Sunday, February 22, 2009

MAKALA YA AFYA BORA NA. 7

Kutoka kwa Dr. Wilbert Bunini Manyilizu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Tanzania.

Article 7

UHARIBIFU WA AFYA KWA UCHAFUZI WA MAZINGIRA KWA KUCHOMA PLASTIKI

Watanzania wengi ni maskini. Hawawezi kuepuka matumizi ya plastiki. Plastiki huwasaidia katika kurahisisha shughuli zao. Lakini sayansi inaonesha kuwa plastiki yaweza kuleta athari kubwa katika jamii inayotumia ama kwa mtu mmoja mmoja au kwa jamii nzima iliyo karibu. Watu wakieleweshwa wanaweza kuepuka madhara makubwa kiafya yanayoweza kuletwa na matumizi mabaya au uharibuji wa plastiki hizi. Habari juu ya madhara yanayotokana na plastiki zinataka ushirikiano mkubwa kati ya wanasayansi, wanajamii, na wanasiasa. Jukumu la awali linabaki kwa msomaji kulifanyia kazi kwa nia ya kujisalimisha na kusalimisha afya za binadamu wenzie. Kuna sampuli nyingi za plastiki. Makundi makubwa mawili yanayojulikana ni yale ya plastiki ngumu na plastiki laini. Plastiki ngumu ni zile zilizotumika kama ndoo, sahani, beseni, kandambili, viatu, chupa za maji nakadhalika. Plastiki laini ni kama zile za mifuko ya rambo, ya maji yenye nembo ya uhai na mifuko laini inayofanana na hiyo. Msomaji anaweza kuhakikisha wingi wa plastiki hizi katika mazingira ya nyumbani, hata nje ya ofisi, na mabarabarani. Plastiki hizi zote zimezagaa mahali pengi hasa majalalani. Zinatumika sana kwa sababu ya bei zake nafuu, wakati mwingine hutolewa bila malipo kwa ajili ya kubebea mizigo midogo midogo dukani, sokoni, kando ya basi barabarani. Mabaki yake huja nyumbani, hubaki barabarani, na maporini. Mwisho wake ni kuchomwa kwa namna mbalimbali, wengine huwashia mkaa wanapotaka kupika, wengine huchoma pamoja na taka zingine jalalani na kubugia sumu yake bila kujua. Sumu hii nitaielezea kwa undani katika aya na makala zifuatazo.

Katika plastiki kuna sumu kali ambayo haitoki kama plastiki hii ikibaki bila kuchomwa. Sumu hii huitwa dayoksini. Jina la kisayansi kamili huitwa 2,3,7,8 tetrachlorodibenzo-p-dioxin. Hii sumu iko katika kundi la sumu kali duniani ziitwazo (Super toxin) hutokea tu kama zalio lisilotarajiwa (byproduct). Maana yake ni kwamba plastiki haikutengenezwa ili itoe sumu hii, bali sumu hii hujitokeza tu pale plastiki inapochomwa. Hakuna mtu anayeruhusiwa kuchoma moto katika nchi zilizoendelea, bali plastiki zote huchambuliwa na kuwekwa kwenye mapipa maalumu na kurudishwa kiwandani kuzungushwa tena au kuharibiwa katika mazingira salama.

Sumu hii inaaminiwa kisayansi kuwa ni mbaya sana, tena ni ya pili kwa ukali kati ya kemikali zinazotokana na kazi ya binadamu (man made organic chemicals), zenye madhara kwa afya na maisha ya binadamu. Sumu hii, kwa ubaya, inafuatia ile inayotokana na taka za aina ya radioaktivu (radioactive waste).

Tabia na madhara ya sumu (dayoksini) ya plastiki inayochomwa

· Sumu hii hujikusanya kwenye mwili.

· Sumu hii huenda kukaa kwenye chembe chembe za mwilini zenye mafuta, sumu hii hupenda mafuta.

· Sumu hii huenda kukaa kwenye kiini (nucleus) cha chembe chembe na kujichanganya na kuwa kama sehemu ya asili ya chembe chembe. Kumbuka kiini cha chembe ndicho kinachoongoza aina ya mtu aweje. Yaani ama awe mzungu, awe mhindi, afanane na baba au mama, chotara, mbilikimo, mwenye magonjwa na kadhalika

· Sumu hii hubadili tabia ya chembe ya mwili na kuifanya iwe na tabia inazotaka yenyewe zenye madhara kwa afya.

· Kwa sababu hubadili mchanganyiko wa asili wa kiini cha chembe chembe, sumu hii inaweza kuleta magonjwa ya kurithi katika familia

· Hupunguza kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali.

· Husababisha mimba kuharibika kabla ya muda wa kukomaa.

· Huleta magonjwa ya mfumo wa neva za fahamu.

· Husababisha ulemavu wa kuzaliwa nao, huleta madhara kwa mtoto anapokuwa angali tumboni, ikishindwa kumtoa kama njiti basi kiumbe hubaki na ulemavu mpaka anapozaliwa. Mfano, spina bifida ambapo mtoto huzaliwa bila mifupa kadhaa ya uti wa mgongo.

· Husababisha ugonjwa wa mfuko wa uzazi (endometriosis)

· Husababisha kujisikia mchovu tu siku zote bila sababu ya kueleweka (chronic fatique syndrome).

· Huleta magonjwa mbalimbali ya damu

· Husababisha kansa za aina mbalimbali.

· Huharibu homoni za mwili (Homoni ni kemikali nzuri za mwili ambazo hutengenezwa sehemu moja ya mwili na kusambazwa kwenye damu ili kurekebisha kazi za mwili ziende vizuri), mfano ili mwanamke awe na sauti ya kike, ngozi laini ya kike, sura ya kike na kadhalika lazima awe na homoni hizi za kike.

· Hali kadhalika ili mwanaume awe na ndevu, sauti ya kiume, misuli ya kiume na vinginevyo vya kiume lazima homoni ziwepo kwa ajili hiyo. Zikiharibiwa basi mume aweza kuwa na tabia ya kike, na mke aweza kuwa na tabia za kiume. Sumu hii yaweza kusababisha mambo haya.

· Huleta madhara kwa afya hata inapokuwa imeingia kiasi kidogo kwenye mwili.

· Hakuna kiasi maalumu ambacho mtu lazima akifikie ndipo aweze kupata madhara kiafya, kiwango kidogo tu chaweza kuleta shida kubwa.

· Mwili wa binadamu hauna kinga dhidi ya sumu hii.

· Kibaya kingine mwili hauwezi kuiharibu sumu hii kama unavyoweza kuharibu sumu zingine kupitia ini, tena inapoingia haitoki kwa haraka kupitia njia za kawaida za kuondoa sumu mwilini, kama figo.

· Husababisha ugonjwa wa ini lenyewe. Inaeleweka kuwa mtu hawezi kuishi bila ini, tena magonjwa ya ini mengi ni vigumu kuyatibu.

· Huharibu insinireta (incinerator), yaani nyumba maalumu inayotumika kuchomea taka.

· Inatishia afya na maisha ya binadamu lakini haijapewa kipau mbele.


3 comments:

  1. Greetings from Italy,good luck

    Hello,Marlow

    ReplyDelete
  2. Asante kwa haya. Twaendelea kufuatilia kuona sehemu ya nane inakuja na uelimishaji gani.
    Amani na Baraka kwako

    ReplyDelete
  3. This is one of the most incredible blogs Ive read in a very long time. The amount of information in here is stunning. Your blog is great for anyone who wants to understand this subject more.
    MHE leasing in qatar

    ReplyDelete