Saturday, February 7, 2009

JAJI MKUU ALALAMIKIA WATU KUIINGILIA MAHAKAMA


Mwandishi Wetu
Daily News; Friday,February 06, 2009 @18:20

Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhani, ametaka Idara ya Mahakama isiingiliwe na mtu yeyote katika kutoa uamuzi wa kesi. Amesema imejengeka tabia sasa miongoni mwa watu hususan katika kipindi hiki cha kusikilizwa kesi za ufisadi, kutoa hukumu dhidi ya washitakiwa kabla mahakama haijafanya hivyo.

Jaji Mkuu amesema watu hao wanasahau kuwa mshitakiwa mbele ya sheria si mhalifu na kwamba hukumu hizo zinaleta mtazamo tofauti mara mahakama inapomwona mtuhumiwa hana hatia.

Jaji Mkuu alisema hayo jana, Dar es Salaam, mbele ya Rais Jakaya Kikwete, katika maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, ambapo alimmwagia sifa Rais kwa kile alichosema hajawahi kuingilia uhuru wa mahakama tofauti na waliomtangulia.

“Awali ya yote, ninachukua fursa hii kukiri kwa dhati, kwamba muda wote wa miaka mitatu na ushei wa uongozi wako, hujaingilia uamuzi wa mahakama kwa matendo wala kauli, waliokutangulia waliwahi kuteleza na kuvunja mwiko huo. Lakini hatuwazungumzii hao, na isitoshe yaliyopita si ndwele,” alisema Jaji Mkuu.

Aliongeza: “Hivyo ndugu zangu majaji na mahakimu, tumpongeze kwa kishindo Rais Kikwete kwa kuwa muumini na kielelezo cha kuheshimu dhana yamgawanyo wa madaraka kwa vitendo na kauli,” alisisitiza.

Kauli hiyo ya Jaji Mkuu ilitoka kwa kuzingatia kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku hiyo, iliyozungumzia nafasi ya Mahakama katika kutekeleza shughuli za mamlaka ya nchi, kulingana na dhana ya mgawanyo wa madaraka, alitaja baadhi ya matatizo yaliyowahi kuwakumba kuwa ni pale Bunge lilipoingilia kazi za mahakama.

Bila kujali uwapo wa Spika wa Bunge, Samuel Sitta katika hafla hiyo, Jaji Mkuu alisema mhimili huo uliwahi kutaka uwe na madaraka ya kimahakama dhidi ya watu ambao wanazozana na wabunge, lakini wazo hilo halikufanikiwa.

“Ingawa ni kinyume cha utaratibu, lilichukua (Bunge) kazi ya Mahakama ya kusikiliza tatizo kati ya Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima na Reginald Mengi (Mwenyekiti Mtendaji wa IPP) ambaye si mbunge,” alisema Jaji Ramadhani.

Aidha, alisema Spika Sitta katika kile alichokiita kughafilika, aliwahi kutoa matamshi kuhusu sakata la mafuta ya petroli Morogoro, baada ya amri ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ya kuvifunga vituo kadhaa vya mafuta, ilipositishwa kwa muda na Mahakama ya Hakimu Mkazi.

“Kauli hiyo ingetolewa ndani wala si nje ya Bunge ingekuwa stahili yake,” alisema Jaji Mkuu na kuongeza, kuwa kutokana na hilo azma ya mahakama ni kufanya mabadiliko ya kutafuta njia ya kuleta mkabala murua, baina ya mihimili miwili mingine ya Dola, kwa kuomba siku ya kukaa pamoja baina ya viongozi wakuu, yaani Rais, Spika na Jaji Mkuu na kuzungumza kwa faragha.

Akizungumzia maslahi ya watumishi wa Mahakama, mafanikio na changamoto zinazoikabili, alisema kwa miaka 10 sasa, kila Februari mbili ni Siku ya Sheria ambayo inaanzisha mwaka wa utekelezaji wa shughuli za Mahakama. Alisema mwaka jana, Tume ya Utumishi ya Mahakama, ilitembelea mikoa mbalimbali na kukutana na wananchi na kamati za nidhamu za mikoa.

Mwaka huu ilifanyika Februari sita kutokana na Rais kuwa katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU), Addis Ababa, Ethiopia. Kuhusu changamoto, alisema bado wanakabiliwa na uchache wa mahakimu katika ngazi za mahakama za mwanzo na pia ufinyu wa bajeti ambapo alimwomba Rais Kikwete kusaidia ili serikali iongeze bajeti ya mwaka ujao wa fedha (2009/10) ambayo alisema wamepata takwimu kwamba itapungua zaidi ya Sh bilioni 21.08 ya mwaka huu na kuwa Sh bilioni 20.03, Rais Kikwete aliahidi kulishughulikia.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida kwa Rais kuzungumza katika hafla kama hiyo, jana utaratibu huo ulivunjwa, baada ya Rais kuombwa na Jaji Mkuu atoe salamu na kutumia fursa hiyo kutoa hotuba fupi akieleza kuwa ilitokana na yeye kuguswa na hotuba ya Jaji Mkuu.

Katika hotuba yake, aliipongeza Mahakama kwa kazi nzuri na ngumu waliyonayo ya kutekeleza haki na kuahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yote waliyoyatoa kwake, ya kuimarisha uhuru wa Mahakama na maslahi yao. Aliwataka wakati serikali ikitekeleza hayo, wao wadumishe uadilifu na uchapakazi ili kupunguza adhabu ya maswali yasiyo ya lazima wanayopata wanasiasa wakati wakiomba kura kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment