Wednesday, February 11, 2009

PERRY WALLACE NA UBAGUZI MAREKANI

Katika somo tuliloandaliwa Jumatatu tarehe 26 Januari, 2009, kulikuwa na Profesa (mwalimu) Perry Wallace (56), Mgeni aliyekuja kutufahamisha kuhusu Maisha ya Ubaguzi Michezoni nchini Marekani (Desegregating the SEC: Race Relations in the United States). Hii SEC kirefu chake ni Southeastern Conference, ambayo kwa nyumbani Tanzania, tunaweza kuifananisha na Ligi ya Kanda ya Soka. Mwalimu huyu ni Mmarekani Mweusi, anatoka katika jimbo la Tennessee katika mji mkuu wake wa Nashville. Jimbo la Tennessee liko kusini mwa Marekani, kulikojichimbia ubaguzi sana kutokana na historia yake ya kuwa na mashamba mengi ya kilimo, na hivyo Watumwa wengi walikuwa kusini ya Marekani zaidi ya walivyokuwa katika majimbo ya Kaskazini.

Habari zake mwalimu huyu za kufanikiwa katika mchezo wa Mpira wa Kikapu (Basketball) na heshima aliyotunukiwa mwaka 2008 na hiyo SEC zimeandikwa na Jack Carey, katika gazeti la USATODAY (www.USATODAY.com) la Januari, 2009. Habari hiyo ina kichwa cha habari kisemacho "An SEC Trailblazer gets his due". Mwalimu huyu alitunukiwa heshima hiyo Januari 24, 2009, miaka zaidi ya thelathini (30) baada ya kung'ara kimichezo.

Mwalimu huyu alizaliwa katika mji wa Nashville alikokulia na kusomea. Hata hivyo alifanya vizuri sana shuleni (alipata A masomo yote) na aling'ara sana katika mchezo wa mpira wa kikapu na hivyo kupata fursa ya kuchaguliwa kuingia chuoni (kwa ufadhili wa mchezo wake zaidi kuliko ubora wa taaluma yake). Kwa kauli yake mwenyewe, hakutegemea kuendelea sana na shule baada ya kumaliza Nashville Pearl High School kwa kuwa alitoka familia duni na kwa kuwa alikuwa ni mweusi, na weusi wakati huo hawakupata fursa za kuendelea na masomo, zaidi ya kuchaguliwa kwenda kusomea Ualimu ili waje kufundisha shule za wanafunzi weusi.

Baada ya kuingia katika chuo cha Vanderbilt na kufaulu vizuri huku akicheza mchezo huo, alifanikiwa kupiga hatua zaidi hadi kufikia kupata digrii ya sheria toka Columbia School of Law mwaka 1975. Mwalimu huyu aliendelea na masomo na michezo katika kipindi kigumu sana cha Ubaguzi wa rangi katika majimbo ya kusini. Anaeleza mwenyewe jinsi wazazi wake walivyokuwa wanapigiwa simu za chuki na matusi na vitisho (walimficha, hawakumwambia), jinsi yeye mwenyewe alivyokuwa anatemewa mate uwanjani na kutupiwa vitu vya kumdhalilisha, na katika yote hayo, hakuonyesha hasira hata mara moja kwa sababu kwa kauli yake, "nilikuwa nakazania malengo yangu ya kudhihirisha kuwa Weusi wanaweza kufanya maajabu katika masomo na michezoni pia!".

Hivyo kwa heshima yake kwa shule aliyoichezea miaka ya sitini (1960s), ndio sasa mwaka 2008 amekuja tambuliwa kwa heshima hiyo aliyotunukiwa na SEC. Zaidi ya miaka thelathini (30). Maana ya heshima hii kwa huku ni hivi. Jezi aliyokuwa anachezea Na.25 inasitishwa kuchezewa na mchezaji mwingine yeyote katika timu ya shule yake. Jezi hiyo Na. 25 inawekwa katika fremu na kutundikwa katika kuta za SEC (Vanderbilt) pamoja na picha yake, kuonyesha kuwa katika mahala hapo aliwahi kuwepo mchezaji huyo aliyestahili heshima hiyo. Profesa Perry Wallace ana umri wa miaka 56 sasa wakati anatunukiwa heshima hii. Mwenyewe anadhihirisha kuwa hakudhani hata siku moja kuwa anaandika Historia. Amesema anaona tu kana kwamba historia ilimshika mkono na akajikuta katika mkondo uliomsaidia kufikisha misingi bora ya maisha ya binadamu nchini mwake Marekani.

Katika kutoa vidokezo alipoulizwa maswali, Mwali Wallace alisema huku Marekani kuna sheria isiyoandikwa iitwayo ONE DROP RULE. Maana yake ni kuwa, hata ukiwa mweupe kiasi gani, ukiwa na ishara moja tu inayojidhihirisha kutoka kwa watu weusi, wewe unasajiliwa kuwa ni Mtu Mweusi. Huku Marekani, kwa maana ya Takwimu zao, kuna makundi matatu ya watu. Weupe, Weusi, na Latino. Hawa Latino ndio wale "wenye nchi" wenye asili ya Wahindi Wekundu waliokuwa ndio wazalendo kabla ya watu wengine kuhamia Marekani baada ya "ugunduzi" wa bara hili na Vasco da Gama. Japo idadi kubwa ya Latino huku wanachukuliwa kuwa ni Wahamiaji toka nchi za jirani za bara la Amerika Kusini, lakini Latino hawa hawana tofauti na Wahindi Wekundu wenzao wazalendo wa Marekani. Hivyo kwa wageni kama sisi, tunaowaona kama wote ni sawa tu.

No comments:

Post a Comment