Friday, February 13, 2009

DC BUKOBA ATEMBEZA MKONG'OTO WA BAKORA KWA WALIMU

Date: Thu, 12 Feb 2009 19:20:17 -0500
From: jamesfrequent@gmail.com

Subject: DC ATEMBEZA BAKORA BUKOBA


Na Lilian Lugakingira, Bukoba na Saa Mohammed, Tanga


MKUU wa Wilaya ya Bukoba, Albert Mnali aliamuru polisi mmoja kuwachapa viboko walimu katika shule tatu za msingi zilizo Bukoba, kutokana na wilaya hiyo kuwa ya mwisho katika matokeo ya darasa la saba.


Tukio hilo la aina yake lilitokea juzi wakati mkuu huyo wa wilaya akiwa ameambatana na koplo huyo wa polisi alipowalaza chini walimu hao na kumuamuru askari huyo wa usalama, kuwachapa walimu hao viboko viwili kila mmoja makalioni na mikononi.


Walimu waliocharazwa viboko, tisa wanatoka Shule ya Msingi Katerero, 11 wa Shule ya Msingi Kanazi ambao walichapwa viboko viwiwili kila mmoja na walimu 12 kutoka Shule ya Msingi Kansenene walichapwa viboko vinne vinne kila mmoja.


Akizungumza jana na waandishi wa habari juu ya tukio hilo, mkuu huyo wa wilaya alisema alilazimika kuwatandika viboko walimu hao baada ya kugundua kuwepo uzembe kazini, ikiwemo kuchelewa kufika kazini na kutofundisha kama mikataba yao ya ajira inavyoeleza.


Alisema uzembe huo umesababisha wilaya ya Bukoba kuwa ya mwisho kimkoa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka jana na kuwa uamuzi huo utasaidia kuwakumbusha walimu wajibu wao.


"Nikweli nimewachapa, mara hii nimewachapwa wakiwa wamefungiwa, wakati mwingine watachapwa hadharani," alisema mkuu.


Kitendo hicho cha ubabe kimevuta hisia za wadau wa elimu, kikiwemo Chama cha Walimu Tanzania (CWT), ambacho kimeitaka serikali kumchukulia hatua kali za kisheria mkuu huyo wa wilaya kwa kosa la kuvunja sheria na kuwadhalilisha walimu 32 wa shule mbalimbali za wilaya ya Bukoba Vijijini kwa kuwachapa viboko.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema suala hilo si jepesi na kwamba mkuu huyo wa wilaya ametonesa kidonda kibichi kwa kukitia chumvi hivyo aliyemweka serikalini mkuu huyo ndio atakayemtoa na kumchukulia hatua.


"Hivyo akaona ni bora kuwaadhibu kwani walimu hao wanadai fidia zao serikalini na yeye akaona hakuna wanachokifanya... kwamba hawafanyi kitu ndio maana kiwango cha elimu kimeshuka,'' alisema Mukoba


Alisema kitendo hicho ni cha kibabe ambacho kinatumiwa na watu wanaofuja madaraka yao.


Aliongeza kuwa CWT itatoa tamko rasmi kwa ajili ya kumpeleka mahakamani mkuu wa wilaya huyo wa Bukoba, kutokana na kukiuka haki za binaadamu.


Alisema taarifa hiyo waliipata saa 5:00 asubuhi juzi ofisi yake walipokea barua pepe kutoka katika chama cha walimu, tawi la Kagera iliyoeleza kuwa mkuu wa wilaya anatembelea shule za msingi wilayani kwake na kutoa adhabu ya viboko kwa walimu.


Alisema kuwa baada ya taarifa hiyo uongozi wake ulitembelea shule ambazo mkuu huyo alipita na kukuta walimu hao kwenye vituo vyao vya kazi na walimu hao walithibitisha kutokea kwa tukio hilo.


Alisema kitendo hicho kimewafanya walimu hao kutokuwa na amani darasani na kufanya hata wanafunzi kuwadharau walimu hao na hata kuwacheka wanapoingia madarasani kwa ajili ya kufundisha.


"Kutokana na hatua hii walimu wanaona kuwa hatua iliyochukuliwa ya kuchapwa viboko ni kitendo cha udhalilishaji na uvunjaji wa heshima ya mwalimu mbele ya mwanafunzi na jamii anayoishi ambayo haijapata kuona tangu waanze kazi,'' alisema Mukoba.


Alisema kuwa baadhi ya walimu walioadhibiwa wanafanya kazi bila ya kulipwa kwa zaidi ya miezi sita, lakini madai hayo yanaonekana ni usumbufu na wanalipwa viboko, badala ya kupewa haki zao.


Mwenyekiti wa CWT mkoa, Dauda Bilikesi alisema wanachama wake wanaitaka serikali kuchukua hatua ili kurudisha heshima zao. Alizitaja hatua hizo kuwa ni kulipwa fidia ya kudhalilishwa na kuvunjiwa heshima kwa kuwa walimu wa kike walipigwa makalioni huku nguo zao zikibaki wazi wakati wamelaala wakiadhibiwa, tena na mwanaume mbele ya kadamnasi.


Pia serikali iwaombe masamaha walimu hadharani na kumtaka mkuu wa wilaya hiyo awajibishwe kwa kutumia madaraka yake vibaya, kutenda kosa la jinai kwa kuwachapa walimu kwa kutumia nguvu kubwa ya dola wakiwa kwenye vituo vyao kazi na kwenye majengo ya serikali na pia kuwakashifu walimu kuwa ni mafisadi kinyume na sheria kwa kuwa wanaidai serikali haki zao.


Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Magembe alikiri kuwa na taarifa hyo na kusema kwamba kamwe hawawezi kulivumilia.


"Ni kweli kuna tukio la aina hiyo na nimeshamwagiza mkuu wa mkoa kufanya uchunguzi na endapo ukweli utapatikana, serikali itachukuwa hatua kali dhidi ya wahusika," alisema Profesa Magembe na kuongeza:


"Nchi yetu haiwezi kuongozwa na watu wa aina hiyo na kamwe serikali haiwezi kukaa kimya... mara tu baada ya mkuu wa mkoa kumaliza kazi yake, atatuletea taarifa na sisi tutalifikisha kwa waziri mkuu kwa hatua zaidi kwani hao wote wako chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu".


"Hilo ni tukio la aina yake na lakusikitisha sana kwa sababu binadamu hawezi kuongozwa njia kwa kuswagwa kama ng'ombe... ni lazima serkali ichukue hatua kali dhidi ya wahusika".


No comments:

Post a Comment