Monday, March 2, 2009

MAKALA YA AFYA BORA NA. 8

Article No. 8 kutoka kwa Dr. Wilbert Bunini Manyilizu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Tanzania.

Tarehe 2 Machi, 2009.

Mwendelezo wa article No 7

Mfululizo wa matukio tangu kuchoma plastiki hadi afya kuharibika

Sumu ya dayoksini hutengenezwa tu pale plastiki inapochomwa. Plastiki inapokuwa inaungua ndipo sumu hiyo hutokea kama mvuke au moshi. Moshi huu huingia kwenye pua ya yeyote aliyepo karibu hata yule wa mbali atakayefikiwa. Huvutwa na kuingia mapafuni ambapo huziingia chembe chembe mbalimbali zenye asili ya kuwa na mafuta (adipose tissues). Hunata kwenye chembe chembe hizo, na hatimaye kuingia ndani ya chembe chembe katikati kabisa kwenye kiini cha chembe chembe (nucleus). Hapa hujichanganya na kujifanya sehemu asilia ya chembe chembe hizo. Chembe chembe asilia za binadamu zina kazi za kuendesha mambo yote ya kifiziolojia (kiutendaji), chembe hizi zinapokuwa zimevamiwa na sumu hii huanza kubadilishwa tabia na utendaji wake wa kazi na kuanza kufanya kazi zingine ambazo zinakuwa zimetumwa na huyu mgeni aliyejichanganya, na huanza kuzalisha magonjwa ambayo yametajwa kidogo hapo awali (article 7) na mengine katika aya zifuatazo.

Moshi wa sumu ambao haukuingia kwenye pua za watu hupeperushwa kwenye hewa mpaka umbali wa kilomita mamia kama vipeperushi vidogo sana. Sumu hii inakofikia hunata kwenye majani ya mimea na mazao mbalimbali. Ng’ombe, mbuzi, nguruwe na wanyama wengine wanapochunga hutumia sumu hii, nayo huwaingia na kutuama kwenye chembe chembe zenye asili ya kuwa na mafuta katika miili ya wanyama hawa. Sumu nyingine inayopeperuka huishia kwenye miti, maziwa (lakes) na bahari na vyanzo mbalimbali vya maji. Huko nako kuna wanyama kama samaki na wadudu wengine, hawa nao hupata dozi ya sumu na kukaa nayo katika chembe chembe za mafuta. Siku nyingine mtumiaji wa samaki, nyama, maziwa yenye mafuta (creamy) hupata sumu hii kupitia mzunguko huu. Hapa madhara ya sumu hii huja kwa binadamu. Hii ni kwa sababu sumu hii haiharibiwi na aina mbalimbali za mazingira nje na ndani ya wanyama na binadamu.

Sumu hii inapokuwa sehemu ya kiini cha chembe chembe huanza kuharibu mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa. Kwa sababu chembe chembe nyeupe (maaskari wa mwili dhidi ya magonjwa) za ulinzi hulewa sumu na dawa inayotengenezwa kushindana na maadui wageni pia hupungua. Mfumo wa uzazi wa kawaida huharibiwa, hamu ya kufanya mapenzi hupotea (loss of libido). Sumu hii hupunguza uwezo wa uzazi na kupoteza uwezo wa kuchukua mimba mpaka miezi tisa, nyingi hutoka kabla ya hapo. Watoto wa kiume wanaobahatika kuzaliwa huwa na homoni za kiume kidogo kuliko kawaida, na baadaye huwa na uwezo mdogo (kutokana na kuwa na kiwango kidogo cha homoni ya testosterone) wa kuzalisha mbegu za kiume za uzazi. Watoto huwa hawana uwezo pia wa kutosha katika masomo (learning disabilities) kwa sababu ya sumu hii. Makuzi ya watoto kama ndiyo waathirika huvurugwa, kwani tezi ya makuzi (thyroid gland iliyoko mbele kwenye shingo) huathirika kwa sumu, neva za fahamu huharibiwa. Sumu hii huleta kansa katika dozi ndogo sana inayoweza kudhaniwa haiwezi kuleta madhara. Sumu hii huwa na tabia ya kuhamasisha uanzishaji wa chembe kichaa za kansa (potent cancer promoter) kwa sababu huzibadili tabia homoni zinazohusika na kukua.

Kukua kwa mtu maana yake ni kugawanyika na kuongezeka kwa idadi ya chembe chembe na kukua kulingana na zile za awali. Sumu huzifanya chembe chembe hizi ziwe nyingi isivyo kawaida badala ya kugawanyika na kuzikuza kwa kawaida mtu aonekane kaongezeka (yaani kakua), zenyewe huzifanya zigawanyike zikiwa chembe mbovu zenye kichaa (zenye tabia isiyorekebishika) zinazozaa haraka kuliko kawaida; hizi ndizo zinazoitwa chembe chembe za kansa. Hivi ndivyo sumu ya dayoksini inavyoweza kusababisha aina mbalimbali za kansa katika kiungo chochote ambacho huwa kina tabia ya kukua.

Habari za utafiti katika wanyama

Utafiti uliofanywa kwa wanyama wa porini waliopewa sumu hii kwa kiwango kidogo sana unaonesha kuwa walipata kansa za viungo mbalimbali zikiwemo kansa ya ini, tezi za adrena, thairoidi, kansa ya ngozi, mapafu, pua na kinywa. Kinga dhidi ya magonjwa iliharibika kwa maisha yote, pale ilipojaribiwa kwa wanyama wenye mimba kwa kutoa sumu hii dozi moja kwa kiasi kidogo mimba ziliharibika. Kuondoa tatizo hili katika jamii za kimaskini, inahitaji nguvu ya kutosha na ushirikiano katika nyanja mbalimbali, kuanzia mtu binafsi, jamii, sekta kama za afya, mazingira na wanasiasa. Tatizo likionekana ni tatizo kwa wote ndipo nguvu inaweza kuelekezwa huko. Kama msomaji anaweza kuona hili naamini hawezi kukaa kimya, na huu ndio mwanzo wa mapambano dhidi ya adui maradhi. Mwanafunzi mzuri hahitaji kusubiri mwalimu aje amwanzishie uelewa na utekelezaji bali mwalimu humsaidia kurahisisha kuelewa. Msomaji anaweza kufanya kitu hapo alipo, ili mradi tu aepuke kuahirisha. Inawezekana.

No comments:

Post a Comment