Thursday, August 16, 2012

WATANZANIA HAWATAENDELEA KUPITIA UJINGA ENDELEVU !!!




Rai ya Jenerali
Hatutaendelea kupitia ujinga endelevu
NIMEKWISHA kueleza udhaifu wa mfumo wo wote unaowategemea akina Pangloss kama wanafalsafa wake; mfumo huo hauwezi kupiga hatua kwenda mbele kwa sababu umeshibishwa na fikra za kuridhika kusikokuwa na msingi.
Si mfumo unaoweza kuangalia nje ya mipaka yake na kubaini kwamba iko mifumo mingine iliyo bora kuliko huo uliopo, na kwamba mifumo hiyo siyo tu inawezezekana bali ndiyo inayotakikana.
Niombe radhi kwa kunukuu msemo mwingine wa Kihaya: Akaana katakyaara kati mawe achuumba. Tafsiri yangu: Mtoto asiyetembeatembea humsifu mama yake kuwa mpishi bora kuliko wote.
Maana yake ni kwamba jamii ambayo imebweteka nyumbani na isisafiri kwenda nje kuona jamii nyingine zinavyofanya kazi itakuwa daima ni jamii inayoamini kwamba inachofanya ndicho bora  kuliko cho chote kinachofanyika kwingine ko kote. Na ndivyo alivyofundisha Profesa Pangloss.
Sasa, haiwezekani kusema kwamba wakuu wa nchi hii hawasafiri kwenda ughaibuni kwenye maendeleo kuliko yetu. Kusafiri wanasafiri sana, na karibu kila wanakokwenda ni nchi zilizo na maendeleo makubwa sana kuliko tuliyo nayo hapa kwetu.
Hata katika nchi za dunia ya tatu, baadhi yake zimepiga hatua kubwa katika maeneo ambayo bado yanatutatiza hapa.  Na sisi wengine tusiokuwa viongozi (kwa maana hiyo) tumesafiri ya kutosha, kote duniani, na tumejionea jinsi wenzetu wanavyofanya.  Kwa hiyo taabu iko wapi?
Taabu kubwa inatokana na kwamba tumefanikiwa (kama hilo ndilo neno mwafaka) kujenga jamii ya watu wasiotaka kujifunza. Kwa maoni yangu tumejifikisha mahali ambapo kila mtu anadhani anachojua kinamtosha na hana haja ya kujifunza kitu kingine. Tumekataa, au tumeshidnwa, au hatujui namna ya kujenga jamii yenye kujifunza (a learning society). Matokeo yake ni kwamba tumezama ndani ya ujinga endelevu, ambao naueleza hapa chini:
Katika lugha ya Kiingereza kuna maneno kadhaa yanayoeleza hali ya kutokujua, ujinga na upumbavu. Nitalichukua mojawapo, “ignorance”, ambalo maana yake tuliyoizoea ni “ujinga.”  Tuliwahi kueleza “ujinga” kama kutokujua kusoma na kuandika, na katika miaka ya kwanza baada ya Uhuru tulifanya kazi ya kuutokomeza kwa “kisomo cha   ngumbaru,” kama kilivyoitwa.
Lakini kutokuweza kusoma na kuandika si ishara pekee ya ujinga. Ni kweli kilema hicho ni muhimili muhimu katika ujenzi wa ujinga, kwa sababu katika ulimwengu wa leo haiwezekani kuondokana na kutokujua bila kuondokana na kutokujua kusoma na kuandika.
Kujua kusoma na kuandika ndio msingi mkuu wa kujenga mazingira ya kuja katika zama zetu, na ndiyo silaha kuu ya kupambana dhidi ya kutokujua. Lakini kujua kusoma na kuandika pekee hakuiondolei jamii ujinga, kwa sababu msingi huo  unaweza ukakaa bila kutumiwa kujengea jengo lo lote la maana, na silaha hiyo inaweza ikaachwa ikaota kutu ilhali adui bado anatishia.
Ili msingi ule niliouzungumza uwe na maana kwetu hauna budi kutumika kwa kuinua jengo juu yake, na jengo hilo ni ujuzi endelevu usiokoma, usiokuwa na mipaka, unaokwenda milele mbele ukitafuta ujuzi mwingine kwa kujisaili na kujikosoa siku zote. Hii ndiyo maana ya elimu endelevu, hali inayompa mwenye nayo uwezo na ari ya kuvumbua sayari mpya za ujuzi kila uchao, asikubali kuridhika na kile anachokijua kwa sababau hata kile alichokijua jana kama elimu, inawezekana leo si elimu tena kwani kimepitwa na wakati. Huu ni upande mmoja wa diameta, upande wa ujuzi endelevu.
Upande mwingine wa diameta ni ule wa ujinga endelevu, si tu ujinga wa kutojua kusoma na kuandika. Kwa hakika, wakazi wa upande huu wanaweza kusoma na kuandika, tena sana, na wanaweza kufanya hisabati za Pitagora, Kopeniki na Galileo; lakini bado ni wajinga kwa sababu wanaamini kwamba walipofikia ndio mwisho wa ujuzi, mbele hakuna jipya.
Wakati mwingine, kwa sababu ya ujuzi kidogo walio nao, wanakuwa watetezi wakubwa wa msimamo wa kutokubali ujuzi mpya kwa sababu ujuzi uliopo wanauona kama usiopingika na unaotosheleza. Ndio akina Pangloss.
Nimesema hapo juu kwamba wakuu wetu wanasafiri, tena wakati mwingine mpaka inachusha. Nasi pia tunasafiri sana. Sote tunaosafiri si  vipofu; tunaona vyema jinsi wenzetu walivyopiga hatua za maendeleo hata katika maeneo ambayo hata sisi tunayamudu. Lakini kwa sababu hatutokani na jamii ya kujifunza (a learning society) hatuyaoni hayo, na tukiyaona kazi yetu ni kustaajabu “mdomo wazi” na kusifia; si kuiga au kujifunza.
(Hapa nimetumia neno “kuiga” kwa makusudi kabisa, kwa sababu katika mazoea yetu, neno hili tumelidhalilisha mno. Tunaambiwa “mambo msiige,” na “msiiige ya wengine,” au ”iga ufe.”  Ajabu yake ni kwamba neno “kuiga” katika lugha nyingi za ki-Bantu nilizozipitia lina maana ya “kujifunza.” Sasa, tunaposema “mambo msiige maana yake ni nini? Tusijifunze? Mimi nasema, iga upone).
Katika madaraja ya ujinga lipo moja ambalo mimi ninaliita daraja la “ujinga endelevu”. Waingereza wanaiita hali hii “obscurantism, ” si tu kwamba ni ujinga, bali ni ujinga wenye msimamo mkali, usiopenda kukosolewa hata kidogo, na ambao aliyeathiriwa nao yu radhi afe kuliko kukubali kuachana nao, na atapigania haki yake ya kuwa mjinga hadi kifo. Huu ndio ujinga endelevu, ujinga ngangari. Obscurantism.
Obscurantism ndiyo inawafanya watu wapambane na teknolojia mpya, kama kompyuta. Walikuwapo watu Uingereza katika karne ya 18 walioitwa Luddites, ambao shughuli yao ilikuwa ni kuvunja mashine, ambazo zilikuwa zinaanza kujitokeza katika mapinduzi ya viwanda, ambazo waliziona kama karakana za shetani, na leo bado tunao katika sura nyingine.
Mkuu mmoja wa Bunge aliwahi kumwambia mbunge aachane na tabia ya kuleta bungeni taarifa za “kuokoteza kutoka internet,” lakini baadaye taarifa hizo zikaja kuwa za maana mno.
Katika uwanja wa siasa tunao obscurantists wengi mno, akina Pangloss amabao hawaamini kwamba kuna haja ya kuandika katiba mpya kwa sababu hii tuliyo nayo inatutosha, na kila tunapokuwa na tataizo tunabandika na kubandua vifungu; akina Pangloss wanaotuambia kwamba kutaja udhaifu wa rais ni sawa na uhaini; akina Pangloss wanaotaka tuamini kwamba majaji wetu wote ni malaika, wakati kila mtu anajua kwamba  asasi nambari wani kutajwa katika taarifa zote kwa kugubikwa na rushwa ni mahakama. Wako kila mahali.
Ili tuendelee tunahitaji vitu kadhaa, na baadhi yake vilikwisha kutajwa tangu enzi za Azimio la Arusha. Chini ya vipengele vitatu vinavyofuata baada ya Ardhi, tunahitaji kuambatanisha maelezo mafupi:
Watu: Watu wakweli, wanaoambizana ukweli, wasioficha wanachohisi, wanaodadisi kila wanachokiona au kukisikia; watu waongofu, wanaochukia na kupambana na rushwa, ufisadi, unafiki, udhalimu,ubinafsi, uroho, ubabaishaji na uongo.
Siasa safi: Siasa inayosimamia maslahi ya wananchi, na si maslahi ya wageni na vibaraka wao; siasa inayokataa ubazazi na biashara ya kununua na kuuza kura; siasa inayojali utu wa mtu si kitu alicho nacho; siasa ya ukombozi wa Mtanzania na Mwafrika.
Uongozi bora: Uongozi unaotokana na sifa za mwananchi aliyeaminiwa na wenzake kutokana na sifa hizo na si fedha za kuhonga, uadilifu wake, uaminifu wake, na uwezo wa kutumikia watu wake na si kujitumikia na kujinufaisha yeye binafsi na familia yake.
Bila hayo, tunaweza kuzikiri uchi usiku na mchana, hatutapata maendeleo ng’o! Na akina Pangloss watakuwa na ajira nzuri tu, ya kujaribu kutushawishi kwamba, kinyume na tunavyojionea sisi wenyewe, tumepiga hatua kubwa kuelekea kwenye ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment