Wiki ya jana, siku ya Alhamisi tarehe 5 Februari, 2009, nililazimika kwenda kwa Kinyozi kunyoa nywele kipara. Nililazimika kwa sababu chanuo lilikataa kupita kabisa kichwani, kwa maana ya kuwa nywele zilishakuwa sana. Nililazimika kunyoa kipara ili kujihami na matumizi ya fedha kwa kazi hiyo. Huku Marekani (Washington DC) nimefanikiwa kunyoa kwa Dola 17 ($ 17) (ambazo kama nyumbani kwa ukadiriaji ni zaidi ya Tshs. 17,000/=), na hiyo ni asilimia ishirini (20%) pungufu (Discount) inayotolewa kwa Wanafunzi, mradi uwe na Kitambulisho chako tu. Hivyo, kwa mtu wa kawaida kwenda kukata au kunyoa nywele ni Dola 19 ($19) walivyoniambia kwa mahesabu yao.
Kwa hiyo, ili kukwepa kulipa dola 17 ($17) zingine kabla sijarejea nyumbani, ndio nikaamua kunyoa kipara kabisa. Ili kwamba ifikapo tarehe ya mimi kurejea Tanzania Juni, 2009, nisihitaji kunyoa tena hapo katikati. Ndio maana nasema hii ni mkakati wa kujihami kiuchumi. Kwa sababu gharama hii ni kubwa mno kwa mtu yoyote wa kawaida kuilipia. Ukijibana sana Dola 17 inaweza kuwa ni matumizi ya mlo wa siku mbili kwa huku. Nyumbani kwa huduma kama hii hii kwa sasa najua ni Tshs.500/= tu.
Mwenye nyumba wangu Bwana Edward (Ted) Mario Vlach, ambaye ni Mmarekani Mweupe; aliwahi kunifahamisha katika mazungumzo kuwa endapo ningehitaji huduma ya kinyozi, yeye atanipeleka kwa kinyozi wake ambaye aliniambia kuwa humnyoa yeye kwa Dola 15 tu ($15). Huyu ni Kinyozi wa Uswahilini ambaye hahitaji kuwekeana miadi (appointment). Kwa vinyozi wa miadi hata sijui wanatoza kiasi gani. Siku ilipowadia na nilipomtolea maombi, akanijibu kuwa Kinyozi wake hana uzoefu wa kunyoa vichwa vyenye nywele kama zangu za kipilipili. Bila shaka aliwasiliana na kinyozi wake kwanza na akamuuliza endapo anaweza kuninyoa mimi.
Hapo ndipo nikang'amua kuwa kumbe huku Marekani, kuna ubaguzi hata katika shughuli pevu kama ya kunyoa. Hivyo ni wazi kuwa pamoja na utawala wa Rais mpya Barack Hussein Obama Mmarekani Mweusi, bado kazi ipo kubwa tu ya kubadilisha hisia za watu katika mashirikiano yao ya kila siku.
Tumshukuru Mungu tumezaliwa Tanzania (Afrika) na kubaki huko. Ni heri sana huu umasikini tulionao na tunaishi kwa misingi ya kuwa wote binadamu tuko sawa huko kwetu, kuliko huku jinsi wenzetu wanavyoishi kwa hisia za kuchukiana, kubaguana, kuogopana, kuoneana kinyaa, ili mradi kwa ujumla wake binafsi naona ni maisha ambayo hayana amani ya kweli moyoni.
Nimefurahi kuiona blog yako,nafurahi akina mama tukijumuika na akina baba kutoa elimu kwa njia hii. Blog yako nzuri nimeiona kupitia blog nyingine niipendayo ya Prof. Mbele.
ReplyDeleteKuhusu hili la kunyoa nywele sioni kama ni ubaguzi wa rangi ila naona huyo kinyozi amekuwa mkweli tu kuwa hajui kukata nywele kama zetu maana angekubali harafu akakukata nywele vibaya kwa kutokuwa na uzoefu nazo nafikiri usingefurahi na labda ingekugharimu peza zaidi kuenda kurekebisha. Ni sawa na dada wa Kizungu aende Salon Tanzania akitaka kusuka mistari au rasta nina uhakika mia kwa mia kuna salon watakataa kwa kutozoea kusuka nywele za aina hiyo, hapo sijui wao utawaweka kundi gani wabaguzi au wamesema ukweli?.Huo ndio mtazamo wangu.