Sunday, March 8, 2009

SAKATA LA MATATIZO YA UMEME LINAENDELEA TANZANIA

Na Saed KUBENEA wa mwanahalisi, tanzania

KELELE za sasa ndani ya serikali kuhusu ununuzi wa mitambo ya Dowans ni jitihada zinazolenga “kukidhi maslahi binafsi,” MwanaHALISI limegundua.
Vyanzo mbalimbali jijini Dar es Salaam na mikoani vimeonyesha kuwa hakuna tatizo la umeme hivi sasa nchini; wala hakuna upungufu wa maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme.
Uchunguzi wa gazeti hili sasa unathibitisha kuwa madai ya serikali, kwamba nchi karibu itaingia gizani kutokana na ukosefu wa umeme, hayana msingi wowote.
Kwa wiki nzima sasa serikali, ikishirikiana na Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) wamekuwa wakitoa tahadhari kuwa iwapo mitambo ya umeme ya kampuni ya Dowans haitanunuliwa mara moja, taifa litaingia gizani wakati wowote kuanzia sasa.
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja amesema serikali ina nia ya kununua mitambo ya Dowans ili kukabiliana na tishio la uhaba mkubwa wa umeme kutokana na mabwawa kukauka.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Idris Rashid amesema kwamba mahitaji ya umeme yameongezeka nchini na kwamba kinachohitajika ni serikali kununua mitambo yote ya Dowans pamoja na vifaa vyote vya kuunganishia kwenye gridi ya taifa.
Hata hivyo, taarifa ndani ya TANESCO zinasema vyanzo muhimu vya nishati hiyo, ambavyo ni mabwawa ya maji, bado viko imara na maji yako kwenye viwango thabiti vya kuzalisha umeme.
Kwa mfano, hadi juzi Jumatatu, bwawa la Mtera mkoani Dodoma lilikuwa na maji ya kutosha ya kuzalishia umeme.
Kima cha juu cha ujazo katika bwawa la Mtera ni mita 698.50 na kina cha chini kwa ajili ya uzalishaji umeme ni mita 690.00. Lakini hivi sasa Mtera ina ujazo wa mita 695.91.
Hii ina maana kwamba kile kinachoitwa, “tishio la mabwawa kukauka,” hakipo katika bwawa hilo. Kinachoonekana kuwa upungufu, wataalam wamesema, hakiwezi kuleta athari yoyote kubwa katika miezi ya karibuni.
Hali kama hiyo ipo katika bwawa la Kidatu mkoani Morogoro. Hadi juzi Jumatatu, maji katika bwawa hilo yalikuwa mita 449.37. Kima cha juu cha maji kwa Kidatu ni mita 451.00 huku kima cha chini ni mita 441.00.
“Kwa maana hiyo, mpaka sasa, na kutokana na takwimu hizi, hakuna ushahidi wa mabwawa hayo kukauka au kuwa hatarini kukauka,” amefafanua injinia mmoja wa TANESCO makao makuu, Dar es Salaam.
Aidha, Mamlaka ya Hali ya Hewa imetangaza kuwa mvua kubwa zimeanza kunyesha katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Dodoma, Kilimanjaro na Tanga.
Wataalamu wa TANESCO wanasema ni mvua hizo ambazo zitajaza mabwawa ya Mtera, Kihansi, Nyumba ya Mungu, Kidatu na Hale kabla ya mwezi Machi na Aprili mwaka huu.
“Kwa mvua hizi zinazonyesha,” kimeeleza chanzo chetu cha habari, “huenda zikalazimu TANESCO kuachia kingo za mabwawa na kuachia maji yatoke ili kuzuia yasibomoke.”
Hadi Jumapili iliyopita, Waziri Ngeleja alikuwa ameanza kampeni kubwa akidai kuwa kununua mitambo ya kuzalisha umeme ya Dowans “siyo kufanya ufisadi” bali ni kuweka maslahi ya taifa kwanza.
Katika wimbo huo, Ngeleja aliungwa mkono na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe ambaye alisema anaweka mbele “maslahi ya taifa.”
Lakini ni Ngeleja aliyeliambia bunge, zaidi ya miezi mitatu iliyopita, kuwa serikali haiwezi kununua mitambo hiyo kwa kuwa imetumika na kwamba kufanya hivyo ni kukiuka Sheria ya Ununuzi wa Vifaa na Huduma serikalini ya mwaka 2004.
Katika haraka isiyo ya kawaida, serikali na TANESCO wametupilia mbali ushauri wa Kamati ya Nishati na Madini ya Bunge na kudandia Kamati ya Zitto wakidai wanatafuta bunge liwaruhusu kununua mitambo ya Dowans.
Kamati ya Nishati na Madini ilishauri TANESCO kufanya kile ambacho wanaona kimo katika uwezo na uamuzi wao. Dowans ni sehemu ya sakata la Richmond ambalo maazimio ya Bunge juu yake hayajatekelezwa na serikali.
Hata hivyo, bado serikali inakabiliwa na mgogoro wa nani hasa wajadiliane naye katika kununua mitambo ya Dowans iliyoko Ubungo, Dar es Salaam.
MwanaHALISI imebaini kuwa wakati kampuni ya Dowans ilikuwa inaweka mitambo yake na baada ya kuanza uzalishaji, haikuwa na ofisi nchini na wala mmiliki wake halisi alikuwa hajulikani.
Hadi sasa, Bunge ambalo liliunda Kamati Teule kuchunguza mkataba wa kampuni ya Richmond iliyokabidhi shughuli zake kwa Dowans, halifahamu mmiliki wa Dowans.
MwanaHALISI imegundua kuwa kuna kampuni inayoitwa Dowans Holdings SA (DH-SA) iliyosajiliwa nchini Costa Rica, Amerika ya Kusini, tarehe 1 Julai 2005 na kwamba ndiyo yenye uhusiano na Dowans iliyoko Ubungo.
Kampuni ya DH-SA ilianzishwa na mtu mmoja aitwaye Bernal Zamora Alce. Taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ambazo gazeti hili limeona, zinaonyesha Zamora alisajili Dowans na makampuni mengine 99 yanayoishia na herufi “SA,” kwa siku moja.
Taarifa zinasema kati ya makampuni hayo 100, Zamora alijitangaza kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi katika makampuni 52.
Hata hivyo, pamoja na utitili huo wa makampuni, imefahamika kuwa Zamora hana simu ya mkononi, hana sanduku la barua wala hajulikani mtaa anakoishi.
Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa habari wa kimataifa na wanasheria mashuhuri nchini Costa Rica umegundua kwamba kampuni ya Dowans haikuwa na ofisi nchini humo haikuwa na simu wala gari.
Si nchini Costa Rica tu, bali kampuni ya Dowans yenye mitambo Ubungo, kwa mujibu wa taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza Richmond, haikuwa na namba za simu wala ofisi; wafanyakazi wake walikuwa wanatumia ofisi za kampuni ya Caspian Limited hapa nchini.
Kampuni ya Caspian inamilikiwa na mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz. Ni Rostam aliyethibitishia Bunge kuwa Dowans ilikuwa inatumia anuani zake.
Katika andishi lililotumwa serikalini na Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Costa Rica, kuitahadharisha serikali ya Tanzania kuhusu Dowans anasema, “Dowans ni kampuni ya mfukoni iliyoanzishwa mahususi kwa ajili ya kufanya kazi maalum.”
Katika mazingira haya, Dk. Rashid alipoulizwa TANESCO inajadili na nani kuhusu ununuzi wa mitambo, alijibu haraka kuwa wao hawafanyi majadiliano bali wamepeleka mapendekezo serikalini. Alisema ni serikali yenye jukumu la kununua au kutonunua mitambo hiyo.
Alipoulizwa sasa serikali itajadiliana na nani wakati mmiliki wa Dowans hajajulikana, Dk. Rashid alisema, “Hayo si yangu. Ni mambo ya wanasiasa. Sisi tumetoa ushauri kwa serikali kwamba tunataka mashine za kuzalisha umeme…”
Alipoulizwa kwa nini TANESCO isishauri serikali kutaifisha mitambo ya Dowans, kwa hoja kwamba kampuni hiyo ilitapeli serikali kwa kurithi mkataba wa Richmond kienyeji alisema, “Hilo siwezi kulizungumzia.”
Waziri Ngeleja hakupatikana kujibu swali kwa nini TANESCO inataka serikali kufanya mazungumzo na Dowans badala ya kuingia katika mchakato wa zabuni.
Chanzo: Gazeti la Mwanahalisi 07-02-2009


No comments:

Post a Comment