Tarehe 25 Februari, 2009 tulitembelea Mahakama Kuu ya Rufaa ya Shirikisho la Marekani (Federal Supreme Court) ambayo ndio mahakama ya juu kabisa ya rufaa nchini humu, iliyopo kati ya First Street na Second Street, Washington DC., U.S.A. Mji huu, ambao serikali yake ya Mtaa huuita Washington Metropolitan Authority (hauitwi city wala manispaa) una wakazi wanaokisiwa kuwa 600,000 kwa mahesabu ya mwaka 2008.
Jambo la kwanza kuliweka wazi katika mhimili huu wa Dola ni kuwa Majaji wa Mahakama Kuu nchini humu hawana umri wa kustaafu. Hivyo Jaji anapoteuliwa kufanya kazi hiyo ni ya umri wake wote uliobaki hadi ashindwe mwenyewe, mathalan kiafya.
Kwa upande wa Mawakili wa Mahakama hii ya juu kabisa nchini Marekani, sifa yao ni kuwa ni lazima wawe wametumikia wadhifa huo wa uwakili (baada ya kupasi Mitihani ya American Bar Association) kwa miaka mitano. Baada ya hapo wanaomba kwa Mahakama hiyo kuwa Mawakili wa Mahakama hii. Wanapokubaliwa ndio wanatambulishwa rasmi kuwa ni Mawakili wa Makama ya Rufani ya Shirikisho. Siku tulipokuwepo, walitambulishwa Mawakili zaidi ya 10 wa Mahakama hiyo. Hiyo maana yake ni kwamba, kuanzia utambulisho wao huo, sasa wanaweza kuwakilisha wateja katika Mahakama hiyo. Wamekuwa Maofisa wa Mahakama ya Rufani ya Shirikisho.
Katika nchi hii ya Marekani, Katiba yao inaruhusu sana Utaratibu wa Mizani ya Dola (checks and balances) ndio maana majaji wao majimboni wanachaguliwa na wananchi kwa kura, na kisha kumuachia Gavana wa Jimbo kuteua, na Bunge lake kuidhinisha. Na vivyo hivyo Majaji wa Mahakama ya Shirikisho huteuliwa na Rais wa Marekani na kuidhinishwa na Bunge (senate). Kwa maana hiyo, Rais anakuwa si mwenye kauli ya mwisho juu ya uteuzi wa Majaji nchini humu, tofauti sana na nchi kwetu Tanzania ambako Rais huteua Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa; japo hana uwezo wa kuwaondoa kikatiba, anao uwezo wa kuwahamisha atakavyo. Na kuhamishwa kwa Jaji hakuna tofauti na kuondolewa kwa sababu kwa kipindi chote atakachokuwa amehamishwa, hataweza kufanya kazi zake kama Jaji wa Mahakama.
Tulipata fursa ya kusikiliza kesi iliyotoka Hawaii iliyohusu masuala ya Ardhi. Katika Nakala ya Kesi hii kutoka mahakama za chini, kumetolewa maelezo kwa mfano kwamba mwaka 1898 Wamarekani walipoivamia nchi ya Hawaii ilikuwa na watu zaidi ya laki nne (400,000) ambao hadi kufikia miaka thelathini baadaye, walibaki 78,000 tu kutokana na ukandamizaji waliopitia wa Wamarekani.
Mambo niliyoweza kuyashuhudia katika Mahakama hiyo ya juu kabisa nchini Marekani ni kama yafuatayo:
1. Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi za kutoka majimboni, ambazo zimeamuliwa kwa kutumia sheria za majimboni huko tu. Mahakama za rufaa za mwisho kusikiliza kesi hizi ni Mahakama za Rufaa za Majimbo husika (State Supreme Courts).
2. Kuna Waheshimiwa Majaji tisa wa Mahakama hii wanaokaa kwa wakati mmoja. Katika idadi iliyokaa siku hiyo, kulikuwa na Mwanamama mmoja Mheshimiwa Jaji Ruth Bader Ginsburg. Mama huyu alituacha hoi kwa kuongoza kuuliza maswali kwa sababu ni majuma matatu tu nyuma yake alitoka kufanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe hatari (malignant tumour) tumboni mwake.
3. Waingiapo Majaji hawa Mahakamani, wanatumia utamaduni wa Kiingereza wa Karani kuita "Court Rise!!!!!" Lakini yeye alitumia maneno yanayofanana na hivyo wote tuliokuwamo tukasimama kwa heshima yao.
4. Lakini wakati wa kumaliza kusikiliza kesi hiyo, waheshimiwa majaji hawakutoka nje. Walibaki vitini, ila sisi wasikilizaji na waandishi wa habari ndio tuliotoka tukiwaacha Waheshimiwa ndani.
5. Pia Washeshimiwa Majaji wana uhuru wa kumtupia maswali msemaji wa wakati huo; awe mshitaki au mshitakiwa (au mawakili wao). Jambo hili nimeona geni sana kwani Tanzania Majaji husikiliza tu hoja zitolewazo toka pande mbili.
6. Chumba cha Mahakama hii ya juu kabisa nchini Marekani sio kikubwa kama nilivyofikiria. Ni kama chumba cha kuweza kuketi watu 300 hivi kwa makisio. Nilitaraji kuwa Mahakama hii ingekuwa na chumba kikubwa zaidi ya hiki.
7. Kuna ulinzi mkali sana katika jengo hili kuanzia nje hadi ndani. Kwa wasikilizaji wa kesi, kila itokeapo kesi hutakiwa kusimama foleni nje kadri watu wafikavyo. Ifikapo saa 3.00 asubuhi ndio askari huruhusu watu kuingia katika chumba cha kuchunguza usalama na kisha chumba cha kuchunguzwa usalama tena kabla ya kuruhusiwa ukumbini.
8. Hairuhusiwi kuvaa makoti wala kofia Mahakamani. Vyote hivi huhifadhiwa katika chumba maalum kabla ya kuingia. Chumba cha hifadhi kila vikabati ambavyo msikilizaji anatakiwa kulipia $0.25 (senti ishirini na tano ambazo kwa Tanzania ni kama Tshs.250/=) ili upate kuvihifadhi vifaa vyako kwa usalama zaidi. Na kila ukitaka kufungua kikabati hicho (Locker), inakubidi ulipie $0.25 nyingine. Mimi yalinikuta kwa sababu nilisahau kuvua kofia baada ya kufunga kikabati. Nikatakiwa kurudi kuhifadhi kofia. Ndipo nikakuta nalazimika kutoa senti ishirini na tano nyingine ili nifungue tena. Nikasema kwa hili tu basi Mahakama Kuu hii inajipatia mamilioni kwa mwaka. Mahakama hii kwa nchi hii huwa inakaa kwa siku tatu kwa kila wiki na kila mwezi isipokuwa wanakuwa na likizo muda fulani tu. Kwa hiyo huduma ya Mahakama hii ni kama ofisi nyingine. Tofauti kwa mfano na Tanzania ambako nadhani Mahakama ya Rufani haikai kwa ratiba ya kila wiki kama hii.
Kiongozi wetu katika msafara huu alituarifu kuwa Mahakama hii ni katika majengo mapya eneo lile (kati ya majengo ya mihimili mikuu ya dola). Amesema jengo la Mahakama lilikamilika ujenzi mwaka 1935. Jirani na Jengo hili kuna Maktaba Kuu ya Wabunge wa Marekani (Library of Congress, ambayo ina majengo makubwa matatu; Madison Bldg., Jefferson Bldg., na Adams Bldg.) na linatazamana na Bunge la Marekani (Capitol Hill). Majengo yote haya yapo katika Mji Mkuu wa Serikali ya Marekani, yaani Washington District of Columbia (DC). Mji mkuu wa biashara katika nchi hii ni New York City, ulio kaskazini ya huu.
Karibu DC Dada
ReplyDelete