Sunday, February 8, 2009

ETI UTAMADUNI UMEPANDISHA GHARAMA ZA MAISHA?

Jamani Mheshimiwa huyu ni dhahiri kuwa Semina ya Ngurdoto haikumsaidia, au alikuwa hajateuliwa wakati wenziwe wakipigwa msasa Ngurdoto, Arusha, Tanzania na Rais Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2006?

Merali Chawe, Kyela
Daily News; Sunday,February 08, 2009 @19:00

MABADILIKO ya tabia na utamaduni katika jamii yamedaiwa kuwa chanzo cha kupanda kwa gharama za maisha na hali ngumu ya maisha iliyopo hivi sasa haisababishwi na Serikali ya Awamu ya Nne. Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Kyela, Japhet Mwakasumi, wakati wa maadhimisho ya miaka 32 ya CCM, ambapo kimkoa yalifanyika Rungwe na kuhudhuriwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Catherine Nao.

Alisema hivi sasa limeibuka kundi la watu linalodai kuwa kupanda kwa maisha kunachangiwa na Serikali ya Awamu ya Nne jambo ambalo si kweli, “mabadiliko ya tabia na utamaduni ndiyo yanayochangia kupanda kwa gharama za maisha".
Akitoa mfano, Mwakasumi alisema katika miaka ya sabini alikuwa akipokea mshahara wa Sh 600 kwa mwezi, ambao kwa wakati huo ulikuwa mkubwa, lakini kutokana na mabadiliko ya tabia na utamaduni, hivi sasa fedha hiyo haiwezi kununua hata kilo moja ya sukari.

“Zamani watu walikuwa wanatoka mijini kufuata mahitaji vijijini, lakini kinachosikitisha hivi sasa hata mchicha watu wanatoka vijijini kuja kununua mjini hivi hapa bado tuseme Serikali ya Awamu ya Nne ndiyo chanzo cha maisha magumu?,” alihoji Mwakasumi.

Naye Mgeni rasmi Nao aliwataka wana CCM Kyela kudumisha umoja na mshikamano ili waweze kukijenga chama na kushiriki katika shughuli za maendeleo. Alisema vyama vya upinzani kwa upande wa Tanzania Bara ni vya mfano wa kuigwa kwa kuwa vimekuwa vikishindana kwa hoja na CCM badala ya kuendekeza vurugu.

"Tutafanya mpango tuje tuwachukue viongozi wa vyama vya upinzani wa hapa Kyela mkawafundishe wenzenu wa Pemba kuwa upinzani ni kushindana kwa hoja na si kwa vurugu,” alisema. Wakati huohuo, zaidi ya Sh milioni tano zilichangwa juzi katika harambee ya kuchangia ujenzi wa ofisi za CCM Kyela, ambapo ujenzi huo utagharimu zaidi ya Sh milioni 500.

No comments:

Post a Comment