Tuesday, February 3, 2009

HUDUMA ZA JELA MARYLAND, USA

Ijumaa ya Tarehe 30/1/2009 tulitembelea jela moja iliyo jimboni Maryland iitwayo Montgomery County Correctional Facility (22860 Whelan Lane, Boyds, Maryland 20841, USA). Kwa tafsiri ya Kiswahili ya jina hilo lingesomeka "Asasi ya Kurekebisha Tabia". Wameiita hivyo makusudi.

Hii kweli ndio shughuli zake; pamoja na kwamba mna wafungwa katika asasi hii, lakini wao wamebadilisha mfumo wa kuishi na wafungwa hao. Watumishi wote wa ndani ya gereza hili hawaitwi "Prison guards - Askari Magereza", wao wanaitwa Maafisa Warekebishaji. Kazi yao akifika mfungwa yeyote hatua ya kwanza anaambiwa wao hawahusiki na kosa alilolifanya wala hawatalitazama kwa macho ya kumuona mfungwa kama mkosaji na hivyo kumuondoa hisia za kujihis ikukandamizwa kisaikolojia.

Kuna kiti cha tekinolojia ya kisasa (bei yake $50,000) ambayo inatambua chuma chochote kilichomo mwilini mwa binadamu. Ofisa Mkuu aliyetutembeza katika jela hiyo alitufahamisha kwamba, kuna mfungwa aliyepita alikuwa ameingia jela akiwa na simu tatu (3) za mkononi kazisokomeza njia ya haja kubwa kwa nia ya kuja kuziuza ndani ya gereza kwa wafungwa wenzie kwa sababu ni bidhaa adimu mno. Kiti hicho kilipombaini ujanja wake huo na kuzitoa, taarifa zikawafikia wahalifu wengine nje ya gereza na sasa ofisa huyo ametuambia hawana tatizo hilo tena. Wafungwa wanaingia wasafi.

Gereza hilo lina kila kitu cha tekinolojia ya kisasa kuhusu ulinzi wa wafungwa, maafisa, jengo na mali zilizomo. Hata sisi wageni wakati tulipoingia sehemu nyeti tulitakiwa kupigwe picha kwanza ndio tuingie ndani. Humo tulionyeshwa sehemu ya "hospitali" ya jela hiyo ambamo mlikuwa na mashine mbili (2) za kufyonza majimaji yanayohifadhiwa na mafigo (dialysis machine) pamoja na vifaa vingine vingi tu. Bei ya mashine hizi kila moja ni $500,000.

Afisa Mkuu ametufahamisha kuwa gereza hilo limegawanyika katika sehemu nne:
1. Wafungwa waliopo katika uangalizi wa kati (medium security)
2. Wafungwa waliopo katika uangalizi wa hali ya juu (maximum security)
3. Sehemu ya Gereza la Wanawake
4. Sehemu ya Gereza la Vijana kati ya umri wa miaka 18 hadi 23.

Hawa vijana ndio wanafaidi zaidi kwa sababu sehemu yao ya gereza imewekewa simu, wanaweza kuzungumza na wazazi na ndugu zao nje ya gereza wakati wowote. Vijana hawa wamewekewa kiwanja cha kufanyika mazoezi ya Mpira wa Kikapu. Pia wanajitegemea kwa kufua nguo zao wenyewe na kuosha vyombo kwa kuwekewa mashine za kufanya kazi hizo.

Wakati huo huo wafungwa wote wanapewa fursa za kusoma Kompyuta, masomo ya ufundi, lugha, masomo ya kujiandaa na kutafuta kazi, na masomo mengine. Tena kuna Maktaba gerezani hapo kwa ajili ya wafungwa naweza kuifananisha na maktaba yoyote ya Mkoa nchini Tanzania. Ndani ya Maktaba hiyo, kuna maktaba ndogo kwa ajili ya wasomao sheria.

Gereza hili ndilo pekee lenye huduma za Afya kwa jimbo hili, hivyo wafungwa wote wauguao huko waliko huletwa katika gereza hili ambapo madaktari bingwa na vifaa vya tiba vya kisasa vinapatikana.

Pana mtaalam ambaye kazi yake kuwafundisha Wafungwa namna ya kuomba kazi baada ya kumaliza vifungo vyao. Anawafundisha jinsi ya kuonekana nadhifu, lugha ya kutumia katika Mahojiano ya kuomba kazi, namna ya kuandika barua za maombi na Wasifu wao, na jinsi ya kutumia kompyuta hasa intaneti katika jitihada za kutafuta nafasi za kazi.

Pia Gereza hili linatoa huduma ya Kitambulisho kwa kila Mfungwa atokaye salama salimini. Kitambulisho hiki huruhusiwa kutumika katika siku 60 za mtu kuwa huru. Kitambulisho hiki kinamsaidia mtu huyo kutumia usafiri bure, kuombea kazi, na mambo mengine mengi tu ambayo bila kuwa nacho mambo yangemuwia vigumu.

Afisa Gereza Mkuu alietutembeza ametufahamisha kuwa katika miaka yake nane aliyokuwa hapo hapajawahi kutokea matatizo ya wafungwa kwa wafungwa kupigana, kujaribu kuruka ukuta (kutoroka), wala kukosana na wafanyakazi. Kwa kauli yake mwenyewe, amesema kazi hiyo anaipenda sana na anafarijika sana anapotokea kusalimiwa barabarani na wafungwa waliogeuka raia wema (asilimia 60) wanaomkumbuka (japo yeye hawakumbuki kwa wingi wao) na kumhakikishia kuwa sasa wamejirekebisha na wamekuwa na familia zao na wanaishi uraiani salama. Asilimia 20 ina uwezekano mkubwa wa kurejea kwa sababu ya kutumbukia katika lindi la uhalifu hata watokapo, na asilimia 20 iliyobaki inaingia kati kwa kati katika makundi hayo mawili.

Gereza hili lina uwezo wa kuchukua wafungwa 1200, hata hivyo wakati tunalitembelea lilikuwa na wafungwa 700. Gereza hili; pamoja na kwamba lipo jimboni Maryland, lakini pia linahifadhi wafungwa watokao Washington DC; mji ambao wamepakana nao kwa sababu tumearifiwa kuwa Washington DC (mji wa makao Makuu ya Serikali ya Marekani) hauna ardhi tena ya kuweza kutosheleza ujenzi wa gereza, hivyo haina gereza lake yenyewe ila hutegemea magereza ya majimbo ya jirani kama hili.

No comments:

Post a Comment