Friday, February 20, 2009

2009 NJAA IMESHATUFIKIA !

2009-02-17 13:46:14 Na Mwandishi Wetu wa NIPASHE
Mkoa wa Kilimanjaro unahitaji tani za chakula 27,159 ili kukabiliana na uhaba wa chakula uliozikumba wilaya tatu za Mwanga, Rombo na Same. Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mohammed Babu wakati akitoa taarifa fupi ya mkoa huo kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye amewasili mkoani hapa jana mchana kwa ziara ya kikazi ya siku ya tatu. Pinda anamalizia maeneo ambayo hakufika baada ya kukatisha ziara yake ya Oktoba mwaka jana. Babu alisema kiasi hicho kitahitajika hadi ifikapo Mei, mwaka huu kwa ajili ya kaya 42,000 ambazo zimekumbwa na upungufu wa chakula. Hata hivyo, alisema tayari jumla ya tani 1,021 zimekwishapelekwa kwa walengwa. ``Serikali imeupatia mkoa chakula cha msaada tani 1,021 zikiwepo tani 970 za bei nafuu, yaani sh. 50 kwa kilo na tani 51 za bure kwa wasio na uwezo… Pia zimetolewa sh. milioni 61.5 kusafirisha chakula hicho kutoka SGR Arusha hadi wilayani,`` alisema. Akijibu maswali ya Waziri Mkuu kuhusu ujenzi wa barabara ya Rombo hadi Tarakea na hali ya kilimo katika kijiji cha Kirya ambacho yeye (Waziri Mkuu) alijitolea kuwa mlezi wake, Mkuu huyo wa Mkoa alisema kwamba ujenzi wa barabara hiyo unaendelea vizuri na sasa umefikia kiwango cha changarawe. Kwa upande wake, Waziri Mku alimweleza Mkuu huyo wa Mkoa kwamba, ameridhishwa na taarifa hiyo ambayo inaonyesha jinsi walivyo na msukumo mkubwa wa kilimo. Alimtaka Mkuu huyo aendelee na mipango waliyojiwekea kulingana na jinsi bajeti itakavyoruhusu. Kuhusu mpango wa Serikali kununua matrekta, Waziri Mkuu alisema inabidi wapange utaratibu wa kuyapata na kuyagawa kwani hayatakuwa ya bure. Leo, Waziri Mkuu anatarajiwa kwenda kukagua Skimu ya Umwagiliaji ya Lower Moshi, kutembelea Chuo cha Mafunzo ya Kilimo cha Kilimanjaro (KATC) na kuhutubia wananchi katika mkutano wa hadhara.

No comments:

Post a Comment