Friday, February 13, 2009

DC AMETENDA KOSA LA JINAI NA KUVUNJA HAKI ZA WALIMU

Wandugu,
Haya mambo, kama kweli sheria inachukua mkondo wake(rule of law & due process) sio madogo.Yaani, kama hakulazimishwa kujiuzulu kwa kitendo hiki, basi Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliyemteua ana haki zote za kumfukuza kazi kwa mengi tu yakiwemo:
1. Kumvunjia haki yake ya Msingi Mwalimu (walimu) kwa kutowafikisha katika vyombo vinavyohusika kuwahukumu (Ibara ya 13 (3) ya Katiba yetu Ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
2. Kitendo cha kuwadhalilisha walimu (Ibara ya 12 (1) na (2) ya katiba
3. Kitendo cha kuamua kuwa wamekosa bil a ya kuhukumiwa rasmi (due process) dhidi ya Ibara ya 13 (6)(b) ya Katiba
4. Kitendo cha kuchapwa viboko hadharani mbele ya kadamnasi iliyojumuisha wanafunzi na wanajumuiya ni kinyume cha Ibara ya 13 (6) (b) ya Katiba
5. Mkuu wa Wilaya amefanya kosa la jinai kwa kuwachapa viboko walimu (assault) chini ya Kanuni za Adhabu (Penal Code) hivyo anastahili kushitakiwa na kulipa fidia kwa kosa hilo.
6. Kwa kuwaumiza walimu kwa majeraha ya bakora (injury), ni kosa la jinai chini ya Penal Code na anatakiwa kulipa gharama zote za matibabu watakazogharimia wahanga hao wa bakora.
7. Walimu wamevunjiwa haki yao ya msingi ya Uhuru wa mawazo yao. Hawakupewa fursa ya kujitetea wala kuelezea kwa nini yametokea yaliyotokea (ya kufeli wanafunzi) chini ya Ibara ya 18 (a) hadi (d) ya Katiba.
8. Walimu wamevunjiwa haki yao ya msingi ya kufanya kazi chini ya Ibara ya 22 (1) kwa sababu katika kipindi cha kuuguza majeraha, hawataweza kujitafutia riziki.
9. Kumvunjia haki ya Mwalimu ya Msingi ya kuwa na utulivu yeye na unyumba wake. Fikirieni familia yake imedhalilika vipi mwalimu huyu na wanamwonaje baada ya mkong'oto? Hii haki ipo chini ya Ibara ya 16 (1) ya Katiba.
10. Kutokana na maelezo kuwa baadhi ya walimu hao hawajapata mishahara kwa kipindi cha miezi 6 ni uvunjaji mkubwa wa Serikali wa haki yao ya msingi ya kupata ujira kutokana na kazi waliyoifanya iliyopo chini ya Ibara ya 22(2) ya Katiba.

No comments:

Post a Comment