Monday, February 9, 2009

SAKATA LA WAZIRI MASHA NA SAGEM !


2009-02-09 10:05:48
Na Mwandishi Wetu, NIPASHE
Uhusiano wa karibu baina ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, na kampuni ya Sagem Securite inayodaiwa kuenguliwa kwenye mchakato wa zabuni za vitambulisho vya Taifa na kumfanya waziri huyo ataharuki, umegundulika.
Vyanzo vya habari ambavyo Nipashe imevipata vimethibitisha kwamba Waziri Masha alisafiri hadi jijini Geneva Uswisi, mwishoni mwa mwaka jana kukutana na wawakilishi wa kampuni hiyo.
Masha akiwa jijini huko baada ya kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi, alikutana na watendaji wakuu wa Sagem na ni baada ya hapo ndipo mvutano ndani ya wizara yake ulipoanza kuhusu kampuni hiyo ambayo iliacha matatizo makubwa nchini Nigeria ambako ilidaiwa kuhonga mawaziri watatu na kusababisha wafutwe kazi na Rais Olusegun Obasanjo na kufunguliwa kesi ya kula mlungula.
Nusanusa za Nipashe zimebaini kwamba Waziri Masha alisafiri kwenda Geneva Oktoba mosi mwaka jana, kuhudhuria mkutano wa wakimbizi kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Uswisi (Swiss Air) akitokea Dar es Salaam.
Kabla ya Waziri huyo kuanza safari hiyo ya kikazi, alikwisha kufanya mawasiliano ya jinsi ya kukutana na wawekezaji hao atakapofika Geneva.
Waziri Masha baada ya kuhudhuria mkutano wa wakimbizi, alifanya kikao jijini Geneva na uongozi wa Sagem wakiongozwa na Mwenyekiti wa kampuni hiyo na Mtendaji Mkuu, JeanLin Fournereaux.
Taarifa za ndani zinasema kwamba kikao hicho kati ya Masha na Sagem kilifanyika Oktoba 5, 2008 kuanzia saa 12.00 jioni hadi saa 2.00 usiku katika chumba cha wageni mashuhuri (suite) chenye namba 0306, hoteli ya Mandarin Oriental.
Vyanzo vyetu vimepasha kwamba katika hoteli hiyo Masha na maofisa wawili wa Sagem walipata chakula cha usiku pamoja.
Kikao hicho kinachoelekea kuwa cha mkakati, kilidumu kwa saa mbili, na kinaelezwa kuwa kilijenga hoja ya kuhakikisha Sagem inashinda zabuni hiyo ya kutengeneza vitambulisho vya Taifa inayotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh bilioni 200.
Taarifa zaidi za kiuchunguzi zinasema kwamba siku iliyofuata, Masha alitembelea zilipo ofisi za Sagem za Geneva huko Max, Schmidheiny, Strasse 202 CH 9435 Heerbrugg, Uswisi kwa mwaliko wa Sagem.
Baada ya kazi hiyo pevu ya maandalizi, Waziri Masha alirejea jijini Dar es Salaam, Oktoba 11, 2008 saa 12.00 jioni.
Hivi karibuni Waziri Masha ameamsha taharuki kubwa nchini baada ya kuvuja kwa taarifa za siri kuhusu mchakato wa zabuni ya vitambulisho vya taifa.
Nyaraka zilizovuja zinaonyesha jinsi Masha alivyoingilia mchakato huo, kiasi cha kuilazimisha timu ya zabuni ya wizara yake kurudia kazi ya utathmini, na kuilazimisha kukata rufaa kwa Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA).
Waziri Masha pia amenukuliwa katika waraka wake binafsi kwenda kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akimlalamikia vilivyo Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kuwa anaingilia kazi za wizara yake bila hata kumjulisha.
Sakata la Masha kuijitosa katika mchakato huo, lilimfanya Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, kuwasilisha hoja binafsi akitaka Bunge kushughulikia kashfa hiyo inayoonyesha wazi kwamba Waziri anavunja sheria ambazo zimetungwa na Bunge.
Hoja ya Dk. Slaa kuhusu Waziri Masha, imepelekwa kwenye Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na hadi mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wake, Wilson Masilingi (CCM), alisema kazi ya kuishughulikia hoja hiyo bado inaendele

No comments:

Post a Comment