Sunday, February 15, 2009

AFYA BORA Na. 6

Kutoka kwa Dr. Wilbert Bunini Manyilizu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Tanzania.

Mwendelezo wa article 5

Mtu hawezi kupata mafanikio makubwa japo atafanya jambo lolote jema kwa ajili ya afya yake, kama vile mazoezi na kula vyakula salama iwapo hajahusisha matumizi ya maji mengi katika programu yake. Maji safi na salama ni kitu muhimu cha pili katika miili yetu baada ya hewa. Mtu aweza kuishi kwa siku nyingi akinywa maji tu bila chakula, lakini ataishi siku chache sana akila chakula kikavu tu bila maji. Yawezekana wengi wa wasomaji hufanya kazi zao za kila siku wakiwa katika hali ya upungufu wa maji mwilini na hivyo hupata maradhi mengi yanayoambatana na tatizo hili kama matokeo, ikiwa ni pamoja na kusikia maumivu ya kichwa wakati wa jioni. Kila kazi mwilini hurekebishwa na hutegemea maji.


Maji lazima yawepo kuchukua vitu vya muhimu mbalimbali kwenda viungo tofauti tofauti, hivi ni pamoja na hewa safi ya oksijeni kupitia kwenye damu, kusafirisha homoni mbalimbali, kemikali zingine kwenda sehemu zinakotakiwa mwilini. Baadhi ya sehemu za mwili zilizoko mbali na moyo haziwezi kupata mahitaji yake ambayo husafirishwa kwa njia hiyo. Maji haya hutumika kusafisha mwili kwa kuondoa uchafu na sumu kutoka chembe chembe mbalimbali. Kuna sababu nyingi mno ambazo mwili huhitaji maji ya kutosha ili utende kazi zake vizuri kila siku. Viungo vinapopungukiwa maji hutoa ishara kwa mhusika.


Kemikali iitwayo histamini huzalishwa ili kuanza kuchukua tahadhari kwa maeneo yaliyoathirika kwanza. Hii histamini inapokutana na neva za fahamu husababisha maumivu. Ndiyo maana kiu, au kukaukiwa huleta maumivu kama dalili ya awali. Iwapo kiu haijatulizwa kwa maji huzalisha maumivu ambayo hudumu na kuwa dalili sawa na magonjwa mengine yanayosababisha maumivu.


Mazoea ya kutokunywa maji mpaka kiu inaposumbua yaweza kuwa chanzo cha maumivu ya kichwa, maumivu ya mgongo, kiuno, msongo na mfadhaiko wa akili, shinikizo la damu, kolestero nyingi, na uzito uliokithiri, kukosa usingizi, kujisikia mchovu, hofu, kupata choo kigumu, baridi yabisi na mengineyo. Haya yote yaweza kudhibitiwa mapema kabla hayajatokea. Unywaji wa mara kwa mara wa maji mengi hukufanya uzoee na kudhibiti magonjwa mengi. Japo awali kabla kibofu hakijajifunza na kuzoea hali hii inasumbua kwa kuongeza idadi ya kwenda kukojoa hatimaye kibofu kikizoea kutunza, mtumiaji hatapata shida tena. Maji ni muhimu mwilini. Hata kiasi kidogo tu cha maji kinapopungua huchelewesha utendaji kazi kwa kiwango cha asilimia 3%.

Mara nyingi upungufu wa maji mwilini ndio hasa unaosababisha mtu kujisikia mchovu wakati wa mchana. Kipimo kizuri cha chini ni mtumiaji kuhakikisha ametumia kiasi cha lita moja ya maji kwa kila kilo 30 za uzito wake. Hii ina maana kama mtu ana kilo 60 za uzito basi anapaswa kunywa si chini ya lita mbili kwa siku ya masaa 24. Ili mtu ahakikishe kwa urahisi kuwa anatumia kiwango cha kutosha cha maji ni vyema akakagua rangi ya mkojo wake, mkojo unaofanana na mkojo wa mtu aliyenyeshewa mvua ni kipimo kisichobabaisha. Kama mhusika ataona mkojo wa rangi ya njano ajue wazi ana upungufu wa maji hivyo achukue hatua.


Utafiti unaonesha kuwa unywaji wa maji ya kutosha kila siku hupunguza hatari ya kupata ugonjwa wa kansa ya njia ya haja kubwa kwenye utumbo mpana kwa kiasi cha asilimia arobaini na tano, pia hupunguza uwezekano wa kupata kansa ya titi kwa asilimia karibu themanini (79%). Mtu huyu hukingwa pia kupata kansa ya kibofu cha mkojo kwa asilimia hamsini. Msomaji akijua haya ni dhahiri atafikiria kujikinga na hii ndiyo hatua ya awali ya kujiepusha na chanzo kikubwa cha magonjwa ya maumivu na mengineyo. Kuna magonjwa mengine pia yaweza kupoteza maji mengi na kuleta upungufu, kama vile kisukari na homa kali.


Madhara yaweza kuwa makubwa zaidi kwa watoto hasa wanapokuwa wamepungukiwa kiasi kikubwa cha maji kwa sababu ya maradhi. Baadhi ya athari ni kama kupata degedege, mtindio wa ubongo na taahira ya akili; shida ambazo ni za kudumu maisha yote. Matibabu yake ni maji, kama mtu amezidiwa inabidi apewe haraka moja kwa moja kwa njia ya mshipa katika hospitali.


Kimsingi hakuna athari ya matibabu haya. Lakini mtu akiona kiu akaamua kuondoa kiu kwa kunywa vinywaji vyenye caffeine ndani yake kama chai, cola, au kahawa anaweza kujisikia vibaya zaidi. Caffeine husababisha kukojoa zaidi, na kuifanya mishipa kuwa midogo kwa muda. Unywaji wa vinywaji hivi huua faida inayoletwa na maji.

No comments:

Post a Comment