JK amtimua kazi DC aliyechapa walimu
KUTOKA GAZETI LA NIPASHE
2009-02-14 10:39:02
Na Waandishi Wetu, Dar na mikoani
Rais Jakaya Kikwete, amemvua madaraka na kumfukuza kazi Mkuu wa Wilaya ya Bukoba (DC), mkoani Kagera, Albert Mnali, kutokana na kitendo cha kuwacharaza bakora walimu wa shule za msingi wa wilaya hiyo.
Habari zilizopatikana jana usiku kutoka ofisi ya Waziri Mkuu zilisema kwamba Rais alichukua hatua hiyo kutokana na mkuu wa wilaya hiyo kufanya kitendo ambacho hakikubaliki, kinadhalilisha na kuwaua moyo waalimu kufanya kazi.
Akiongea na Nipashe kwa njia ya simu, Mwandishi katika ofisi ya Waziri Mkuu, Irene Bwire, alisema kwamba madaraka ya DC huyo yalitenguliwa rasmi kuanzia jana.
Mnali anadaiwa kuwaamrisha polisi kuwacharaza viboko walimu hao kutokana na kusababisha wanafunzi kufeli mitihani pamoja na kuchelewa kazini.
Katika taarifa ya kumfukuza kazi DC huyo, Rais alisema kulingana na taratibu, kamati za nidhamu za wilaya na mikoa ndizo zenye majukumu ya kutoa adhabu kwa wafanyakazi wa umma kama ikionekana inafaa na kwamba kitendo alichofanya mkuu huyo wa wilaya kimekiuka kanuni hiyo.
``Amevunja kanuni na ameidhalilisha ofisi na mamlaka ya ukuu wa wilaya,`` sehemu ya taarifa hiyo ilisema kama ilivyosomwa na Bwire.
Mapema jana, Waalimu karibu nchi nzima walilaani vikali kitendo kilichofanywa na Mkuu huyo Wilaya wakisema kimewadhalilisha na ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Baadhi ya walimu mkoani Ruvuma, walitoa malalamiko yao kwa masharti ya kutotajwa majina, wakisema kitendo hicho alichokifanya DC huyo ni kinyume cha sheria na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Walisema kuwa kitendo hicho kimewadhalilisha sana walimu, si wa watanzania tu bali wa dunia nzima na kwamba haijawahi kutokea walimu kucharazwa bakora na kuongeza kuwa Mnali ameonyesha wazi kuwa amejichukulia madaraka mikononi kwa kutumia cheo chake.
Baadhi ya wakuu wa shule za sekondari mkoani Ruvuma ambao walikuwa kwenye mkutano wa kuboresha elimu ya sekondari mjini hapa, walisema kuwa ipo haja sasa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuchukua hatua za haraka za kumuajibisha Mnali ambapo walitishia kutotamuunga mkono endapo atachelewesha kulitolea maamuzi jambo hilo, ambalo limewakatisha tamaa walimu nchini.
Walimu hao walisema kuwa Mkuu huyo wa Wilaya kabla ya kujichukulia sheria mkononi, alipaswa kutafuta kiini cha tatizo lililosababisha wanafunzi kufeli na kwamba wilaya yake inawataalam waliobobea, wakiwemo maafisa elimu na Katibu waTume ya Utumishi ya Walimu (TSD) ambao wangeweza kumpa ushauri wa kitaalamu na kujua ni kwa nini wanafunzi wamefeli na adhabu ya kuwapa walimu na si vinginevyo.
Naye Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Ruvuma, Luya Ngonyani, alisema kuwa kitendo alichofanya Mnali, kimewasononesha na kuwadhalilisha walimu wenzao na kwamba wanaamini taratibu zingine za kisheria zitafuatwa ili kurejesha utu na heshima ya walimu pamoja na utumishi wao.
Alisema wameunga mkono taarifa ya Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwamtumu Mahiza, ya kumtaka DC huyo akapimwe akili kabla ya taratibu zingine kufuatwa.
Nyanda za Juu wamuomba JK kumfuta kazi DC
Nacho chama cha waalimu (CWT) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kimemuomba Rais Jakaya Kikwete kutengua wadhifa wa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Albert Mnali, na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa askari polisi aliyetekeleza amri isiyo halali.
Akizungumza na waaandishi wa habari ofisini kwake jana, Katibu wa CWT Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Tweedsmuir Zambi, alisema chama chao kinalaani kitendo cha Mkuu wa Wilaya hiyo kuamuru walimu wachapwe viboko.
Alisema wanamwomba Rais Kikwete amfute kazi Mnali na pia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, amchukulie hatua za kinidhamu polisi aliyetekeleza amri isiyo halali, ya kuwachapa viboko walimu.
Aidha, alisema chama hicho kinamwomba mwajiri wa walimu hao waliochapwa viboko agharimie uhamisho ili kulinda hadhi ya walimu hao kwa kuwa wameathirika kisaikolojia.
Moshi wataka DC ashughulikiwe
Kwa upande wake CWT mkoani Kilimanjaro kimeiomba serikali kumchukulia hatua za kisheria Mnali kutokana na kuwadhalilisha walimu kwa kuwacharaza viboko kwa madai ya kushusha kiwango cha elimu wilayani mwake.
Kaimu Katibu wa CWT, Dauson Temu, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa na kuongeza kuwa kitendo hicho kimewadhalilisha walimu na kuwashushia heshima mbele ya wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Alisema CWT kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hizo na kinalaani vikali kitendo hicho kwani si cha kiungwana wala taratibu za ajira na utawala bora na kuwa kimewaathiri walimu kisaikolojia.
Temu alisema wanaiomba serikali kukemea tabia hiyo na kumwadhibu Mkuu huyo wa wilaya na isitokee kwa kiongozi mwingine wa serikali kutumia vibaya madaraka yake na kuwa walimu watapanga kufanya maandamano ya kupinga kitendo hicho.
``Serikali imchukulie hatua kwani taswira ya sasa inaonekana hadhi ya walimu itashuka hata mbele ya wanafunzi wanaowafundisha na tabia hii isipoangaliwa mapema hata watendaji wa vijiji watawachapa walimu makonde na viboko kwa tuhuma kama hizo,`` alisema Temu.
Alisema Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imewahi kushika mkia mara sita mfululizo mkoani hapa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba kuanzia mwaka 1994 hadi mwaka 2000 lakini wadau mbali mbali walikutana na kuondoa kasoro zilizopo na sasa wilaya ya Hai inapeta katika matokeo hayo kila mwaka.
Alisema Mkuu wa Wilaya ya Bukoba hanabudi kutembelea Mkoa wa Kilimanjaro na kujifunza namna mbalimbali za uboreshaji wa elimu katika wilaya yake na si kuwaadhibu walimu pekee, tena kwa adhabu ya aibu ya viboko.
Kaimu huyo alisema toka nchi imepata uhuru wake, hajawahi kusikia kokote duniani mwalimu kuchapwa viboko kwa sababu ya wanafunzi kufeli na kwamba tukio hilo limeweka historia nchini na duniani.
Zaidi ya walimu 32 wa wilayani Bukoba wameripotiwa na vyombo vya habari wakidai kucharazwa viboko na Mnali.
Tume ya Haki za Binadamu yalaani Wakati huo huo, TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, imelaani kitendo cha Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Albert Mnali cha kuwachapa viboko walimu wa shule tatu za msingi, wilayani humo, ikisema kuwa kitendo hicho ni ukiukwaji wa haki za binadamu na kimedhalilisha utu na kuwavunjia heshima kwa wanafunzi, familia zao na jamii kwa jumla.
Walimu walioripotiwa kuchapwa viboko na Mkuu huyo wa Wilaya, ni wa Shule za Msingi za Katerero, Kanazi na Kasenene mkoani Kagera.
Tamko hilo lilisomwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mahfoudha Alley Hamid, kwa niaba ya Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Amiri Manento, alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Tume hiyo, jijini Dar es Salaam jana.
Jaji Mahfoudha alisema Tume imeshitushwa na kusikitishwa na taarifa kuhusu kitendo kilichofanywa na Mkuu huyo wa Wilaya dhidi ya walimu hao.
``Kitendo hicho ni cha ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa mujibu wa sheria za nchi hususan Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na mikataba ya kimataifa inayolinda haki za binadamu na misingi ya utawala bora ambayo Tanzania imeridhia,`` alisema Mahfoudha.
Alisema Ibara ya 13 (6) (e) ya Katiba inatamka kuhusu adhabu kwa kusema: ``Ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.``
Kutokana na hali hiyo, alisema Tume, ambayo ina mamlaka ya Kikatiba, inalaani vikali kitendo kilichofanywa na Mkuu huyo wa Wilaya, ambaye moja ya majukumu yake ni kulinda hazi za binadamu na misingi ya utawala bora.
Alisema uvunjaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora uliofanywa na Mkuu huyo wa Wilaya ni pamoja na kutoa adhabu isiyostahili kwani adhabu ya viboko hutolewa na mahakama peke yake tena kwa kosa la jinai lililoainishwa kisheria.
Pia kutoa adhabu ya kutweza au kudhalilisha utu, ikiwamo walimu wa kike kucharazwa bakora, kuwapa adhabu walimu bila kufuata taratibu za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha maafisa elimu wa wilaya na Idara ya Utumishi wa Walimu na kutumia vibaya madaraka aliyokasimiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na akala kiapo.
Alisema kitendo hicho alichokiita cha aina yake na cha aibu nchini, kimeleta athari kubwa kwa walimu, ikiwamo kuwavunjia heshima kwa wanafunzi, familia zao na jamii kwa jumla na pia kimewavunja moyo katika kazi zao za kila siku.
Hata hivyo, aliwataka walimu kuzingatia maadili yao ya kazi ili nao wawatendee haki watoto ya kupata elimu bora, badala ya kuwa watoro, wazembe na walevi kama walivyotuhumiwa.
Imeandikwa na Gideon Mwakanosya, Ruvuma Jackson Kimambo, Moshi Pendo Fundisha, Mbeya na Muhibu Said, Dar.
No comments:
Post a Comment