama kuwa na ngozi isiyo nyororo yenye magamba, kupukutika nywele, kuchelewa kupona kwa vidonda, kujisikia mchovu, kutumika bila mpangilio mzuri kwa wanawake, na matatizo ya uzazi (fertility).
No comments:
Post a Comment