Wednesday, February 11, 2009

GHARAMA YA KUJIFUNGUA KWA KAWAIDA MAREKANI NI $7,000

Mwalimu wetu wa Sheria za Afya (Health Law) Chuoni American University, Washington College of Law (WCL) Profesa David Chafkin katufahamisha darasani jana tarehe 10/2/2009 kwamba gharama za kujifungua za kawaida kwa mzazi wa kawaida asiyepata matatizo yoyote katika kujifungua huko hulipa dola elfu saba (US$7,000). Endapo inatokea kuwa mzazi akapatwa na matatizo mengine katika kujifungua huko, mathalan, kama atajifungua kwa kisu (Caesarian section) au kama kuna dharura nyingine yeyote inayoweza kujitokeza wakati wa kujifungua, basi gharama hiyo itazidi.

Kung'oa jino moja huku Marekani ni Dola 1,000 (US$1,000). Hayo yalimkuta mwenzetu mmoja kutoka China Bw. Hwang Wei. Katika mikataba yetu ya Ufadhili, huwa inasema wazi kuwa bima yake ya afya haitoi huduma kwa magonjwa ya kinywa na macho. Hivyo mwenzetu huyu alipofika huku Washington DC na kuishi miezi mitatu, akaugua jino (gego). ndio hilo lililomgharimi dola elfu moja. Fedha hiyo kalazimika kuitoa mfukoni mwake kwa sababu ugonjwa huo haumo katika Bima ya Afya tuliyokatiwa tukiwa huku masomoni.

Mimi mwenyewe nilipata bahati mbaya ya kuteguka mguu tu nikapelekwa Sibley Memorial Hospital iliyopo kwenye Kitongoji kiitwacho "The Palisades" jirani na ninapoishi. Hapo gharama ya Mapokezi (dharura) ni peke yake. Gharama ya X-ray ni tofauti na gharama ya kitanda na dawa tofauti. Nashukuru kuwa sikuwahi kulazwa, nilipimwa x-ray na baada ya kuhakikisha kuwa sikuvunjika mguu, nikaruhusiwa baada ya kuwekewa Crepe Bandage na kupewa mikongoja miwili inisaidie kutembelea kwa wiki moja. Sikupewa hata aspirini.

Kwa maana hiyo gharama niliyoletewa na Hospitali hiyo ya $450 (Dola mia nne na hamsini)(makisio fedha za nyumbani Tanzania ni kama Tshs.450,000/=) ndio imejumuisha huduma hizo za x-ray, crepe bandage na mikongoja miwili.

Baada ya Profesa kutoa somo la jinsi huduma ya tiba ilivyo imedorora sana Marekani kulinganisha na nchi zingine duniani (alisema na utajiri wake wote ilionao, USA ni ya 39), nami kufahamu ughali wa huduma hizo kwa undani, ndio nikathibitisha na kufahamu ni kwa nini Wamarekani wanahofia sana ugonjwa wa aina yoyote. Kumbe wanahofia gharama za matibabu yake! Jitihada zote zinazofanywa na Chama cha Democratic kiwapo madarakani tangu 1905 kuanzisha utaratibu wa Huduma ya Afya kwa Umma zinakwama na zinagonga mwamba, kwa sababu hii ni nchi ya Kibepari na Wabunge wa Republican na wadau wengine wanahakikisha sheria kama hiyo haipiti.

Maana mwalimu huyu alisema hata Kiwanda kama cha Ford cha Magari kule Detroit, Michigan kinashindwa kupunguza bei za magari yake na kushindana na Viwanda vya Japan vya Magari kwa sababu ya kuwalipia gharama kubwa sana wafanyakazi wake Bima zao za Afya.

Hivyo tusidhani kuwa watu wa Marekani kwa sababu ni Taifa kubwa na kwa kuwa ni tajiri sana, watu wake wana unafuu wowote kwa upande wa Afya. Mwalimu alisema kuwa inakadiriwa nusu ya Wamarekani wote hawana Bima ya Afya, jambo ambalo ni hatari kwa maisha kwa waishio huku kwa sababu hutapata huduma bora na kamilifu ya afya endapo unategemea kujilipia toka mfukoni mwako kutokana na uzito wa gharama.

Hivyo tusifikirie kuwa kwa kuna watu wanaishi huku basi wana raha sana. Kwa kweli wengine wana shida kuliko sisi tulio katika nchi zinazoendelea.

No comments:

Post a Comment