Gazeti Dada la Washingtonpost , EXPRESS la Ijumaa TAREHE 30 Januari, 2009 limemuonyesha Rais Barack Obama na mkewe Michelle Obama wakifika katika shule asomayo binti yao mdogo wa miaka saba Bi Sasha Obama, shule ya sidwell Friends iliyopo katika Tarafa ya Bethesda, Maryland.
Ugeni huo ulikuwa umekwenda kumsikiliza binti yao huyo (ambaye kwa umri wake ni sawa na binti wa darasa la Kwanza nchini Tanzania) akitoa mada darasani kwake (presentation). Katika msafara huo pia alikuwa bibi yake Sasha mzaa mama Bi. Marian Robinson.
Kwa wenzetu huku Marekani, mtoto anapotoa mada kama hivyo, wazazi kuhudhuria ni jambo la muhimu.
Lakini la kushangaza zaidi na la kupendeza na kusifiwa, ni kuwa watoto tangu darasa la kwanza wanafundishwa kutayarisha mada zao wapendazo na kuziwasilisha darasani mbele ya wenzao. Hili ni somo zuri sana la kuigwa kwa vijana wetu pia.
Kwa ufahamu wangu mdogo wa Saikolojia, naamini jambo hili linawajengea uzoefu watoto wao kuweza kuzungumza kadamnasi bila woga, kujiamini na kujiandaa kutayarisha kitu cha kuweza kuzungumzia. Vile vile kutoa mawazo na maoni yao juu ya mambo mbalimbali juu ya maisha yanayowazunguka.
Walimu nchini Tanzania na Afrika, mpo? Hii ni changamoto kubwa sana kwetu!
No comments:
Post a Comment