|                |               |       Prof.     Possi        |             “Kampeni   ya kuhamasisha usawa wa jinsia, imeanza kupoteza mwelekeo. Baadhi ya watu   wanachochea ushindani kati ya wanawake na wanaume badala ya kuhamasisha   ushirikiano kati yao,” anasema Profesa Mwajabu Possi. Profesa Possi   ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya mawasiliano na uandishi wa habari ya Chuo   Kikuu cha Dar es Salaam, anasema ipo tofauti kubwa kati ya harakati za   kupigania usawa wa jinsia na harakati za kupigania haki na ukombozi wa   mwanamke yaani “feminism.”     Anasema usawa wa jinsia una maana ya uhusiano kati ya mwanamke na mwanamume.   Uhusiano huo unalenga katika shughuli za maendeleo ya kijamii, kiuchumi na   kisiasa na kwamba kampeni ya usawa huo inapaswa kushughulikiwa kwa   ushirikiano kati ya wanaume na wanawake. Anaeleza kuwa Feminism ni harakati za   kupigania haki za wanawake.     Anafafanua kuwa ufanisi wa harakati hizo umewezesha kuanzishwa mkakati wa   kupigania usawa wa jinsia. Harakati za kupigania usawa wa jinsia zinatokana   na chimbuko la harakati za kupigania haki za wanawake ambapo makundi mbalimbali   ya wanawake wa magharibi yaliibuka karne ya 20 na kupinga unyanyasaji,   ukandamizaji na udhalilishaji dhidi ya wanawake.     “Wakati ule wanawake walikuwa wanakandamizwa. Hawakuwa na haki ya   kupiga kura, kupata elimu wala kazi bora…Mali na madaraka yote yalishikwa   na wanaume. Hali hiyo iliwalazimu wanawake kuunda vikundi vya kutetea haki na   ukombozi wa wanawake. Kwa kuwa vikundi hivyo vilikuwa vya wanawake pekee,   ilionekana kama ni mambo ya kike,” anasema Possi.     Anaendelea kusema, “hata hivyo suala hilo limeanza kupoteza mwelekeo na   tafsiri ya feminism imebadilika… Badala ya kutetea haki za wanawake,   baadhi ya wanawake wenye uwezo wanataka kutumia fursa walizonazo kuwanyanyasa   au kushindana na wanaume.” Kinachofanyika katika Siku ya Wanawake ni   kujenga usawa wa jinsia kwa kujadili na kutathmini maendeleo na changamoto   zinazowapata wanawake, kwa kuwa waliachwa nyuma na kubaguliwa kwa miaka   mingi.     “Siku ya leo ni mahsusi kupima maendeleo ya kujenga usawa kwa kuwapatia   wanawake fursa na haki sawa katika elimu, madaraka, kazi na huduma   mbalimbali… Maendeleo hayo hayawahusu wanawake pekee… Utekelezaji   wake unapaswa kufanyika kwa ushirikiano kati ya wanawake na wanaume,”   anaeleza. Anawahimiza Watanzania kuondokana na ‘mawazo mgando’ na   kushirikiana kuendesha kampeni ya kukuza usawa wa jinsia badala ya kuibeza   kwa kuwa athari zake zinafifisha maendeleo ya taifa.     “Suala la usawa wa jinsia ni muhimu, hatuna haja ya kuvutana…Ni   kweli wanawake walibaguliwa katika elimu na kunyimwa fursa za kufanya uamuzi.   Ukatili na uonevu dhidi ya wanawake vinaendelea hadi hivi sasa ukiwamo   ubakaji, mauaji ya vikongwe na walemavu…. Haya ni mambo mazito   yanapaswa kukemewa na wanaume na wanawake,” anaeleza. Ingawa anasema   suala la usawa wa jinsia ni changamoto kwa jamii mbalimbali hasa katika nchi   zinazoendelea kwa kuwa zinakabiliwa na umasikini, kuna uwezekano wa kufanya   mabadiliko.     Anafafanua kuwa mabadiliko hayo yanaweza kufikiwa kwa haraka kama wanawake   wataweka mikakati ya kujiendeleza kielimu na kushika nafasi mbalimbali za uongozi   badala ya kubweteka na kulewa madaraka. Wapo wanawake wenye uwezo wa   kujiendeleza kimasomo lakini hawafanyi hivyo. Mtu akipata cheo kidogo,   anaridhika na kutumikia cheo hicho kwa muda mrefu bila kujiendeleza kielimu,   pia wapo wanaobweteka kutokana na madaraka ya waume zao.     “Pia kuna wanawake ambao wanapata fursa ya kujiendeleza kimasomo lakini   hawajitumi ipasavyo au wengine wanaogopa changamoto za wanaume…Mfano   wanafunzi wengi wa uandishi wa habari wanapenda utangazaji badala ya kuandaa   vipindi. Jambo hili linatoa fursa kwa wanaume kujiona kuwa ni bora kuliko   wanawake,” Possi anaeleza. Possi ni miongoni mwa wanawake ambao   wamejitahidi kujiendeleza kimasomo, kufanya kazi kwa bidii na kushika nafasi   zinazowawezesha kufanya uamuzi bila kusubiri nafasi za upendeleo.     Possi, ambaye kitaaluma ni mwalimu, alianza kazi akiwa na elimu ya stashahada   na kufundisha katika sekondari mbalimbali nchini kabla ya kujiunga na Chuo   Kikuu cha Dar es Salaam kusomea shahada ya ualimu na kisha kufanya kazi   Wizara ya Elimu. Possi hakuridhika na nafasi hiyo, mwaka 1981 aliamua kurudii   katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuchukua Shahada ya Uzamili katika fani   ya ualimu. Alihitimu elimu hiyo mwaka 1985. Ufanisi wake katika masomo   ulimwezesha kuwa mhadhiri wa chuo hicho.     Alifanya kazi kwa miaka mitatu na kuamua kwenda kuongeza elimu na ujuzi ili   aweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Mwaka 1987 alijiunga na Chuo Kikuu cha   Ball State, kilichopo Indiana na kusoma shahada ya uzamili ya ualimu katika   elimu maalumu kwa watu wenye ulemavu na kisha akajiunga na shahada ya uzamivu   katika Chuo Kikuu cha Ohio, ambapo alisoma saikolojia katika elimu maalumu.   Baada ya kumaliza masomo hayo, Possi alirudi kufanya kazi Chuo Kikuu cha Dar   es Salaam. Kati ya mwaka 1994 na 1999 alifundisha masomo ya Saikolojia katika   chuo hicho akiwa mkuu wa Idara ya Saikolojia.     Desemba 1999, alichaguliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania,   nafasi iliyomwezesha kufanya uamuzi mzito katika mchakato wa kukifanya chuo   hicho kuwa na hadhi ya Chuo Kikuu. Kutokana na utendaji wake mzuri, mwaka   2004 Possi aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Mawasiliano na Uandishi   wa Habari iliyopo chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nafasi anayoitumikia   hadi sasa.     “Kwa kushirikiana na wafanyakazi wenzangu tumefanikiwa kukifanya chuo   cha uandishi wa habari kuwa taasisi ya Chuo Kikuu, tumeanzisha kituo cha   kurushia matangazo cha Redio Mlimani, kituo cha Televisheni Mlimani na gazeti   la Hill Obsevers,” Possi anaeleza. Possi, ambaye amekulia katika   familia yenye malezi ya Kiislamu, alifanikiwa kujiendeleza kimasomo hata   baada ya kuolewa. Anasema ufanisi alionao unatokana na ushirikiano na   maelewano mazuri kati yake na mume wake.     “Kamwe nisingefikia hatua hii kama mume wangu asingekubali kubaki na   watoto wakati nilipokwenda masomoni nje ya nchi….Hiki ni kielelezo kuwa   usawa wa kijinsia ni kati ya baba na mama katika familia…Na mwanamke na   mwanamume katika sehemu za kazi,” Possi anasisitiza. Amewataka   Watanzania kuachana na dhana potofu kwa kudhani maadhimisho ya Siku ya   Wanawake yanawahusu wanawake pekee na kuwataka wanaume washiriki kikamilifu   ili kuongeza kasi ya maendeleo.       |   
 
No comments:
Post a Comment