Sunday, February 8, 2009

SOMO LA AFYA BORA NA. 4

Kutoka Kwa Dr. Wilbert Bunini Manyilizu, wa Chuo Kikuu Mzumbe, Tanzania;Jumatatu, Februari, 2, 2009.

Article 4

MAJI YALIVYO MUHIMU KIAFYA KAMA TIBA

Maji ni kimiminika chenye matumizi mengi na muhimu katika maisha ya kawaida ya kila kiumbe hai. Maji ndiyo sehemu kubwa ya mwili wa binadamu. Bila maji maisha hayawezekani kuendelea. Kwa binadamu maji yaweza kutumika kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za usafi wa mwili kuondoa uchafu kwenye ngozi na kuifanya ngozi ing’ae na kufanya vitundu vya kutolea uchafu vitoe jasho na uchafu mwingine na kujenga afya bora ya ngozi. Katika article hii maji yatazingatiwa kwa upande wa kutumika kama hitaji kuu la utendaji wa shughuli zote katika mwili wa binadamu. Maji haya yanapatikana mwilini kupitia chakula tunachokula au kwa njia ya kunywa moja kwa moja. Maji yana uwezo kufanya mambo mengi ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kushangaa na kudhani ni miujiza. Haya yatajadiliwa katika aya zifuatazo kwa kutumia takwimu za kisayansi. Maji yana uwezo wa uponyaji. Watu wengi wameugua miaka mingi wakijaribu madaktari hapa na pale wasiondokane na shida zao, kumbe wengine waliacha dawa nyumbani kwa kutokujua, laiti wangejua wangefurahia maisha bila machungu ambayo yamewatatiza kwa muda mrefu. Maumivu mengi yawe ya kichwa, viungo kama kiuno, miguu, mgongo yamesababishwa na uwepo wa maji kidogo katika mwili (dehydration). Wagonjwa hawawezi kuhusisha hili na ugonjwa sababu hakuna aliyewahi kuwaamsha kujua hili.

Daktari mmoja alisema, kama ingetokea fani ya utabibu kushtakiwa mahakamani kwa kosa la kusahau tiba safi kwa wahitaji, basi swali la kwanza hakimu angeuliza kwa madaktari lingekuwa “kwa nini kwa zaidi ya karne 20 mmepuuza kutumia maji kama tiba kwa wagonjwa wenu?”

Nini kinachofanywa na maji mwilini?

Sehemu kubwa ya mwili imechangiwa na maji kiasi cha asilimia 75. Maji haya yanapopungua kwa kiasi kidogo shida huanza. Upungufu hutokea pale kiasi cha maji kinachopotea kutoka mwilini kuwa kikubwa kuliko kinachoingia. Maji yaweza kupotea kutoka mwilini kwa njia ya hewa mtu anapopumua, anapoongea, njia ya mkojo, haja kubwa, na jasho.

Maji husaidia kulainisha viungo, kama grisi ilivyo kwenye vyuma vya gari, baiskeli na kadhalika. Mfano, watu wengi wamezoea kunywa maji wanaposikia kiu. Hii ni kutokuutendea mwili haki. Kwani, hata dereva mwaminifu huwa hawezi kusubiri taa nyekundu iwake ndipo aongeze oili ya injini. Kama mwenye kusoma article hii amewahi kuwa na gari ya dizeli anaweza kukubali kuwa si busara kusubiri taa ya mafuta kuwaka ndipo aongeze dizeli, na anaweza kukueleza madhara yake kwa gari. Msomaji anaposikia kiu ajue kuwa ni taarifa mbaya, ambapo mwili umesubiri mpaka umesema wenyewe kwamba umekaukiwa hauwezi tena kufanya kazi bila maji. Mwenye kiu asipotii taarifa hii mwili utaendelea kupata shida, na kuufanya mwili weneywe usimamishe maji yoyote yaliyo baki yasitoke tena.

Hapa ina maana jasho yawezekana lisitoke tena japo yuko juani, mate katika kinywa huwa mazito yasiyokubali kutemwa kirahisi, mkojo nao huzuiwa kutoka, ukitoka kwa shida lazima pawepo maumivu, tena lazima mkojo huo ukamuliwe na mwili wenyewe ili maji yote yabaki, mkojo ukitoka, basi utoke wa njano yaani ni makapi tu na chumvi nyingi. Tena habari hupelekwa kwenye senta ya maumivu kwenye ubongo ili maumivu yaendelee kukumbusha kwamba mtu huyu anatakiwa afanye kitu, yaani atafute maji.

Maji ni ya muhimu kama kichocheo cha kupunguza uzito uliozidi. Maji husimamisha tamaa ya chakula na pia husaidia mwili kuvunjavunja mafuta yaliyotunzwa mwilini bila kazi. Utafiti unaonesha kuwa maji yakiwa kidogo mwilini hufanya mafuta yalundikane, wakati maji mwilini hupunguza shida hiyo. Figo haziwezi kutenda kazi vizuri bila maji ya kutosha. Figo kazi yake ni kama chekecheo la uchafu, na kwa kupitia mkojo uchafu hutoka. Figo zisipofanya kazi vizuri baadhi ya kazi zake hupelekwa katika ini ambalo pia huchuja sumu. Kimsingi ini linatakiwa kuvunjavunja mafuta yaliyotunzwa mwilini ili yasaidie kutoa nguvu za kutumika kwa kazi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment